NGOMA ZILIZOFUNGA 2018 NA KUFUNGUA 2019

NOVEMBA 23, 2016 Ngoma ya Muziki ya Darassa akiwa amemshirikisha Ben Pol iliachiwa rasmi na baada ya hapo ilibaki kuwa historia kwani ilifanikiwa kupendwa na mashabiki wengi na kutoboa hadi 2017 ambapo hadi leo hii imetazamwa na mashabiki zaidi ya milioni 13 katika Mtandao wa Youtube.  

 

Lakini pia 2017 mwishoni mkali mwingine katika Bongo Fleva, Alikiba aliachia Ngoma ya Seduce Me ambayo nayo iliwateka mashabiki wengi na kutoboa hadi 2018 ambapo napo leo hii imetazamwa na mashabiki zaidi ya milioni 10. Imekuwa jambo la kawaida kwa wakali wengi kwenye muziki kuachia ngoma za kufungia mwaka na zikabamba kinomanoma.

 

Nchini Nigeria kumekuwa na ushindani wa kufunga mwaka na kutoboa mwaka kwa ngoma kali, Davido amefunga mwaka jana na Ngoma ya Wonder Woman wakati Tekno aliyekuwa amepotea kwa muda mrefu akifunga kwa Ngoma ya On You huku Patoranking akifunga na Everyday, Tiwa Savage akiachia One.  Kibongobongo wapo wakali wengine ambao walifunga mwaka 2018 kwa kuachia ngoma kali zilizotoboa hadi mwaka huu na Risasi Vibes linakuanikia listi ya baadhi ya wakali hao na ngoma zao.

 

SHETTA

Miaka miwili iliyopita mara baada ya kufanya poa na Ngoma ya Shikorobo, Kerewa na Wale Wale, Shetta alikaa kimya kwa muda bila kuachia ngoma yoyote. Mwishoni mwa mwaka jana ameonesha kuwa kipaji chake bado kipo juu baada ya kuachia Ngoma ya Hatufanani akiwa amemshirikisha Mr Blue huku kwenye kiitikio akikamatia Jux. Ngoma hiyo imetokea kubamba na kutoboa mwaka huu ambapo kwenye Mtandao wa Youtube hadi sasa imeshatazamwa na mashabiki zaidi ya milioni 1.5.

DARASSA CMG

Mara baada ya kutikisa na Muziki aliachia Ngoma ya Hasara Roho mwanzoni mwa 2017 ambayo haikubamba kivile na kumfanya kukaa kimya kwa muda mrefu huku akizua maswali mengi kwa mashabiki na wengine kudai ‘amezama’ kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

 

Mwishoni mwa mwaka jana aliwatuliza mashabiki wake kwa kuachia ngoma mbili kwa mpigo, Tofauti ikiwa ni ya mapenzi pamoja na Achia Njia.  Hata hivyo, Achia Njia ambayo kideo chake kimepikwa nchini Afrika Kusini chini ya Dairekta Justin Campos imetokea kupokelewa vizuri na kufungua mwaka poa, imeshatazamwa na mashabiki zaidi ya laki tisa.

HARMONIZE

Huwezi kumuacha katika listi hii kutokana na kutengeneza ngoma zilizofunga mwaka vizuri. Ngoma ya Paranawe akiwa ameshirikiana na Rayvanny kutoka katika lebo yao ya Wasafi Classic Baby (WCB) ndiyo iliyofunga mwaka vizuri kwa upande wake.

Ngoma hiyo aliyoachia Desemba 10, mwaka jana hadi sasa imetoboa mwaka huu ikiwa imetazamwa na mashabiki zaidi ya milioni 2.

ALIKIBA

Baada ya kuachia Seduce Me na kufunga mwaka vizuri, Kiba aliachia tena Mvumo wa Radi ambayo haikubamba kivile na kuamua kuendelea na harakati zake nyingine zikiwemo kujiingiza katika mpira na kusimamia lebo yake ya Kings Music.

 

Desemba 14, mwaka jana alifunga mwaka kwa kuachia Ngoma ya Kadogo ambayo imefungua mwaka ikiwa imetazamwa na mashabiki zaidi ya milioni 2.

KINGS MUSIC

Ukiambiwa utaje listi ya lebo zilizofunga mwaka jana kwa ngoma kali huwezi kuacha kuitaja Kings Music iliyoanzishwa mwaka jana chini ya Alikiba ikiwa na vichwa kama vile Abdu Kiba, Cheed, Killy na K 2ga.

 

Ngoma yao ya Toto walioachia Novemba mwaka jana ndiyo iliyowatambulisha rasmi kwenye muziki na kufungua mwaka ikiwa imetazamwa zaidi ya mashabiki milioni moja huku ngoma yao nyingine ya Masozy aliyoimba Cheed akishirikiana na K 2ga ikiwa imetazamwa na watu zaidi ya laki nane.

Loading...

Toa comment