The House of Favourite Newspapers

Nelly Muosha Magari wa Posta-27

0

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Doreen aliyekuwa kapagawishwa vya kutosha na Nelly kupitia kwenye simu na kujikuta akifikia kilele cha Mlima Kilimanjaro na kupitwa usingizi, aliposhtuka alfajiri na kukumbuka kilichojiri akaishia kutabasamu. Je, kilifuatia nini? Songa mbele…

Doreen alipoachia tabasamu, akajikuta akijisemea moyoni:
“Mh! Huyu Nelly ni balaa, tukikutana laivu ni moto na kwenye simu pia ni moto zaidi!” Doreen aliwaza.

Msichana huyo aliyekuwa amekolezwa na penzi tamu la sharobaro Nelly aliendelea kumfikiria kijana huyo hadi alipopitiwa tena na usingizi.

Kulipokucha alimsikia Anne akiwa bize na kufanya usafi, akajiuliza amwambie kuhusu uhusiano wake na Nelly au ampotezee kuhofia huenda naye angelitamani penzi la kijana huyo kutoka Tandika.

“Haina haja, kama atahisi halafu akiniuliza nitamwambia lakini nitampiga mkwara asimzoee na kumtishia siku nikimbamba anajicheketua kwa Nelly ndiyo utakuwa mwisho wa kufanya kazi,” Doreen aliwaza.

Anne alipomaliza kufanya usafi alijiandaa akanywa chai kisha alimuaga Doreen aliyekwishaamka akaelekea chuo, huku nyuma Doreen akawasha runinga na kwenda kukaa sebuleni.

Binti huyo wa kishua alichukua simu yake na kumpigia Nelly kwa lengo la kumjulia hali na kujua muda ule walikuwa wako wapi, cha kusikitisha hakupatikana hewani.
“Huyu atakuwa hajawasha simu yake, ngoja nimsubiri,” Doreen alijisemea moyoni.

Akiwa katika hali hiyo ya kusubiri, akasikia kengele ya getini ikilia akaachia tabasamu, akiwa kavaa pensi iliyoishia juu ya mapaja yake iliyombana na kuzifanya hipsi zake zionekane vyema na singlendi iliyozionesha vyema chuchu zake akatoka kwenda kufungua.

Alipofungua akamuona Zakayo, almanusura asonye lakini akapotezea na kumsalimia kisha msaidizi huyo wa fundi akaingia ndani, Doreen akafunga geti na kurudi sebuleni bila kuzungumza zaidi na Zakayo.

“Huyu mtoto jamani kaumbika, sema tu ni haya mambo ya kazi, maana ukijifanya kidume halafu baba yake agundue hakika utalambwa shaba na maiti yako isionekane milele,” Zakayo alijisemea moyoni.

Kule ndani, Doreen alizidi kumuwaza Nelly kwani alitamani sana kumuona ndipo akasikia tena kengele ya getini ikilia, akatoka mbio kwenda kufungua akiwa na imani alikuwa fundi Yassin na Nelly kwani walikuwa na kawaida ya kufika pamoja.

Alipofungua akakutana na Haruni, kama ilivyokuwa awali alitamani kutoa msonyo akajizuia, Doreen akamsalimia ndipo kijana huyo licha ya kumtamani Doreen kwa jinsi alivyokuwa kanona, hakuthubutu kumwangalia mara mbili wala kusema chochote zaidi ya kuelekea eneo la kazi.

Kitendo cha fundi Yassin na Nelly kutowasili, kilimkosesha raha binti huyo wa kishua, hata hivyo hakukata tama kwa kuhisi huenda foleni ilichangia kuchelewa.
Doreen alikwenda mezani akamimina maziwa ya moto kwenye kikombe akachukua na soseji mbili na kurejea sebuleni kusubiri kusikia kengele ya getini ikilia.

Alipokunywa mafunda mawili na nusu soseji, akasikia kengele, aliachia tabasamu pana kwani alikuwa akijua sasa Nelly wake kawasili, akatoka na kwenda kufungua geti, badala ya kumuona Nelly akamuona fundi Yassin.

“Shikamoo fundi!” alimsabahi.
“Marahaba,hujambo Doreen?” fundi Yassin alimsalimia.
“Sijambo!” msichana huyo alijibu.

Fundi akiwa ameingia ndani, Doreen alimwuliza Nelly alikuwa wapi akamwambia siku ile asingefika, jibu la fundi lilimnyong’onyesha binti huyo wa kishua aliyemuuliza alikuwa na tatizo gani.

Fundi Yassin hakutaka kumwambia ukweli, akamdanganya kwamba alimweleza hakujisikia vizuri nahisi kutokana na uchovu wa kazi, kauli hiyo ilimfanya Doreen kumuonea huruma mpenzi wake.

“Jamani pole yake,” msichana huyo alimwambia fundi Yassin kisha akafunga geti na kuelekea ndani kwao akiwa hana raha.

Akiwa ameketi kwenye sofa alijaribu kumpigia simu Nelly lakini hakupatikana ndipo kwa hasira akaenda chumbani kwake na kujitupa kitandani na kuendelea kumuwaza Nelly.

Wakati Doreen akiwa katika hali hiyo, asubuhi Nelly alikwenda nyumbani kwa rafiki yake Ipyana aliyemkuta akimsubiri na baada ya salamu walikwenda kituoni walikopanda daladala ya Posta.

Kama ilivyokuwa kawaida ya sharobaro Nelly kupenda mademu, alikuwa akimtazama kwa matamanio sistaduu mmoja aliyekuwa amesimama naye karibu kwa sababu wote walikosa siti.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia wiki ijayo.

Leave A Reply