New Zealand Kuharamisha Silaha Zinazofanana na za Jeshi

 

NEW ZEALAND itapiga marufuku silaha za aina yoyote zenye muundo wa kijeshi zilizotumika katika shambulio la mji wa Christchurch, Waziri Mkuu, Jacinda Ardern, amesema.

 

Sheria za matumizi ya bunduki nchini humo zimemulikwa tangu mshambuliaji mwenye itikadi kali za ubaguzi wa rangi alipowaua watu 50 katika misikiti miwili Ijumaa iliyopita.

 

Bi Ardern amesema anatarajia sheria hiyo mpya kuidhinishwa ifikapo Aprili 11. Amesema watu wanaomiliki silaha hizo watasamehewa watakapozisalimisha na pia kutaidhinishwa mpango wa kuzinunua kutoka kwa wamiliki hao.

 

Ameongeza kwambaserikali inakadiria kwamba gharama ya kuzinunua upya silaha hizo kutoka kwa wamiliki huenda ikawa ni “kati ya Dola mil. 100 na 200. Lakini hiyo ndiyo gharama ambayo ni lazima tuilipe kuhakikisha usalama wa jamii yetu”.

 

Mwanamme huyo aliyekuwa  na bunduki za rashasha ikiwemo ya AR-15, aliwaua waumini waliokuwa katika sala ya Ijumaa.   Inaaminika kwamba aliikarabati silaha yake ili iweze kutumia risasi za kiwango cha juu.

 

Brenton Tarrant, raia wa Australia anayeshtakiwa kwa mauaji hayo, alipata leseni ya kumiliki silaha nchini New Zealand mnamo 2017.

 

Akigusia athari kwa wamiliki wa bunduki, waziri mkuu huyo amesema anafahamu “wengi wenu mnawajibika kwa sheria”.

 

Aliongeza: “Wakati Australia ilipoidhinisha mageuzi kama haya, mtazamo wao ulikuwa ni kuruhusu wakulima kumiliki silaha hizo watapowasilisha ombi, ikiwemo idara ya udhibiti wa wadudu na wanyama. Tumechukua hatua kama hiyo kuzitambua silaha zinazohitajika kisheria katika maeneo hayo.

 

“Naamini  kwamba wamiliki halali wa silaha hizi nchini New Zealand wataelewa kwamba hatua hizi ni kwa maslahi ya taifa na watayakubali na kuyapokea mageuzi haya,” amesema Bi Arden.

 

Amesema mambo yote yatachambuliwa kuzuia watu kukimbilia kuzinunua silaha kabla ya sheria kuidhinishwa. Waziri wa Polisi  nchini humo, Stuart Nash, amesema: “Nataka nikumbushie kwamba ni fursa na si haki kumiliki silaha nchini New Zealand.”


Loading...

Toa comment