The House of Favourite Newspapers

NECTA Yafanya Mabadiliko Maswali ya Mtihani wa Darasa la Saba

 

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limesema litafanya mabadiliko ya mfumo wa utungaji wa mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka huu kwa wanafunzi wa darasa la saba nchini.

 

Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi amesema mabadiliko hayo aliyatangaza katibu Mkuu wa baraza hilo, Dkt. Charles Msonde katika mkutano mkuu wa tano wa maofisa elimu mkoa na wilaya unaofanyika mjini Dodoma ambapo kila somo litakuwa na maswali 45, kati ya hayo, maswali 40 yatakuwa ya kuchagua jibu sahihi na matano yatakuwa ya kujieleza/kuonyesha njia na jibu ili kupima uelewa wa wanafunzi hao.

 

Kwa maswali 40, kila moja litakuwa na alama 1 na maswali matano kila moja litakuwa na alama 2 huku majibu ya maswali 40 yatajibiwa kwenye fomu za OMR na maswali matano yatajibiwa kwenye karatasi maalum itakayoandaliwa.

 

Necta imetoa wito kwa walimu wakuu kuanza kuwapima wanafunzi kwa kutumia mabadiliko hayo ili kuwajengea uzoefu wasipate shida wakati wa mtihani huo wa Taifa.

Comments are closed.