The House of Favourite Newspapers

Ngoma Hizi Zimebeba Maisha Halisi ya Harmonize au Konde Boy Mjeshi

0
Harmonize au Konde Boy Mjeshi.

 

RAJAB Abdul Kahali almaarufu Harmonize au Konde Boy Mjeshi; ni msani wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania ambaye ni miongoni mwa wasanii waliofanikiwa pakubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

 

Wimbo wake wa Never Give Up au usikate tamaa unaelezea safari ya mafanikio yake kwa undani zaidi.

Kabla ya kuwa msanii maarufu nchini Tanzania, Harmonize alionekana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha kuonesha vipaji cha Bongo Stars Search na aliambiwa na majaji hajui kuimba.

 

Hata hivyo, kwa bahati nzuri alipuua mbali ushauri wa majaji hao wa muziki na kuendelea na kile alichoona ni kipaji.


Hatimaye kujiamini kwake kulizaa matunda na leo hii anajivunia mamilioni ya wapenzi wa muziki wake katika Mtandao wa YouTube.

 

Tangu aanze muziki kwenye Lebo ya WCB mwaka 2015, Harmonize amekuwa ni moja ya wasanii bora sana kuwahi kutokea kwenye historia ya Bongo Fleva.

 

Moja ya silaha ambayo imeweza kumfikisha hapo ni pamoja na uandishi bora wa nyimbo zake. Harmonize au Teacher Konde ni mmoja ya wasanii wachache duniani ambao wanaweza kuelezea mambo yao binafsi ya kimaisha kwenye nyimbo zao.

 

Mara zote Harmonize huwa hafanyi ajizi kuzungumzia mahusiano yake ya kimapenzi, washindani wake wa kimuziki, bifu na hata kutaja majina ya baadhi ya watu wake wa karibu kwenye nyimbo zake; zote hizi zikiwa ni harakati za kuwajulisha mashabiki

 

wake nini hasa kinaendelea kwenye maisha yake ya kila siku.

Zifuatazo ni ngoma tano kutoka kwa Harmonize ambazo zimebeba maisha halisi ya mwamba huyo;

 

NEVER GIVE UP

Hii ni ngoma ambayo Harmonize ameweza kuhadithia historia yake ya kimaisha tangu alipotoka huko Mtwara, kukutana na Diamond Platnumz mpaka kuanzisha kiwanda chake cha kuchakata vipaji vipya cha Konde Music Worldwide.

Harmonize anawaaminisha Watanzania kwenye ngoma hiyo kuwa yeye ni maana halisi ya kutokukata tamaa.

Anasema; “Najua maisha safari na bado sijafika I got long way to go ila naona afadhali kulala uhakika na kula so ka before…”

 

VIBAYA

Hii ni ngoma ambayo Harmonize aliiachia mahususi kwa ajili ya mpenzi wake za zamani, Kajala Masanja au Mama Pau ambaye kwa sasa anamkosesha amani akimhitaji amrudie.

 

Hii ni ngoma ambayo iliashiria kuwa mahusiano yake na Kajala Masanja yamefikia mwisho kwani kupitia mistari ya ngoma hiyo, Harmonize anamkumbusha Kajala viapo vya kimapenzi ambavyo waliwekeana na kumuomba wasichukiane na kusemana vibaya hata wakiachana.

 

Kwenye vesi ya kwanza ya ngoma hiyo, Harmonize anasema; “Sitaki kuamini kwamba lile kapu la mabaya yangu halina hata machache mema. Nitakuwa mshamba nikiyasema yote mabaya ya mwenzangu ili nionekane mwema. Japo mapenzi yanaumiza I wish tusisemane vibaya…”

 

JESHI

Jeshi ni ngoma ambayo ilimtambulisha rasmi Harmonize nje ya lebo yake ya zamani ya WCB.

Hii ni ngoma ambao Harmonize anajipongeza kwa mafanikio aliyoyapata na ukubwa alionao na ndiyo maana anastahili kuitwa Jeshi.

 

Anasema; “Kamwe siwezi kujibizana ila mwenzenu nimeumbwa na subra, cheki madili yanavyogongana coz nyota yangu ni Libra.”

Kwenye ngoma hiyo, Harmonize anatoa shukrani za dhati kwa mashabiki wake wote hasa jamii ya mitandaoni kuanzia Twitter na Instagram kwa kumshika mkono huku akipeleka shukrani za dhati kwa Master Jay na Madam Rita kwa kumpa moyo wa kupambana kwenye muziki.

 

TEACHER

Teacher ni ngoma ya Amapiano ambayo ndani yake Harmonize ameonesha ukubwa wake, namna ambavyo ameibadilisha tasnia ya muziki nchini Tanzania na jinsi gani wasanii wengine wakubwa wanafuata nyendo zake ikiwemo kuiga aina yake ya muziki. Anasema; “Wakati wanahanya kugombea kiti, mie jicho liko nyanya nishakula kijiti na magoma yakipigwa huko club mtiti…”

 

MTAJE

Kama ambavyo Diamond Platnumz alimsifia Wema Sepetu kwenye Ngoma ya Moyo Wangu au Rayvanny alivyofanya kwenye Valentine maalum kwa ajili ya mpenzi wake, Paula Kajala, basi Harmonize alifuata kwa kuachia ngoma ya Mtaje kwa ajili ya aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja. Mtaje ni ngoma ambayo Harmonize amejimaliza kwa Kajala kwa kumpa sifa kedekede mpenzi wake huyo bila kumtaja jina na mwishoni kabisa mwa ngoma hiyo Harmonize anawapa home work mashabiki wake kuwa wawaulize watu wake wake wa karibu kama Jose Wa Mipango, Alice Kella na Uncle Duke maana wanajua ni nani hasa ameimbiwa wimbo huo.

Anasema; “Ana kasura kaupole miaka nenda rudi hazeeki tena ni mtu wa gym gym, shepu ndo linanipa wazim wazim na tattoo nimchore ila ndo hivyo tena hapendeki ama kweli mapenzi hayana mwalimu, wengine hata kuniona ni adimu…

Leave A Reply