The House of Favourite Newspapers

Nikiiangalia Zanzibar; bado Watanzania tupo majaribuni

0

sheinsseifHAKIKA Mungu ni mwema na anastahili kuhimidiwa milele. Nasema hivyo kutokana na hali ya usalama na amani ambayo ipo nchini kwa sasa. Wengi kabla ya uchaguzi mkuu tulikuwa na wasiwasi na tulikuwa tukikesha tukiombea nchi amani, Mungu ametusikia.

Lakini jambo moja la wazi ni kwamba mgogoro wa Zanzibar unaumiza vichwa watu wote wanaoitakia mema nchi hii na tukiri kuwa tupo majaribuni.

Kwa usemi wa wahenga ni kwamba majaribu yasipokuua, yanakuimarisha zaidi, Tanzania kama taifa, limepita na kwa namna fulani bado lipo katika majaribu.

Nikikumbuka tangu tunaanza kampeni za uchaguzi mkuu, hadi tunapiga kura na kutangazwa matokeo, pamoja na kutarajia kuchagua viongozi watakaoongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Watanzania walikuwa na mtihani mwingine muhimu lakini haukuwa dhahiri sana.

Ushindani mkubwa miongoni mwa wagombea, hamasa na wakati mwingine jazba zilizotokana na maneno na kejeli za wakati wa kampeni za uchaguzi huo kwa baadhi ya wagombea au wapambe wao ziliwafanya baadhi ya watu ndani na nje ya nchi, kuanza kuamini kwamba huenda ile sifa ya Tanzania kuwa kisiwa cha amani inaweza kutoweka.

Jambo ambalo hawakulijua waliokuwa na hisia hizo ni kwamba hii ni Tanzania ya Watanzania. Pamoja na yote yaliyojitokeza, uchaguzi kuwa na ushindani mkubwa pengine kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi, Tanzania kwa kiasi kikubwa imeendeleza utamaduni wake wa amani na utulivu.

Watanzania kwa kutambua kwamba Utanzania wao hautokani na mipaka tu ya kijiografia iliyowekwa na wakoloni, bali uhusiano wa kindugu na upendo miongoni mwao uliojengwa juu ya misingi imara ya utu wa binadamu, walijitokeza kistaarabu na kwa utulivu mkubwa kwenda kupiga kura.

Wakakaa na kuwa wavumilivu wakati wa kusubiri matokeo rasmi yatangazwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) chini ya Mwenyekiti Jaji Damian Lubuva.

Hivyo, Watanzania wameendelea kuwaenzi waasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume ambao kwa namna ya pekee waliweza kujenga taifa lenye mshikamano na umoja miongoni mwa raia wenye imani, itikadi na kabila tofauti.

Lakini pia Watanzania kwa mshikamano wao wameidhihirishia dunia kwamba taifa hili linaweza kuhimili mikikimikiki ya uchaguzi kwa amani.

Jumuiya za kimataifa na vyombo vya habari vya nje vilikuja kufuatilia uchaguzi huu, ili kuona kama Watanzania wanaweza kuvuka salama katika mazingira ya ushindani kwa kiwango hiki lakini wameshuhudia kuwa tumeweza.

Nawapongeza Watanzania kwa kulinda heshima yao na heshima ya taifa lao, wameonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa ambao unastahili pongezi.

Jaribio lililopo mbele yetu linakuja ninapoangalia mgogoro wa kufutwa kwa matokeo ya kura au uchaguzi wa upande wa pili, yaani Zanzibar.

Naamini kuwa Wazanzibari wameonesha uungwana kipindi hiki cha uchaguzi na bila shaka wameendelea kuwa mfano kwa nchi nyingine katika kuendesha mchakato wa uchaguzi na kusubiri matokeo kwa njia ya utulivu.

Sasa ili kulinda heshima hiyo, uungwana unatakiwa utawale katika kushughulikia tatizo la uchaguzi wa Zanzibar ili liishe salama.

 Sina haja ya kusema kifanyike nini kumaliza mgogoro huo mzito lakini naamini viongozi wanajua nini cha kufanya ili nchi isiingie katika ghasia ndiyo maana nimesema Watanzania bado tupo majaribuni.

Leave A Reply