The House of Favourite Newspapers

NI SUMU? DAKTARI AMCHOMA MTOTO SINDANO, MKONO WAKAUKA!

TAHARUKI ya aina yake imezuka ndani ya hospitali moja kubwa mkoani hapa (jina linahifadhiwa kwa sababu maalum) baada ya madai kuzagaa wodini kuwa kuna mtoto ameongezewa damu mwilini yenye sumu. 

 

Vyanzo vya habari kutoka hospitalini hapo vililiambia Uwazi hivi karibuni kuwa mtoto anayedaiwa kuongezewa damu iliyozua utata ni lssaya Merikion mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Imedaiwa kuwa mtoto huyo akiwa na mama yake alifika katika hospitali hiyo na kulazwa wodi namba 6 akikabiliwa na tatizo la upungufu wa damu.

 

HALI ILIVYOTOKEA

Inaelezwa na mama mzazi wa mtoto huyo aitwaye Regina Hassan alipofanya mazungumzo na Uwazi kuwa: “Mimi naishi mzumbe wilaya ya Mvomero mwanangu alikuwa ana tatizo la upungufu wa damu mwilini. “Zahanati ya mzumbe walituambia kuwa tumlete kwenye hospitali kubwa hapa mjini ili apatiwe tiba zaidi.

 

“Tulipofika tulilazwa na kuandikiwa matibabu ikiwemo kuongezewa damu, sasa kuna muuguzi alikuja akatuambia kuwa anataka kumuwekea mtoto damu. “Tukamuadaa; akamchoma sindano, akamuwekea damu kisha akaondoka lakini baada ya muda nikaanza kuona hali ya mtoto inabadilika.

 

“Nilipomuangalia vizuri mkono ulikuwa mwekundu ni kama damu zilikuwa zimevilia, ikabidi nimshike ili niangalie vizuri. “Nikashangaa kuona mkono umekauka kama kuni ikabidi nichanganyikiwe, ndo nikamwita nesi ili aje amwangalie mwanangu aone kilichompata, “ alisema mama wa mtoto huyo.

 

YAHARUKI YA SUMU ILIVYOSAMBAA

Kufuatia mkono wa mtoto lssaya kukakamaa na kuwa kama kuni baadhi ya watu waliokuwa wakiuguza watoto wao waliingiwa na hofu huku wengine wakimtuhumu nesi aliyemhudumia mtoto huyo huwenda alichanganya na sumu kwenye damu ambayo imemdhuru mtoto huyo. “Watu wangapi wameongezewa damu hawajapata tatizo kama hili, hii itakuwa ni sumu,” mama mmoja alisema jambo lililomfanya mama wa mtoto kuangua kilio akiamini huwenda lisemwalo lipo.

 

MANESI WAHAHA KUZIMA SOO

Mara baada ya tuko hilo kutokea, baadhi ya waguzi na maesi katika hospitali hiyo walianza kuhaha kuiondoa skendo hiyo huku wakionesha matumaini kuwa mtoto huyo atapewa rufaa kwenda Muhimbili ambako atatibiwa na kupona.

“Hakuna sumu katika tiba, kilichotokea ni kitu cha kawaida, mtoto apewa rufaa, msiwe na wasiwasi, alisema nesi mmoja wakati akijaribu kutuza hali ya hewa kwa ndugu na jamaa wa mtoto huyo ambaye mpaka sasa mkono wake umekauka.

 

BABA WA MTOTO AIBUKA

Baba wa mtoto Issaya alipoona hali hiyo na kubaini kuwa taarifa za uwepo wa mtoto huyo zimeshafika kwenye vyombo vya habari aliomba habari isiandikwe akihofia kuwa huenda wauguzi wakamfanyia mwanaye kitu kibaya zaidi. “Mimi ni baba wa mtoto kweli lakini habari hii sitaki iandikwe, kuna baadhi ya madaktari nimeongea nao wamesema kuwa wanaweza kunisaidia kumtibu mtoto wangu, “ alisema baba huyo aliyejitambulisha kwa kina moja la Merikion.

 

KINACHOWASHANGAZA WENGI

Watu wengi waliofika kumjulia hali mtoto huyo wameshangazwa na hali ya mkono huo kukauka kama kuni ghafla huku mtoto akikosa hisia na maumivu ya aina yoyote kwenye mkono huo.

“Sasa sijui mkono umekuwaje, huku hata ukimfinya haumii, naogopa mwanangu asije kuwa amepata ulemavu wa kudumu,” alilia mama wa mtoto huyo huku akiomba serikali na hasa wizara ya afya iangalie namna ya kumsaidia mwanaye kupata tiba. Wakati taharuki hiyo ikiendelea baadhi ya watu wamekuwa wakimshawishi mama huyo kumfungulia mashtaka nesi aliyemsababishia Issaya tatizo hilo.

Image result for ummy mwalimu

DAKTARI AELEZEA TATIZO

Daktari maarufu mkoani Dar es Salaam ambaye amefanya kazi katika hospitali mbalimbali za mkoa huo maarufu kwa jina la Dokta Chale alipoulizwa juu ya tatizo hilo la mtoto kuwa limesababishwa na sumu au nini, haya ndiyo yalikuwa majibu yake:

 

UWAZI: Kuna mtoto amekauka mkono wakati akiwekewa damu, watu wengi wanahusisha tukio hilo na sumu.

CHALE: Hapana haiwezi kuwa sumu.

UWAZI: Ni kitu gani pengine kitabibu wewe unaweza kuwaeleza watu wakaelewa zaidi kuliko kuendelea kuwa na hofu kuwa mtoto awekewa sumu?

CHALE: Kama maelezo waliyotoa ni sahihi tatizo hilo kitaalam linaitwa DRY GANGRENE yaani kuzuiwa kwa damu yenye hewa ya Oksijeni kusafirishwa kwenye mishipa ya mkono.

 

UWAZI: Kuzuiwa huko kulitokana na nini, kwa mtazamo wako?

Kitabibu kuna mambo mengi, lakini kwa kuwa tatizo lilitokea wakati akiongezewa damu huenda mtu aliyefanya zoezi hilo alitoboa mishipa inayosafirisha damu nyepesi (artery) kutoka kwenye moyo kwenda mwilini na kuacha mishipa inayosafirisha damu nzito kuelekea kwenye moyo kisha kusambaa mwili mzima yaani veins.

 

UWAZI: Kama kosa hilo likifanyika, nini huwa kinatokea?

CHALE: Kinachoweza kutokea ndiyo kama hicho kilichompata huyo mtoto, ni kwamba ukilazimisha mishipa inayosafirisha damu inayotoka kwenye moyo isafirishe damu kwenda kwenye moyo hilo haliwezekani, ni sawa na kuingilia mlango wa kutokea.

 

UWAZI: Aisee!

CHALE: Ndiyo hivyo ukikosea utajikuta damu safi inazuiliwa kutoka kwenye moyo na hii inayoingizwa inabaki kuziba njia ya damu nyepesi isipite lakini hata yenyewe haiwezi kupitia njia ambayo siyo yake, matokeo yake mishipa inakosa damu, inakakamaa na kiungo kinakuwa kama kuni.

UWAZI: Nini tiba ya tatizo hili dokta?

CHALE: Mara nyingi hali hii ikitokea matibabu pekee yanayoweza kumsaidia mgonjwa ni kukata sehemu iliyokufa.

 

MGANGA MKUU ALIPOLAZWA ISSAYA AKOSEKANA

Uwazi lilipotafuta nafasi ya kumuona mganga mkuu wa hospitali hiyo anayetajwa kuwa na mamlaka ya kulizungumzia tatizo hilo hakuweza kupatikana, jambo ambalo Uwazi limeona kama sababu ya kutotajwa kwa hospitali hiyo kwa vile upande wa pili haukupatikana kuzungumza.

Hata hivyo, Uwazi linaendelea kumtafuta akipatikana huenda akaeleza kile kilichotokea mpaka mtoto Issaya kukauka mkono na kuwa kama kuni.

Daktari Amchoma Mtoto Sindano ya SUMU, Mkono Wakauka!

Comments are closed.