‘Ni vizuri mwanaume, amfiche mkewe vipato vyake’

couple-counting-money-475Ukipata bahati ya kukaa kwenye vijiwe vingi vya wanaume, kauli za ‘mwanamke usimueleze kila kitu’ huwa zinatawala. Wanaambizana kwamba ili uhusiano udumu, usimueleze kila kitu mwanamke. Wanasema mfiche asijue kila kitu.

Taswira hiyo imeanza kama utani lakini pengine kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele, sasa inakuwa kama sheria. Wanaume wanasambaziana mbinu hiyo ili kukabiliana na wanawake zao. Wanaona ni bora kuwaficha baadhi mambo ili mambo yaende vizuri.

Mwanaume anaamini akimficha baadhi ya vitu mkewe, inasaidia kumfanya aishi kwa amani. Hataki kumueleza kila kitu kinachomhusu kwani anaamini uwezo wake wa kukabiliana na mambo hauwezi kuwa sawa na yeye hivyo bora amfiche.

Hali hiyo haikuja hivihivi, imetokana na visa mbalimbali wanavyokutana navyo katika uhusiano. Wanafikia hatua ya kuwafananisha wanawake na watoto. Kwamba hata kama mwanaume hana fedha, hapaswi kumueleza mwanamke kuwa hana fedha.

Kwamba mwanamke usimueleze vyanzo vyote vya mapato maana ukimueleza ni tatizo. Lazima ataleta usumbufu. Atakuwa wa kwanza kuhoji matumizi na kutaka kila kitu wapange wao.

Mwanaume asipokubaliana naye, anakuwa wa kwanza kuleta chokochoko ambazo mwisho wa siku zinasababisha mtafaruku ndani ya nyumba. Hapo ndipo wanaume wengi wanapopakwepa.

Wanakubali kuumia kimoyomoyo. Hamuelezi hata siku moja ukweli kuhusu mapato yake. Hata kama hana kitu, mkewe au mchumba wake akiomba fedha, anampa tu matumaini kwamba asiwe na wasiwasi atampatia siku fulani hata kama hana uhakika wa kuzipata.

Utasikia: “usijali baby nitakupa kuwa mvumilivu.”

Tafsiri ya wanaume hao ni kwamba, hata ukiwaeleza ukweli, wanawake wana kasumba ya kutoelewa. Wanaume wanaamini kwamba wanawake wengi wanapenda matokeo chanya ya mambo yao bila kujua ugumu au mazingira ambayo wanaume wanayapitia.

Hiyo ndiyo sababu ya wanaume wengi hulazimika kuwaficha mishahara wake zao wakiamini wakijua ni tatizo. Wanaamini kwamba watalazimisha matumizi hata yasiyo ya lazima kwa kuwa wanajua mishahara ya mabwana zao.

Wanashindwa kuwaeleza kwa sababu wanaamini wanawake hawana fikra ya kujua hatima ya kesho. Wanawazia matumizi ya leo tu. Kwa ujumla, wanaume huamua kuficha vyanzo vyao ili tu kuepusha ugomvi.

Wakati mwingine wanaamua kuficha baadhi ya vyanzo ili mwanamke ‘atakapong’ang’ania’ matumizi ya baadhi ya vyanzo anavyovijua, anajua vipo vya ziada ambavyo vitamfanya awe huru kutokana na kutohojiwa matumizi yake.

NINI CHA KUFANYA?

Kama nilivyofundisha wiki iliyopita, wawili ambao mna uhusiano ambao upo ‘serious’, hamna sababu ya kufichana. Hapa nawazungumzia wale ambao wanaelekea kwenye ndoa au tayari wapo kwenye ndoa. Nilisema wenye uhusiano wa aina hiyo, wanapaswa kuondoa u-mimi.

Mnapaswa kutumia u-sisi. Kwamba nyinyi sasa mnakuwa mwili mmoja hivyo hakuna sababu ya kufichana katika mambo yenu. Muelezane ukweli hata kama ni mgumu. Hamna sababu ya kufichana kwani nyinyi ni mwili mmoja.

Wanawake wanapaswa kukubaliana na mazingira ya wanaume. Mtengenezee mazingira ya kumuelewa mumeo au mchumba wako kwamba hata akikuambia hana kitu, hauwezi kuleta kelele. Utamtia moyo hivyo wakati utapita.

Uchunguzi unaonesha wanaume wengi hupenda kuwaficha wanawake wao kwa sababu tu, hawapendi malumbano. Wanaamini wakiwaeleza ukweli wake zao kitakachofuata ni malumbano hivyo ni bora kumficha baadhi ya mambo.

Japo inasaidia kudumisha lakini hakuna kitu kizuri kama kuambizana ukweli.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.


Loading...

Toa comment