The House of Favourite Newspapers

Ni Kweli Kuna Dawa za Kutibu Nguvu za Kiume? -6

0

BAADA ya kuwasoma wataalamu mbalimbali wa afya, yaani madaktari na wale wa lishe na kuona namna walivyochambua mada hii ya ukosefu wa nguvu za kiume, leo tuhitimishe kwa kuangalia kama kweli kuna dawa au la. Kwa kifupi ni kwamba upungufu wa nguvu za kiume ni kile kitendo cha mwanamume kutokuwa na uwezo wa kusimamisha nyeti yake na kutoa mbegu bora zisizo na uwezo wa kutungisha mimba.

 

Tatizo hili limeongeza sana nchini na sababu kubwa ya ongezeko hili ni kwamba dawa nyingi zinazodaiwa kuponya, hazina viwango vya kuitwa dawa, bali ni vichocheo tu kwani kinachopigiwa chapuo huwa ni kumudu tendo kitandani na si nguvu asilia. Ukweli ni kwamba upungufu wa nguvu za kiume hauondolewi kwa dawa za kuchochea nguvu wakati wa tendo. Hizi dawa zina madhara makubwa na mara kadhaa husababisha vifo kwa wanaume kama madaktari walivyofafanua katika matoleo yaliyopita.

 

Matatizo ya nguvu za kiume huchangiwa na kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari, kula vyakula ambavyo si vya asili na mengineyo mengi. Pia dawa za kuua wadudu huleta tatizo hili kwani zina viambata sumu viitwavyo ‘estrogen’, matatizo ya kisaikolojia, kupiga punyeto kwa muda mrefu na kutumia vyakula vyenye kemikali zinazowekwa kwenye makopo. Wataalamu wanasema kuna uhusiano mkubwa sana kati ya upungufu wa nguvu za kiume na kuwa na sumu mwilini zinazotokana na vyakula vyenye kemikali tunazobugia kwa kupenda au kutokupenda ndiyo maana wapenzi wa vyakula hivyo wengi wakiwa vijana, wanapata tatizo hili.

 

Ni vizuri wenye matatizo kama hayo wakatumia vyakula vya protini hasa ya mimea kwani hurutubisha mbegu. Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Lishe, Abdallah Mandai, kuna aina ya vyakula ambavyo vimefanyiwa utafiti na kubaini kuwa ni moja ya vyakula vinavyosaidia kuongeza nguvu za kiume.

 

TANGAWIZI

Mandai anasema tangawizi ni moja ya chakula kinachoweza kurejesha nguvu za kiume, unaweza kuichemsha tangawizi na ukatumia kwa kuinywa kama chai asubuhi, mchana na jioni. Pia unaweza ukaitumia katika mchanganyiko wa kiasili kwa kutumia habat soda, asali na kitunguu saumu.

 

JINSI YA KUTUMIA

Chukua tangawizi na kitunguu saumu vitwange kisha vichanganye na asali pamoja na unga wa habat soda na uwe unakunywa mchanganyiko huu kwa kutumia kijiko cha chai kimoja kutwa mara tatu kwa muda wa wiki moja na utaona mabadiliko.

 

TIKITIMAJI

Chakula kingine kinachosaidia kuongeza nguvu za kiume ni tunda la tikitimaji. Mandai anasema unaweza ukachukua tikitimaji ukalikata na kutengeneza juisi yake kisha ukawa unakunywa, lakini hata lenyewe unaweza ukalila.
Jitahidi kutumia tunda hili hata ikiwezekana kila siku kwani linasaidia sana kwa wenye matatizo ya nguvu za kiume.

 

ZINGATIA MAMBO HAYA

Mtu mwenye tatizo hilo anatakiwa kufuata mambo yafuatayo; kufanya mazoezi, na kwa wenye kisukari, kutokula vyakula vyenye sukari kama vile soda, chokoleti, aisikrimu, pipi, juisi za kopo na kuacha kutumia sukari yenyewe kama kiungo kwenye kinywaji chochote.

 

VYAKULA

Vyakula anavyopaswa kuvitumia mwenye upungufu wa nguvu za kiume wakati wa kutibu tatizo hilo ni ugali wa dona, faida yake ni kuwa ataongeza uwezo wake wa nguvu za kiume na mbegu za kiume pia zitaimarika. Anashauriwa kula mbogamboga hasa za majani kwa wingi, zabibu mbivu, samaki aina zote, maziwa freshi, maharage, kunde, mihogo, viazi vitamu, mafuta ya alizeti, ufuta au mawese, achaache kutumia mafuta ya wanyama. Mwenye ttizo la nguvu za kiume atumie matunda kama vile parachichi, ndizi mbivu, machungwa, chenza, madalanzi, maboga, tikitimaji, papai, nanasi, tende, nyanya, pera, kitunguumaji, zabibu, karoti, madafu, bamia, bilinganya, mayai ya kienyeji n.k.

 

MAZOEZI

Ikiwa una tatizo hili unatakiwa kula karanga na kunywa maji mengi sana. Kama tulivyoona hapo juu, mazoezi ni muhimu, mwenye upungufu wa nguvu za kiume ahakikishe kila siku anafanya mazoezi kwa angalau nusu saa ama kwa kukimbia au kwa kuruka kamba akiwa nyumbani kwake. Mazoezi haya ndiyo yanayofanya mzunguko wa damu uwe mzuri na mgonjwa asimamishe uume vizuri. Hata hivyo, mazoezi yasiwe makali sana. Mwenye tatizo hili aache kula vyakula vya viwandani kwani vina kemikali nyingi, badala yake kama tulivyoshauri awali ale vyakula vya asili na aache kula nyama nyekundu.

 

HITIMISHO Makala haya yamedhihirisha kuwa zipo dawa za hospitali za kuongeza nguvu za kiume kama vile Viagra, Erecto, Cialis na Suagra lakini mnywaji lazima ashauriwe na daktari asijinywee tu kwani ni hatari. Pia dawa za mitishamba serikali imesema zipo lakini hazijathibitishwa na serikali na serikali ipo mbioni kufanya hivyo japokuwa vyakula vya asili ni salama na vinasaidia kuondoa tatizo hili.

MWISHO.

Makala: ELVAN STAMBULI

Leave A Reply