Ni Kweli Bifu la Diamond na Harmonize ni Mchongo?

PAMOJA na kwamba mwaka 2021 umepinduka na sasa ni mwaka 2022, lakini bado dunia ya burudani Bongo imebaki kwenye mjadala uleule wa bifu la wasanii wakubwa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na Harmonize au Konde Boy Mjeshi.

 

Stori za vijiweni zinadai kwamba, eti ishu ya Harmonize kujiengua kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) ya Diamond na kwenda kuanzisha lebo yake ya Konde Gang Music ulikuwa ni mchongo wa wawili hao kwa lengo la kumpoteza King Kiba ambaye ndiyo kwanza bifu lake na Diamond lilikuwa limeshika kasi.

 

Hija zao zinaegemea kwenye wakati ule tetesi zinasambaa kuwa Harmonize anaondoka WCB aliskika mlevi mmoja akidai Harmonize ili atoke WCB anatakiwa kulipa shilingi milioni 500 na haikujulikana ilikuwaje au alililipa na ghafla tu ikasikika kwamba ashalipa, lakini kabla ya hapo Harmonize mwenyewe alikuwa amesema pesa hizo hana.

 

Cha ajabu ni pale alipokuwa akihojiwa Clouds FM akasema ameshalipa baada ya kuuza nyumba zake tatu jijini Dar!

Mara tu baada ya kulipa pesa hizo, eti hapohapo akapata tena pesa nyingine akanunua vifaa vya studio, akaweka maneneja na madairekta, mabodigadi, akapanga mijengo ya kifahari kwa ajili ya ofisi na makazi kisha akawa na mandinga makali ikiwemo Toyota Land Cruiser V8 na mengine akawagawia wasanii wake.

 

Stori za maskani zinaendelea kudai kwamba, eti Diamond na Harmonize walikaa meza moja, wakajadili jambo baada ya Harmonize kutaka kukaa nje ya WCB.

 

Harmonize alipoeleza nia yake hiyo, Diamond alimkubalia fasta kama alivyofanya kwa Rayvanny ambaye ameanzisha lebo yake ya Next Level Music na wakatengeneza kwanza kiki, lengo zima likiwa ni kupoteza maboya ili ionekane kweli wana bifu, lakini ukweli ni kwamba ilikuwa ni namna ya kuzima ushindani mkali wa King Kiba.

 

Wawili hao; Diamond na Harmonize waliamini hata kama watu watawaona maadui, lakini ukweli utabaki kuwa Harmonize ni zao la Diamond.

Stori za kitaa zinakwenda mbali zaidi na kudai kwamba, ukifuatilia kwa ukaribu, hakuna Team Kiba anayemshabikia Harmonize isipokuwa kuna Team Konde Gang ambayo wanamshabikia King Kiba.

 

Wanadai ni katika mazingira hayohayo ambapo Harmonize anadaiwa kuwashawishi Cheed na Killy kuondoka Kings Music ya King Kiba na kuhamia Konde Gang; jambo ambalo lilipangwa na upande wa pili lengo likiwa ni kuzidi kupunguza nguvu ya King Kiba.

 

Swali wanalojiuliza ni kwamba, kwa nini hakuwashawishi Lava Lava au msanii mwingine kutoka WCB?

Makala hii imejaribu kuwasilisha maoni ya wana wa kitaani na kile wanachokiamini na si hitimisho la kuendelea kujadili. Acha mjadala uendelee!

MAKALA; SIFAEL PAUL, BONGO


Toa comment