The House of Favourite Newspapers

NI KOSA KUMPA MCHUMBA HUDUMA ZA MKE AU MUME !

 NIANZE kwa kumshukuru muumba wa mbingu na nchi, kwa rehema na fadhila anazonifanyia katika maisha yangu ya kila siku, ama kwa hakika ni Mungu mwenye upendo. Ahsante baba. Natumaini hujambo na kama unasumbuliwa na jambo lolote, iwe kiafya au kiuchumi, naomba usikate tamaa kwani matatizo ni sehemu ya maisha, jambo la muhimu ni kumuomba Mungu na kujaribu kutafuta suluhu ya tatizo hilo.

Kama mada inavyojieleza hapo juu, kwa kawaida ukiwa ni mwanamke huwezi kumpa kila mwanaume huduma za mume wakati bado ni mchumba tu. Vijana wa siku hizi wanapochumbiana au kutafuta urafiki wa kawaida kati ya kaka na dada (dating), wengi hawajajua kwamba hiyo ni hatua ya mwanzo kabisa na ni kama usaili tu wa kumpata mtu wa kuoana na kujenga naye maisha.

Ndoa na uchumba (girlfriend au boyfriend) ni vitu viwili tofauti kabisa. Uchumba huhusisha kumfahamu mwenzako kama anafaa kuwa mke au mume na ndoa ni agano na kumkubali mtu kuishi naye hadi kifo kiwatenganishe. Hata siku moja, asikudanganye mtu, uchumba si ndoa na ndoa si uchumba. Kila kimoja kina mipaka yake.

Ukimpa mchumba haki za mume au mke, siku mkiachana na huo uchumba (kitu ambacho ni kawaida kama ukiona uliyenaye katika uchumba hawezi kuwa bora kwenye ndoa) utaumizwa zaidi hasa mwanamke kwani mwanaume anaweza kumpata binti mwingine jioni yake au usiku huohuo na akaendelea na maisha bila kokoro.

Kinachoshangaza pia ni kwamba hata uhusiano unapovunjika mara nyingi mwanaume huumia kidogo kwa kuwa mwanaume siku zote anapoingia kwenye mapenzi huingia kwa tahadhari, wakati mwanamke akimpata mwanaume (mchumba) anajiona amepata kitu cha pekee.

Utasikia akina dada wengi wanasema ‘mimi nipo kwenye uhusiano kamili’ wakati ndiyo kwanza wapo kwenye urafiki wa kimapenzi ambao waweze kuyeyuka muda wowote. Ni kweli wanaweza kuwa sahihi, lakini wanatakiwa kuacha nafasi kwa ajili ya kuchunguza na si kumfanya huyo mwanaume ni mume na kumpa haki au huduma zote kiasi kwamba uhusiano ukivunjika unaanza kulia na kusaga meno.

Si busara kumpa mwanaume kila kitu katika uhusiano wa uchumba wakati hujaoana naye. Unamfulia nguo, unalala kwake na unampikia chakula wakati yeye ni rafiki wa kiume tu? Umeliwa! Swali ambalo mwanaume anajiuliza ni kwa nini aingie gharama za kukuoa kama umeshakuwa mke hata bila kuvalishwa pete kwenye kidole?

Kwa nini akuoe wakati tayari ameshajua kila kitu kuhusu wewe ikiwemo kukutumia atakavyo? Kwa nini anunue ng’ombe kama maziwa na nyama vyote anapata? Kumbuka wazazi wetu walikuwa makini sana na hayo mambo na mwanamke yeyote hakujifanya mke wakati ni mchumba tu. Uchumba ni daraja tu la kupita kufikia ndoa. Huwezi kugawa zawadi zote ambazo zipo kwenye begi kabla ya kufika kwa mwenyeji wako katika safari ya kuelekea kwenye ndoa. Wanaume ni binadamu, si Mungu na kila binadamu ana sifa ya kugeuka nyuma pale anapoona njia anayoenda si yenyewe.

Uwe na lengo la kuhakikisha unaweza kuweka mipaka na usimfanye huyo mwanaume ndiyo awe kila kitu hapa duniani kwani kuna siku anaweza kubadili uamuzi ndipo utakapojuta. Ni busara kwa wewe mwanamke hata kama una mchumba uendelee kujihusisha na kazi na taaluma yako kiasi kwamba hata ikitokea amekuacha, huwezi kuchanganyikiwa.

Kama umewekeza kwa mchumba upendo na mapenzi ya asilimia mia moja. Je, baada ya kuoana utawekeza kiasi gani? Jiulize na ujitafakari kisha uchukue hatua! Kwa maoni, nicheki kwenye namba hiyo hapo juu. Pia usikose kutembelea ukurasa wetu wa Gazeti la Ijumaa Wikienda kwenye Facebook.

Comments are closed.