Ngassa, Yondani Wagoma Kuagwa

WACHEZAJI wa zamani waliocheza kwa mafanikio ndani ya Yanga, Mrisho Ngassa na Kelvin Yondani wamefunguka kuwa wao kwa sasa hawana mpango wa kuagwa na klabu yao hiyo kwa kuwa bado wanaendelea kucheza soka.

 

Ngassa na Yondani wametoa kauli hiyo baada ya wadau mbalimbali kuzua mjadala wa kwa nini Yanga hawajafanya sherehe za kuwaaga wachezaji hao ambao wamecheza kwa muda mrefu zaidi ndani ya kikosi hicho kuliko Niyonzima ambaye aliagwa juma lililopita.

 

Meneja wa Ngassa ambaye yupo karibu na Yondani, Godlisten Anderson (Chicharito), aliliambia Championi Jumatatu kuwa wachezaji hao wamekataa kuagwa na Yanga kwa sasa kwa sababu bado wanaendelea kucheza soka na wanaamini mchezaji anayeagwa ni yule ambaye anastaafu.

 

“Kiukweli mimi binafsi nimewashauri Ngassa na Yondani wakubali kuagwa na Yanga kama mwenzao Haruna kama viongozi wakitaka kufanya hivyo lakini wote wamekataa kabisa ishu hiyo kwa sasa.

 

“Hoja yao wanasema kuwa bado wapo kwenye gemu sana na wachezaji wanaoagwa ni wale ambao wanaachana na masuala ya soka. Hivyo wao wanaona hadi siku wakistaafu ndipo wafanyiwe sherehe ya kuagwa,” alisema Chicharito.

 

Ngassa anamalizia maisha mafupi ya mkataba wake ndani ya Gwambina ambao unafikia ukomo baada ya ligi kumalizika, wakati Yondani yeye anatumika ndani ya kikosi cha Polisi Tanzania.

 

JOEL THOMAS, Dar es Salaam


Toa comment