The House of Favourite Newspapers

NECTA Kuvifuta Vituo vya Mitihani Vitakavyofanya Udanganyifu

0
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde.

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA), limetishia kuvifutia usajili vituo vyote vya kufanyia mitihani ya Darasa la Saba inayotarajiwa kufanyika kesho Jumatano Septemba 6 na Alhamisi, Septemba 7, 2017 nchini kote.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde wakati akizungumza na wanahabari Makao Makuu ya NECTA, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

“Baraza linawataka wamiliki wa shule zote kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya kufanyia mitihani, hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani hiyo.

“Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litabaini na kuthibitisha pasina shaka kuwa kituo hicho kinajihusisha na udanganyifu wa mitihani. Tunatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kipindi hiki cha ufanyikaji wa mitihani ili wanafunzi wafanye kwa utulivu.

“Tunawaasa walimu, wamiliki wa shule, wasimamizi na jamii kwa ujumla kutojihusisha na udanganyifu wa aina yoyote. Wataokiuka haya hatutasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Msonde.

Awali alieleza kuwa wanafunzi hao watafanya masomo matano ambayo ni: Kiswahili, Hisabati, Maarifa ya Jamii, Sayansi na English ambapo mitihani hiyo imeshasafirishwa kupelekwa vituoni.

Wanafunzi 917,072 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kesho na keshokutwa (Septemba 6 na 7).
Kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 432,744 sawa na asilimia 47.19, wakati wasichana ni 484,328 sawa na asilimia 52.81.
Watahiniwa 882,249 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na 34,823 watatumia lugha ya Kiingereza.
Jumla ya watahiniwa 94 wasioona wamesajiliwa  kufanya mtihani huo, wakiwemo wavulana 58 na wasichana 36.

Mwandishi: Edwin Lindege

TAZAMA VIDEO MSONDE AKIFUNGUKA

Leave A Reply