The House of Favourite Newspapers

NGOMA, YANGA WAFANYA KIKAO KIZITO

UONGOZI wa Klabu ya Yanga, jana Alhamisi ulitarajiwa kukutana na kufanya kikao na mshambuliaji wa timu hiyo, Donald Ngoma kwa ajili ya kujadiliana juu ya hatma ya mshambuliaji huyo ambaye hajacheza kwa muda mrefu kutokana na kuwa na majeraha ya kujirudiarudia ya nyonga.

 

Yanga wamefikia hatua hiyo ya kukutana na Ngoma baada ya mchezaji huyo kushindwa kuitumikia timu hiyo ndani ya miezi sita mfululizo, ambapo viongozi wa timu hiyo waliomba ripoti ya daktari kwa ajili ya kuangalia taarifa zake.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika ameliambia Championi Ijumaa, kwamba walikutana na mchezaji huyo kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo, lakini kila kitu watakiweka bayana mara baada ya kufikia maafikiano baina ya pande hizo mbili.

 

“Kama tulivyosema siku chache zilizopita kwamba tungekuwa na kikao cha uongozi na mshambuliaji wetu, Donald Ngoma, ambaye kwa muda mrefu hajatumika kwenye timu kwa sababu yuko nje kutokana na kuuguza majeraha.

 

“Tutakutana naye leo (jana) Alhamisi kwa ajili ya kujadiliana naye, hadi sasa kila kitu kimeamuliwa sawa katika vikao vyetu vya mwanzo, hivyo kujua zaidi nini kati yetu tumeridhiana, subirini tutakiweka wazi baada ya kufikia makubaliano halisi ila kwa sasa elewa kwamba tumefanya naye kikao cha kwanza tu,” alisema Nyika ambaye pia ni mwenyekiti wa usajili wa timu hiyo.

 

Yanga walimsajili Ngoma misimu mitatu nyuma akitokea FC Platinum ya kwao Zimbabwe ambapo misimu miwili iliyopita alichangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kufanya vizuri kwenye ligi kabla ya msimu huu kupata majeraha na kuwa nje.

Na Musa Mateja na Said Ally | Championi

Comments are closed.