Netanyahu Kukukutana na Trump White House Kuwajadili Hamas
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anatarajiwa kukutana na Rais wa Marekani, Donald Trump katika Ikulu ya White House, Jumanne ya Februari 4, 2025.
Katika taarifa aliyoitoa Netanyahu leo Jumapili, miongoni mwa mambo muhimu anayoenda kujadiliana na Trump ni kuhusu wapiganaji wa Kipalestina, Hamas ambao siku chache zilizopita, walikubaliana kusitisha kwa muda mapigano baina ya pande hizo mbili.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa anaamini Israel imewashinda Hamas lakini anataka kuumaliza kabisa mtandao wao pamoja na wanaowaunga mkono.
Masuala mengine watakaojadiliana, yanatajwa kuwa ni uhusiano wa Israel na Iran ambao upo kwenye mashaka makubwa ya kuibuka kwa machafuko baina ya pande hizo mbili pamoja na kujadiliana namna ya Israel kuboresha uhusiano wake na nchi za Kiarabu.
Mkutano huo utakuwa ni wa kwanza kwa Trump kukutana na viongozi wa mataifa ya kigeni tangu alipoapishwa ambapo unakuja wakati wasuluhishi wa mgogoro wa Israel na Hamas wakiwa kwenye jitihada za kuingia kwenye hatua ya pili ya upatanishi, itakayomaliza mapigano katika Ukanda wa Gaza.