The House of Favourite Newspapers

NECTA Yafunga Vituo Viwili Vya Kufanyia Mitihani, Waliodanganya Mitihani Kidato Cha Nne Kurudia – Video

0

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limevifungia vituo viwili vya mitihani ambavyo ni Shule Sekondari Thaqaaf iliyoko Mwanza na Twibhoki iliyoko Mara baada ya kubaini ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uendeshaji mitihani ya CSEE mwaka 2022.

Aidha baraza hilo limesema wanafunzi 337 waliofutiwa mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE)  mwaka 2022, watafanya mitihani hiyo pamoja na wanafunzi wa kidato cha sita kuanzia Mei 2 hadi 15, mwaka huu na kwamba maandalizi ya mitihani hiyo ya marudio imekamilika na itaanza Mei 2 hadi Mei 15.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 30, 2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Said Ally Mohamed amesema pamoja na kufungia vituo hivyo, baraza lilijiridhisha Shule za Sekondari Thaqaaf na Twibhoki zilifanya ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa mitihani.

“Baraza limefungia vituo hivi kwa mujibu wa kifungu cha 4(8) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 hadi tutakapojiridhisha kuwa ni vituo salama kuendesha mtihani wa kitaifa,” alifafanua.

Vituo vilivyobainika awali kuhusika katika udanganyifu huo na kutangazwa kufungiwa kuwa vituo vya mitihani ni Shule za Sekondari Cornelius na Andrew Faza Memorial zilizopo Dar es Salaam na Shule ya Sekondari Mnemonic Academy iliyopo Zanzibar,” alisema Dk.Mohamed.

amoja na kufungia vituo hivyo, amesema baraza hilo litaendelea kuthamini mchango wa uwekezaji wa wadau mbalimbali katika sekta ya elimu nchini na kwamba haitakuwa dhamira au sifa yao ya kufungia shule nyingi kuwa vituo vya mitihani.

Amesisitiza pale itakapobainika pasi na shaka kuwa shule inaacha kutekeleza majukumu yake ya msingi kutoka kituo cha kutoa elimu na kufundisha maadili mema na  kugeuka kuwa kituo cha kufundisha udanganyifu kwa watoto na kufanya vitendo vya hujuma, watachukua hatua kali za kijinai na kinidhamu ikiwemo kufungia shule.

Akizungumza kuhusu kurudiwa kwa mitihani ya kidato cha nne, Dkt. Mohamed amesema,  uamuzi wa watahiniwa kurudia mitihani umezingatia kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa waliofanya udanganyifu, chanzo chake kilitokana na mipango iliyoratibiwa na vituo husika kwa kushirikisha wamiliki wa shule, wakuu wa shule na wasimamizi wa mitihani.

Dk. Mohamed amesema baraza limekwisha wasilisha taarifa ya wale waliohusika kufanikisha udanganyifu huo kwa mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kuongoza baraza limesimama imara kutekeleza sheria, kanuni, miongozo na taratibu za uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kama zilivyo.

“Panapotokea udanganyifu waathirika wakubwa ni watahiniwa wenyewe hivyo nawaomba watahiniwa wote nchi nzima wasidanganyike wala kujaribu kufanya udanganyifu katika mitihani iwe kwa ridhaa yao binafsi au kwa kuwezeshwa na shule zao, tutachukua hatua stahiki ikiwemo kufuta mtihani na kufungia shule iliyoratibu uhalifu huo kiwa kituo cha mtihani,”  amesema Dkt.Mohamed.

BARAZA LA MITIHANI LATANGAZA TAREHE ya MITIHANI YA KIDATO CHA SITA, LAFUNGIA SHULE KADHAA…

Leave A Reply