The House of Favourite Newspapers

Ridhiwani Aitaka NHC Kuwa na Mipango Ya Muda Mrefu

0
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt. Maulidi Banyani (Aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete katika kikao chake cha Bodi pamoja na Menejimenti ya NHC tarehe 24 Januari 2022.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuwa na mipango ya muda mrefu ya miradi ya ujenzi wa nyumba zake kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kukidhi mahitaji yanayoendana na ukuaji wa miji.

Ridhiwani ametoa kauli hiyo tarehe 24 Januari 2022 jijini Dar es Salaam alipokutana na Bodi pamoja na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa kwa lengo la kupata uelewa jinsi shirika linavyofanya kazi na kupata taarifa ya miradi ya shirika.

‘’Hapa la msingi ni kuwa na plan za mbele, lazima tuzungumzie Shirika la Nyumba la Taifa ndani ya miaka 100 ijayo’’ alisema Ridhiwani.

 

Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) alipokutana nao Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam kupata uelewa wa majukumu na miradi ya shirika .

 

Akitolea mfano wa mkoa wa Morogoro, Naibu Waziri Ridhiwani alisema, Shirika la NHC lazima lifikirie mipango yake kwenye mkoa huo hasa ikizingatiwa mkoa huo ni kiunganishi cha mkoa wa Dar es Salaama na Makao Makuu ya nchi Dodoma.

 

‘’Sisi tunaiangaliaje Morogoro? plan lazima zije maana nikitaka kupunguza safari ya kwenda Dodoma ni mkoa wa Morogoro hivyo NHC tunaingaliaje Morogoro, hata kama hatuna mpango wa leo tuangalie kesho ‘’ alisema Ridhiwani.

Ridhiwani Kikwete akiangalia sehemu ya bwawa la kuogelea kwenye mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa wa Morocco Square jijini Dar es Salaam alipokwenda kukagua mradi huo

 

‘’Suala hilo ni sanjari na maeneo mengine, nimeangalia Morogoro kama eneo linalokuwa na jambo hili ni muhimu, tuangalie ‘future’ inakuaje na tunaendaje? Alisema Naibu Waziri wa Ardhi.

 

Aidha, alilitaka Shirika la Nyumba la Taifa kuangalia uwekezaji kwenye miradi ya nyumba za bei nafuu sambamba na miradi ya ujenzi wa nyumba inayofanyika kuzingatia mahitaji ya kila eneo kwa lengo la kupata wateja.

 

Hata hivyo, Ridhiwani aliipongeza NHC kwa hatua yake ya kuanza kuzifanyia ukarabati nyumba zake zilizochakaa na kusema kwamba, hatua hiyo itazifanya nyumba za shirika sasa kuwa na taswira nzuri.

...Ridhiwani Kikwete akiangalia mandhari ya jiji la Dar es Salaam akiwa kwenye moja ya jengo la miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa ya Morocco Square

 

Shirika la Nyumba la Taifa lina nyumba 17,115 za kupangisha katika maeneo mbalimbali nchini. ‘’Pale mtaa wa Uhuru kuna jengo limetoa na kivuli jengo ni imara lakini mazingira yake na nawashauri wakati wa kufanya ukarabati wa nyumba zenu basi mfikirie namna wapangaji waliopo mtawapeleka wapi wakati wa ukarabati’’. Aliuliza Ridhiwani.

 

Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa Dkt Maulidi Banyani alimueleza Naibu Waziri kuwa, Shirika lake limejiwekea mpango wa miaka mitano wa kufanya ukarabati wa nyumba zake zilizochakaa na kubainisha kuwa, katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 shirika hilo limetenga takriban shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ukarabaiti wa nyumba hizo.

 

‘’Mhe Naibu Waziri Nyumba baadhi ya nyumba za shirika zimechakaa na nyingi ni zile zilizotwaliwa miaka ya 1971 na plan ya matengenezo ni ya miaka mitano na kwa mwaka huu wa fedha tumetenga takriban bilioni 8. Jumla ya bilioni 52 zitatumuka kutekeleza mpango huo.

 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Ridhiwani Kikwete alitembelea mradi wa shirika la Nyumba la Taifa wa Morocco Square unaohusisha viwanja vilivyopo barabara ya Mwai Kibaki na mtaa wa Ursino, Dar es Salaam.

 

Ridhiwani ameridhidhwa na maendeleo ya mradi huo alioueleza kuwa, una sifa nyingi sambamba na sura ya kipekee kwa sababu una ‘junction’ kubwa kwenye makutano. Alisisitiza kuwa, ameridhika na mazingira aliyoyakuta kwenye mradi huo wa Morocco Square na kuahidi kumpa ushirikiano Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt Maulid Banyani.

 

Kwa mujibu wa Dkt Banyani mradi huo wa Morocco Square unaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 137.5 umefikia asilimia 90 na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.

Leave A Reply