Nelly Muosha Magari wa Posta-11
Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Nelly alipomnong’oneza fundi Yassin ahamie siti ya dirishani, alifanya hivyo kwani alijua nini shalobaro huyo alikuwa anataka kukifanya….Je, kiliendelea nini? Songa mbele na kitu hiki kitamu….
Fundi Yassin alitoa kauli hiyo kuwazuga abiria wengine wasiushitukie mpango wake na Nelly, kisha alimnong’oneza Nelly kwamba kama kweli alitaka teni ya fasta kazi ilibakia kwake.
“Kabla ya kufika Mwenge ndiyo utabaini mimi ni Nelson Nzamba a.k.a Nelly,” Nelly alimwambia fundi Yassin kwa sauti ya kunong’ona.
Basi likiwa limefika Tangi Bovu, Nelly alimgusa yule mrembo mgongoni ambaye wakati huo alikuwa kasimama pembeni yake na kumwambia aketi, kwa kuelewa Nelly alitaka kushukia kituo cha Bondeni yule mrembo aliketi na Nelly akasimama.
“Asante kaka yangu!” mrembo alimwambia Nelly.
“Usijali, ingawa bado sijafika mwisho wa safari nimeona nawe ukae japo kidogo,” Nelly alimwambia yule msichana.“Asante sana kaka kwa kunijali,” yule mrembo alimwambia Nelly bila kujua lengo la kijana huyo.
Wakati Nelly akizungumza na mrembo huyo, fundi Yassin alikuwa kishamvulia kofia na kujisemea moyoni:
“Kweli huyo dogo ni balaa hadi kufika Mwenge atakuwa kamuweka sawa huyu kiumbe,” fundi Yassin alijisemea moyoni.Gari lilipofika Makongo, Nelly alimtania yule dada kwamba jioni ile alikuwa akielekea wapi, mrembo akamwambia Keko.
“Keko ndiyo unakoishi au unakwenda kazini?” Nelly akamwuliza.
“Nyumbani!” mrembo akamjibu.Baada ya mrembo huyo kumfahamisha hivyo, Nelly alimwuliza alikuwa akiishi Keko ipi maana kuna Magurumbasi, Keko Mwanga, Keko Machungwa, Keko Madawa au Keko Akida?
Kufuatia Nelly kumtajia mrembo huyo vitongoji vya Keko akajikuta akicheka na kumwuliza kama kote huko alikuwa akikufahamu, Nelly akasema ndiyo maana kamtajia.
Wakati maongezi yakiwa yamepamba moto, walishtukia gari limefika Mwenge ambapo wote walishuka na kwenda kupanda basi la Tandika ambalo lilikuwa likijaza abiria.
Kwa kuwa basi hilo lilikuwa na viti vilivyokuwa wazi, Nelly alimpa ishala fundi Yassin akae siti iliyofuata ambapo yeye na yule mrembo wakaketi siti ya watu wawili.
“Daa, leo imekuwa bahati tumepata usafiri kirahisi namna hii?” Yule msichana alimwambia Nelly.
“Yaani huwezi kuamini kwa jinsi usafiri wa hapa unavyosumbua, mfano jana ilikuwa kasheshe tupu!” Nelly alimdanganya yule mrembo jambo lililomfanya fundi Yassin kutabasamu.
“Kweli huyu dogo ni balaa, kisha mpiga changa la macho dada wa watu, kweli ukitaka kumpata mrembo yeyote lazima uongo utumike,” fundi Yassin aliwaza.
Hawakukaa muda mrefu basi lilianza kuondoka, Nelly alifurahi sana kwani alijua mpaka kufika Keko atakuwa tayari kishamuweka sawa yule mrembo.Wakiwa wanaendelea na safari Nelly alimwuliza tena yule mrembo alikuwa akiishi Keko ipi kati ya alizomtajia, mrembo alitabasamu na kumwuliza mbona alihitaji sana kujua alikokuwa akiishi.
“Jamani kwani kuna ubaya gani ukinifahamisha, halafu unaweza kushangaa kukuta wewe ni ndugu yangu au unaishi jirani na ndugu zangu,” Nelly alimwambia yule mrembo aliyeishia kucheka.
“Haya bwana, mimi naishi Keko Juu ambayo hukuitaja,” yule mrembo alimwambia Nelly aliyeishia kucheka.
“Keko Juu karibu na Twiga Hoteli au Shule ya Msingi Mgulani?” Nelly alimwuliza.
“Du! Wewe kaka kweli unalifahamu hili jiji, mpaka Keko Juu unapafahamu?” yule mrembo alimwuliza.
Nelly alimfahamisha kote huko anakufahamu ndipo yule mrembo akamwambia alikuwa akiishi karibu na Twiga Hoteli.
Nelly alifurahi sana na kumwambia alikuwa akifika mara kwa mara katika uwanja wa mpira uliokuwa eneo lile kucheza mpira, Wawili hao waliendelea na maongezi ambapo Nelly alimwomba yule dada kama hatajali ampatie namba yake ili siku atakayorudi hewani wawasiliane.
“Kwani hauna simu?” yule mrembo alimwuliza.
Kufuatia Nelly kupenda kujipaisha, alimwambia alikuwa na simu yake ya kisasa ‘smartphone’ ambayo aliibiwa na dogo mmoja aliyeingia chumbani kwake akiwa anaoga.
Yule mrembo bila kujua akadanganywa, alimpa pole kisha alimwambia hata akimpa namba yake isingesaidia kitu kwa kuwa hakuwa na simu, Nelly akamwambia pale alikuwa na fedha za kununua simu na siku ilifuata angekuwa hewani.
Kitendo cha mrembo kuambiwa na Nelly kwamba alikuwa na fedha za kununua simu nyingine akajua kumbe alikuwa mambo safi na kwamba ikiwa alihitaji kununua simu ya kisasa hakukosa laki mbili au zaidi.
“Kama ana laki mbili yupo vizuri ngoja nimpe namba yangu najua tukizoeana nitakuwa nampiga mizinga mpaka akome,” yule msichana akawaza.