Niffer Amshukuru Rais Samia Baada ya Kuachiwa Huru – Video

Mfanyabiashara Jennifer Bilikwija, maarufu kama Niffer, ameushukuru uongozi wa Serikali na vyombo vya sheria baada ya kuachiwa huru kufuatia uchunguzi ulioonesha kuwa hana hatia.
Akizungumza mara baada ya kutoka gerezani, Niffer alisema kuwa anashukuru Mungu, familia yake, na wote waliomsimamia wakati akiwa kizuizini.
“Nawashukuru sana familia yangu kwa kuwa upande wangu toka nikiwa gerezani mpaka sasa kuachiwa,” alisema Niffer.
Aidha, alitoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa msamaha uliomwezesha kurejea uraiani, pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa usimamizi na ufuatiliaji wa hatua za kisheria zilizofanikisha uamuzi huo.

Niffer pia aliwatahadharisha wananchi na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuzingatia amani nchini, akisisitiza kuwa machafuko yanaweza kuathiri shughuli nyingi, ikiwemo mwenendo wa kesi na uchumi wa wananchi. Alihimiza pia msaada kwa wafungwa magerezani, akibainisha kuwa mahitaji yao bado ni makubwa.
“Kwa sasa mimi binafsi nitakuwa balozi mzuri wa kuwaasa vijana kuachana na masuala yanayoweza kuvuruga amani,” alisema Niffer.
Kwa upande wake, mama mzazi wa Niffer, Mwanaisha Isack, alisema kuwa furaha yake ni kubwa kutokana na uamuzi wa Rais kumuachia mtoto wake huru. Alieleza kuwa kipindi alichokuwa mbali na mwanawe kilimletea maumivu na msongo wa mawazo.
“Leo narudi kwako kwa kukushukuru kwani nina furaha kuwa na mwanangu. Familia yangu yote imenituma kusema asante,” alisema mama huyo.
Mwanaisha pia aliwataka vijana kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani, ili kulinda utulivu wa nchi na mustakabali wa maisha yao.

