The House of Favourite Newspapers

Ni Ajabu! Miaka 20 Bado Bongo Muvi Inatambaa

0
Muigizaji wa Bongo Muvi, JB

DUNIANI kuna maajabu mengi, kuna vitu vinavyofanywa au vilifanywa ambavyo vinashangaza mno. Mfalme Nebukadneza wa Babylon (Iraq) alimjengea bustani malkia wa Sheba bustani inayoelea angani. Ukiachana na hayo, Wamisri walijenga mapiramidi miaka mingi nyuma, mapiramidi yaliyokuwa na mawe makubwa, mpaka leo wanasayansi wanashangaa, yale mawe makubwa yaliyojenga yalipelekwaje juu na wakati hawakuwa na vifaa? Mbaya zaidi, eneo yalipokuwa mapiramidi yale (Giza) hakuna hata mawe pembeni.

Muigizaji wa Bongo Muvi, Gabo

Ukiwa unashangaa kwenye mambo yanayoendelea, hebu pia utatakiwa kuishangaa tasnia ya filamu ya Bongo Muvi. Ninachokumbuka ni kwamba tasnia hii ilianza miaka ya 2000 wakati filamu kama Girlfriend na nyinginezo zilitoka. Ni miaka mingi, ni miaka ambayo mtoto aliyezaliwa enzi hizo sasa hivi yupo kidato cha sita.
Ni ajabu, inashangaza. Kinachouma zaidi ni kuona wale Wahindi wanapiga hatua sana, wanatuacha kwa kasi kubwa. Walipokuwa wameanza, tuliona, enzi hizo kama ni filamu za mapigano, unaona kabisa ngumi inapita hewani, kama ni risasi, unasikia kabisa kwamba mlio uliotoka si wa risasi bali kitu kingine kabisa.

Muigizaji wa India, shahrukh khan

Hawa Wahindi ambao tuliwaona wapo nyuma, wazugaji kama tulivyokuwa, leo hii wanakimbizana na Hollywood. Unaweza kuamini? Wahindi wapo siriazi na filamu zao. Walijua kwamba wapo nyuma lakini wakataka kupambana, wakapambana, wakapewa sapoti na mwisho wa siku kufika walipo sasa hivi.

UDHAIFU WAO, WALIUFANYIA KAZI
Wao ni kama sisi. Kitambo walikuwa wakichukua filamu za Hollywood na kuziigiza wao. Kama unakumbuka, walikwishawahi kuchukua filamu ya The Godfather ya mwaka 1972 wakaiigiza kwa kuipa jina la Sarkar, kuna filamu ya Yuvvraaj (2008) iliyochukuliwa kutoka katika filamu ya The Rain Man (2008), kuna Zinda (2006) iliyochukuliwa kutoka Oldboy (2003), Dhoom (2003) kuoka kwenye filamu za The Fast And Furious (2001) na Ocean Eleven (2001).


Wahindi waliiba ideas za muvi za Hollywood zaidi ya mia moja. Walichokuwa wakifanya ni kukopi na kupesti, kilichokuwa kikibadilika ni mandhari na waigizaji tu. Watu waliwalalamikia kwa kile walichokuwa wakikifanya na mwisho wa siku wakaamua kuacha na kutengeneza muvi kwa ideas zao wenyewe.
Kwa kukudokeza ni kwamba mpaka sasa hivi filamu iliyoingiza pesa nyingi nchini India ni filamu ya Baahubali 2: The Conclusion ambayo imeingiza kiasi cha dola milioni 263 ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni 500 huku ikifuatiwa na Raees ya Shah Rukh Khan iliyoingiza kiasi cha dola milioni 45 ambazo ni zaidi ya bilioni 90.
Elimu ndogo inawaangusha Bongo Muvi

Muigizaji wa India, Priyanka Chopra

Huu ni ukweli usiopingika. Haijalishi ni kwa kiasi gani utakuwa na kipaji, pasipokuwa na elimu bado kipaji chako kitaonekana kuwa butu. Waigizaji wa Bongo Muvi hawana elimu, watu wengi wakishindwa maisha huingia kwenye tasnia hiyo ilimradi tu wapate pesa na kuchukua wanawake/wanaume kadiri wawezavyo.
Afrika tunaamini kwamba ili ujue Kiingereza ni lazima uwe umekwenda shule. Hilo ni tatizo kwetu, waigizaji wengi hawaifahamu lugha hiyo na ndiyo maana filamu zao zinaishia hapahapa Bongo.
Kanumba aliwapiga gepu kwa kuwa aliijua lugha, aliweza kuwasiliana na muigizaji wa Nigeria, Noah Ramsey na kuigiza filamu ya Devil Kingdom. Isingekuwa lugha, ninaamini Kanumba asingeweza kufanya hivyo.
Alipofariki tulisema kwamba fulani angechukua nafasi yake, yupo wapi? Mbona mpaka leo ni mwaka wa tano tangu Kanumba afariki lakini yupo hapohapo? Akaja mwingine, tukasema huyu ataweza, naye akashindwa. Tatizo kubwa ni lugha, hakuna mtu anayethubutu kwa kuwa tu lugha imekuwa tatizo kwa waigizaji wengi wa Bongo.

Muigizaji wa Bongo Muvi, Gallis

GALLIS AMEANZA! TUMUUNGE MKONO
Najua inauma lakini wakati mwingine jipoze tu. Galis alikuwa msanii mchanga aliyeamua kuthubutu kwa kufanya kazi kama alivyokuwa akifanya Kanumba. Ninapomwangalia, ameanza kupiga hatua, hakuonekana kuridhika, alijua kabisa kwamba ili ujulikane ni lazima ufanye kazi na waigizaji wa kimataifa. Huwezi kujulikana kimataifa huku ukifanya kazi nchini mwako tu.
Kijana Galis amejitahidi, ameigiza filamu na waigizaji wa Nigeria na Ghana katika filamu ya When Your Boyfriend is Unromantic. Humo, mwanzo mwisho kapiga Kiingereza na waigizaji hao, hii inaonyesha kwamba kama ukiijua lugha hiyo vizuri basi kwako kutusua halitakuwa tatizo, utatakiwa kuwa na subira tu.

Muigizaji wa Bongo Muvi, Wema Sepetu

HIVI WEMA YUPO KWELI?
Labda hajafahamu ni kitu gani anatakiwa kufanya! Labda anahisi yeye ni msichana hawezi kutoka. Labda hajiamini, au tuseme hajaamua kuthubutu tu. Ukweli ni kwamba anajirudisha nyuma.
Huyu ana mambo mengi yenye faida, anajulikana, ameonana na wasanii wakubwa akiwemo Noah Ramsey (Nigeria), Van Vicker (Ghana) na wengine wengi, anajua Lugha ya Kiingereza, ila kwa nini yupo hapo alipo? Hivi kweli uigizaji kwake haulipi ama? Hivi kuna watu wangapi wanatamani kuwa na nafasi kama aliyokuwa nayo? Tatizo kwake ni nini hasa? Au hawaoni wakina Emma Watson? Au hamuoni Lupita Nyong’o? Kipi kinamshinda?
Tatizo la waigizaj wengi wanaridhika na vitu vidogo. Mchukulie msanii kama Priyanka Chopra wa India. Alianza kuigiza nchini India, aliendelea na mwisho wa siku kuonekana Hollywood na kumchukua kisha kumuweka kwenye muvi zao kama Quantico, Baywatch na nyinginezo na kutengeneza pesa.


Hakuna mtu asiyependa kitu kizuri, kama Wema angejitangaza Afrika, kutokana na uzuri wake angeweza kupata nafasi, lakini tatizo linalokuja ni kwamba karidhika, si yeye tu bali hata waigizaji wengine wa kike wanajiona wamefika! Waende Hollywood kufanya nini bwana na wakati kama kuuza nyago Instagram inawapaisha?

HITIMISHO.
Bongo muvi inatambaa, haikui, kila siku ipo palepale. Wanayoifanya isikue ni waigizaji wenyewe. Wana filamu mbaya, makosa mengi, ideas zinafanana, hawaoni umuhimu wa kutengeneza filamu nzuri, hawataki kutumia pesa nyingi kutengeneza filamu zao.
Dunia imebadilika. Kwa sasa Hollywood wanazunguka duniani kutafuta waigizaji wazuri. Unapokuwa mzuri, umejitangaza na uwezo kuonekana, kwa nini wasikuchukue? Wasanii wa Bongo Muvi ni nafasi yao kuchagua, kusuka au kunyoa? Kama wataishia kutambaa tu, kuna siku magoti yatachoka na kuamua kukaa kabisa, na huo ndiyo utakuwa mwisho wao.

Imeandikwa na Nyemo Chilongani, GPL

Leave A Reply