The House of Favourite Newspapers

NI UNYAMA! MAMA ASIMULIA MWANAYE ALIVYOBAKWA – VIDEO

Zalijah akisimulia.

 

INAUMA! Mama mmoja, Zalijah, mkazi wa Keko-Mwanga, Wilaya ya Temeke jijini Dar amesimulia jinsi mwanaye wa kike, (jina linahifadhiwa) alivyobakwa na jamaa aliyefahamika kwa jina moja la Nyaumiza.

Akizungumza kwa majonzi, Zalijah alisema kuwa, tukio hilo lilijiri Machi 2, mwaka huu wakati yeye alipokuwa ameenda kwenye mihangaiko ya kutafuta fedha.

 

“Ilikuwa majira ya jioni, kama ya saa kumi na moja nilikuwa nimetoka kwenye biashara zangu na kumkuta mwanangu akiwa mpole tofauti na siku zote. Nilimuuliza ana matatizo gani? Akaniambia kuwa hana tatizo, nikajaribu kumbana huenda amechokoza wenziye akawa hajanijibu, nikaondoka.

“Baada ya kurudi nikamkuta amelala kwenye kochi na dada yake alikuwa nje akichota maji, aliporudi akaniambia nimwangalie vizuri mwanangu kwani alipita baba Eva (Nyaumiza) na kumuita huku akiwa amelewa, ikabidi nimchukue mwanangu na kumuingiza chumbani kumhoji,” alisimulia Zalijah kwa uchungu.

 

Aliendelea kusimulia kuwa, alimbana zaidi mwanaye kuhusiana na Nyaumiza akafunguka kuwa aliitwa akiwa na mwenzake na kuulizwa kama wanataka hela, yeye akakataa ndipo mzee huyo akachomoa shilingi mia mbili na kumuambia mwanangu aongozane naye hadi kwake akamtume sehemu.

“Walipofika huko nyumbani kwa Nyaumiza, mwanangu aliambiwa alale kitandani, akakataa, akasukumizwa kitandani kisha akavuliwa nguo ya ndani na kufanyiwa mchezo mchafu. Nilishtuka sana, ikabidi nimshike mkono mwanangu hadi kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Keko Mwanga, Elizabeth Tosy.”

 

Akiendelea kusimulia, Zalijah anasema alipofika kwa mwenyekiti alimchukua mtoto na kumhoji, baada ya hapo aliwasiliana na sungusungu na kwenda kumkamata Nyaumiza nyumbani kwake na kumfanyia utaratibu wa kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Chang’ombe ambako alifunguliwa jalada lenye namba CHA/ RB/2769/2018 UBAKAJI.“Mwanangu alipelekwa katika Hospitali ya Temeke na kupatiwa matibabu,” alimaliza kusema mama huyo.

 

Risasi Jumamosi lilizungumza na baba wa mtoto huyo, Mwisindi ambaye alilaani kitendo kilichotokea kwa mwanaye na kuiomba serikali kuweka sheria kali dhidi ya watu wanaofanya vitendo hivyo.

“Si kitendo kizuri mtaani na kwenye jamii, si mwanaume wala mwanamke ni kitendo kibaya sana. Naomba serikali iweke sheria kali ikiwezekana hata wafungwe miaka 100,” alisema.

Akizungumza kwa jazba, mmoja wa jirani wa Zalijah, Said Ahmed alilaani tukio hilo na kusema kuwa ni la kidhalilishaji hivyo kuiomba serikali wakitokea watu kama hao wachukulie hatua kali ili iwe fundisho.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi

Inasikitisha! Mtoto wa Miaka 6 Abakwa, Aeleza Hali Halisi

Comments are closed.