Nikki afichua siku atakayoachia kichupa cha Baba Swalehe
Mwana Hip Hop mahiri nchini, Nikki wa PiliNa Hans Mloli.
MWANA Hip Hop mahiri nchini, Nikki wa Pili ametangaza rasmi kuwa anatarajia kuachia ‘kichupa’ cha ngoma yake gumzo kwa sasa mitaani, Baba Swalehe mwishoni mwa mwezi Desemba, mwaka huu.
Nikki au Genius ameliambia Championi Jumatano kuhusiana na ishu hiyo katika mahojiano maalum ambapo alifunguka kuwa tayari ameshaanza maandalizi ya awali ya ‘ku-shoot’ video ya wimbo huo ingawa hajajua itafanyika nchi gani na atalifahamu hilo mapema baada ya kumaliza kupanga bajeti zake.
Aidha, aligusia pia kuhusiana na kushangazwa na kufurahia mapokeo ya wimbo huo ulivyovunja rekodi ya nyimbo zake zote za nyuma na kugeuka gumzo kila kona ya jiji.
“Nimepanga kuanza ku-shoot mwanzoni mwa Desemba na nitaichia mwishoni mwa mwezi huo, sijajua nitafanyia wapi, tukimaliza zoezi la kupanga bajeti nafikiri nitakuwa nishafahamu nitafanya kazi na kina nani na mahala gani maana kila director anajulikana bei zake na mazingira yake.
“Lakini aisee mapokezi ya huu wimbo yamekuwa makubwa kwa kipindi kifupi mno, tofauti na nyimbo zangu nyingine za nyuma maana ‘interview’ zimekuwa nyingi, maofisini, mitaani, kila kona mijadala ni Baba Swalehe,” alisema Nikki ambaye ni memba wa Kundi la Weusi.