The House of Favourite Newspapers

Ni tatizo mume kuishi kwa kutegemea kipato cha mkewe?

0

vegeterians-couple-bed

Kazi imekuwa ni kigezo cha msingi sana ili ndoa ziweze kuwepo. Hata hivyo, wakati wengine wakijitahidi kutafuta wachumba wanaofanya kazi, wapo wanaume wasiopenda kuoa wanawake wanaofanya kazi huku wakitoa sababu ambazo kwa kiasi kikubwa hazina uzito bali ni dhana potofu tu.

Huko nyuma wanawake walikuwa wakichukuliwa kama mama wa nyumbani wasiostahili kufanya kazi nje ya nyumba. Wao walionekana ni viumbe wanaostahili kufanya kazi za nyumbani.

Dhana hiyo katika kipindi hicho iliwaathiri wanaume wengi na baadhi kujikuta wakikataa kuoa wanawake wanaofanya kazi. Hata ikitokea kumpenda mwanamke anayefanya kazi, atamshauri kuacha ili amuoe.
Mawazo hayo mpaka sasa yapo kwani wapo wanaume hawataki kabisa kuoa wanawake ambao wanafanya kazi huku kila mtu akitoa sababu zake.

Si hivyo tu, dhana hii pia imewaathiri wanawake walio wengi, baadhi ‘wamesusa’ kufanya kazi wakiamini lazima wataolewa na wanaume wanaofanya kazi.

Mimi siwezi kuyaingilia maamuzi ya mtu ila ni vizuri tukashauriana katika mambo ambayo ni yenye manufaa kwetu.
Ifahamike kwamba, wanawake pia wana haki ya kufanya kazi, hawakuumbwa kwa ajili ya kukaa nyumbani tu na kuwategemea waume zao kwa kila kitu.

Kwa hali ilivyo sasa, wanaume kwanza wamekuwa makini sana kiasi kwamba kabla hawajachukua uamuzi wa kuoa wanahakikisha wana kazi ambayo itawafanya waweze kuendesha maisha vizuri ndani ya familia.
Naamini kabisa hakuna mwanaume anayeweza kudiriki kuoa huku akiwa hana kazi na ikitokea hivyo basi mwanaume huyo atakuwa na matatizo.

Wapo wanaume ambao, licha ya kuwa na kazi lakini pia wanapooa mwanamke ambaye hana kazi hujitahidi kumtafutia kibarua angalau wasaidiane kuboresha maisha yao.  Sambamba na hilo, wanawake wengi sasa hawataki kuwa tegemezi kwa waume zao, wamekuwa wachakarikaji wasiopenda kugeuzwa ‘magoli kipa’.

Kuoana mkiwa wote mnafanya kazi kuna faida zake. Kwanza mnadhihirisha usawa uliopo baina ya mke na mume kwamba wote mnastahili kufanya kazi na kuchangia katika maendeleo ya familia na ya taifa kwa ujumla.

Zaidi ya yote, wanandoa wanaweza kusaidiana katika kuchangia matumizi ya ndani ya familia kutokana na kila mtu kuwa na kipato. Maisha ya sasa ni kusaidiana na si kutegemeana, labda ziwepo sababu za msingi za mume kutegemea kipato cha mke ama mke kutegemea kipato cha mume.

Cha msingi kwa wanandoa wote ni kufahamu kwamba ndoa ni heshima na ili heshima hiyo idumu milele, lazima kuwepo na ushirikiano, uaminifu, maelewano na majukumu kwa kila mtu.

Aidha, tumezoea kwamba katika familia mwanaume ndiye anayetegemewa kwa kiasi kikubwa na ndiyo maana inashauriwa kwamba bila yeye kuwa na kazi, si busara kuoa, labda kama itatokea kwamba anayetaka kumuoa anafanya kazi na amekubali kuwa na mume kula kulala.

Lakini cha kujiuliza katika hili ni kwamba, hivi ni sahihi mume kugeuka tegemezi kwa mkewe? Kwamba mume hana kazi na amekubaliana na hali hiyo lakini mke anafanya kazi tena ya kipato kikubwa na yuko tayari kumhudumia mumewe, inakuja kweli?

Mimi sikatai kwamba kila mtu ana mfumo wake wa maisha aliojipangia, sasa kama mwanaume umekamilika halafu unaona ni sawa kulishwa, kuvalishwa na kuhudumiwa kwa kila kitu na mkeo, ni wewe na ‘ubwenyenye’ wako.
Ndiyo, nasema ni ubwenyenye kwa sababu mume kuwa tegemezi ni jambo ambalo halijazoeleka. Labda mwanaume awe mgonjwa au mlemavu lakini kama ana nguvu zake, akili na maarifa, hawezi kukubali mkewe asubuhi anaamka kwenda kazini yeye kalala.

Niseme tu kwamba, mwanaume kugeuka tegemezi siyo jambo linaloleta picha nzuri mbele ya jamii. Ishi kwa kumtegemea mkeo kwa sababu za kueleweka lakini kinyume chake wewe utakuwa ni mume bwege ambaye huenda wala huyo mkeo hujamuoa ila kakuoa.

Leave A Reply