Nenga: Mimi na Nandy Mguu kwa Mguu Hadi Peponi!

WILLIAM Lyimo almaarufu kama Billnass, Bilinenga au Nenga, ni bonge moja la rapa hapa Bongo. Billnass amesikika kwenye ngoma kibwena zilizokamata vilivyo kama Chafu Pozi, Ligi Ndogo, Acha Nizikwe, Tagi Ubavu, Sina Jambo, Mazoea, Raha, Mafioso, Bugana, Kiboko Yao na nyinginezo.

Billnass ambaye alianzia kuimba kwenye kwaya miaka kadhaa iliyopita kabla ya kutumbukia kwenye Hip Hop, amekuwa akitrendi kinoma baada ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Queen wa Bongo Fleva, Faustina Charles ‘Nandy’.

Uhusiano wa wawili hawa ulianza kuwa wa moto kipindi kile ilipovuja video yao ya faragha wakifanya yao chumbani.

Kuna kipindi waliachana kabla ya baadaye kurudiana ambapo mwaka huu, Nenga amemvisha Nandy pete ya uchumba ambao umekuwa ukipigwa mawe na wengi wakisema hawatafika mbali.

Mara nyingi kumekuwa na uhusiano wa kimapenzi wa kulegalega kati ya staa na staa mwenzake na inakuwa ngumu sana kwa wote wawili kudumu kwenye mapenzi muda mrefu kwa sababu kila mmoja anakuwa anajua nyendo za mwenzake kama staa.

Lakini leo tunaona utofauti mkubwa kutoka kwa Nenga ambaye ameweka wazi kabisa uhusiano wake na Nandy na kusema yeye na mwanadada huyo watakuwa pamoja na watakwenda mguu kwa mguu hadi peponi.

Nenga amefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na IJUMAA SHOWBIZ na kufunguka mengi juu ya uhusiano wake na Nandy;

IJUMAA SHOWBIZ: Mambo vipi Bilinenga, michongo inaendaje?

BILLNASS: Salama tu, nashukuru Mungu mambo yanakwenda.

IJUMAA SHOWBIZ: Hongereni sana kwa kuzindua NB (Nandy Bridal), naona hadi bibie Nandy amekusifia ulikuwa ukimsukuma… hii imekaaje?

BILLNASS: Asante sana. Unajua kwenye maisha lazima msukumane na kukumbushana ili vitu viende sawa.

IJUMAA SHOWBIZ: Hivi kwako wewe Nandy ana utofauti gani na wanawake wengine wengi uliowahi kuwa na uhusiano nao?

BILLNASS: Sitaki kumaanisha kuwa niwaponde wanawake niliowahi kuwa nao, lakini kwa kweli Nandy amekuwa ni mwanamke wa kipekee sana kwangu?

IJUMAA SHOWBIZ: Unaweza kuuelezea utofauti wake?

BILLNASS: Nandy amekuwa ni mtu ambaye anajituma sana. Robo tatu ya maisha yake ni mwanamke anayefanya kazi sana. Muda mwingi sana anafikiria maisha na ni mwanamke muelewa sana.

IJUMAA SHOWBIZ: Mbona kuna baadhi ya watu wanasema Nandy ni mkorofi, je, umewezaje kukaa naye?

BILLNASS: Ni lazima au ni rahisi mtu kusema hivyo kwa sababu hakai naye hata kidogo na wengine hawamjui kabisa, lakini ukweli ni kwamba, ni mwanamke ambaye hapendi hata kidogo mambo ya ugomvi kabisa.

IJUMAA SHOWBIZ: Inadaiwa kuwa na wewe ni kama Uchebe (mpigaji wa mwanamke), yaani ngumi mtu, unazungumziaje hilo?

BILLNASS: Siwezi kumpiga hata siku moja na sina mkono huo wa kupiga na hata ningekuwa napenda kupiga wanawake, yeye (Nandy) nisingempiga kwa sababu ni mwanamke ambaye huwezi kuona kosa lake kirahisi.

IJUMAA SHOWBIZ: Mara nyingine tunaona uhusiano wa kimapenzi kati ya watu wanaofanya kazi ya aina moja ni ngumu hasa kwa upande wenu mnaofanya muziki ni ngumu kudumu kwenye uhusiano, unazungumziaje hilo?

BILLNASS: Kwa upande wangu au wetu ni ngumu hilo kutokea, kwani tuna misingi mikubwa sana tumejiwekea sisi wawili, hivyo ni ngumu. Kingine Nandy ni kama rafiki yangu, hivyo tunajuana na tunaweza kufanya mambo mengi.

IJUMAA SHOWBIZ: Ungependa kuzaa watoto wangapi na Nandy?

BILLNASS: Mimi napenda sana watoto na yeye anajua hilo, tumekubaliana watoto nane halafu ndiyo atapumzika.

IJUMAA SHOWBIZ: Inavyoonekana kama wazazi wa Nandy bado hawajakukubali vizuri, maana hawafunguki wazi kama wewe ni mkwe wao, hili limekaaje?

BILLNASS: Ni haki yao kwa sababu siyo kila kitu wakiweke wazi kwenye mitandao ya kijamii, maana wale ni watu wazima na wana uelewa mkubwa, siku yenyewe ikifika wataweka wazi kila kitu.

IJUMAA SHOWBIZ: Nandy amekuwa anaandamwa sana na Gigy Money kwenye mitandao ya kijamii, wewe kama mchumba wa Nandy unamuambiaje au kumshauri nini?

BILLNASS: Kila siku namwambia huwezi kuwa na jina kubwa ushindwe kupitia mambo kama hayo, hivyo nampa moyo tu aendelee kupiga kazi.

IJUMAA SHOWBIZ: Ugomvi mwingi wa wapenzi unatokana na simu, kwa upande wako simu haijawahi kuleta shida kwenye uhusiano wenu?

BILLNASS: Hakuna kabisa na sisi kila mmoja anashika simu ya mwenzake muda wowote anaotaka, anajua namba yangu ya siri na mimi ninajua yake, ndiyo maisha yetu.

IJUMAA SHOWBIZ: Unamwambia neno gani zuri Nandy kutoka kwako?

BILLNASS: Nataka kumwambia nampenda sana na nitaendelea kumpenda hadi siku ninapelekwa kaburini.

IJUMAA SHOWBIZ: Asante Nenga, nashukuru kwa ushirikiano wako.

BILLNASS: Asante sana karibu tena.

MAKALA: IMELDA MTEMA

Toa comment