The House of Favourite Newspapers

Niler Bernard Modo Mbongo Anayetusua Kimataifa

0
Modo wa Tanzania anayetusua Kimataifa, Petroniler Bernard.

WATU wengi wanafahamu kuhusu Wanamitindo Millen Magese na Flaviana Matata ambao baada ya kufanya vizuri katika sanaa ya urembo nchini, sasa ni mabalozi wazuri katika anga la kimataifa.

Kwa sasa, Flaviana Matata aliyewahi kuwa Miss Universe Tanzania 2007 ni mwanamitindo anayefanya kazi zake nchini Marekani wakati Millen, aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2001, anafanya vitu vyake Afrika Kusini.

Hata hivyo, nje ya mabinti hao wawili, yupo mdogo wao, ambaye ndani ya miaka minne tu, tayari ameshajitengenezea jina na sasa anawakimbiza mamodo wa kimataifa.

…Akiwa kwenye mapozi.

Jina lake ni Petroniler Bernard, akizaliwa Septemba 25, mwaka 1992 jijini Arusha. Baada ya kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Sinoni na baadaye Sekondari ya Lemara na Ndumma, mwaka 2010 alijiunga na Chuo cha Utumishi wa Umma Mtwara, akisomea Record Management Certificate kabla ya kuja kupata Diploma katika Chuo cha Utumishi, Dar es Salaam mwaka 2014.

Simulizi yake kuelekea umodo ni ya kufurahisha, kwani ilianza kama utani, miaka minne tu iliyopita, wakati mtoto wa mama yake mkubwa alipomfahamisha uwepo wa Zanzibar Fashion Week 2013 na kumtaka akajaribu bahati yake, kwani umbo na uelewa wake ungeweza kumsaidia.

Akiwa hajui lolote kuhusiana na masuala ya urembo na uanamitindo, Petroniler, ambaye kwa sasa anajitambulisha kama Niler Bernard, alikwenda katika mchujo uliofanyika Septemba jijini Dar mwaka huo na kukuta rundo la watu 150, wake kwa waume ambao walitakiwa kugombea nafasi 14 zilizotakiwa, saba kila jinsia.

“Huwezi kuamini, nilibahatika kuchaguliwa kati ya wasichana saba. Basi ndivyo ilivyokuwa, tukaenda kushiriki na kurudi, hamu ya kuijua zaidi sanaa ya urembo ndiyo ikanikamata. Mwaka huohuo nikashiriki tena shindano moja lililoitwa Tanzania Top Model, ambalo liliandaliwa na Jackson Kalikumtima.

“Mungu alikuwa mwema kwa kweli, maana nilifanikiwa kutwaa taji hilo na kupata zawadi ya shilingi milioni 3.5. Nilishinda vipengele pia vya Kipaji na Vazi Bora la Asili. Hata hivyo, nilisumbuka sana kwenye kuipata hiyo hela, maana nenda rudi zilikuwa nyingi na hata siku naipata, niliogopa.

“Nilikuwa nimekaa pale Best Bite, mtu aliyeniletea hizo hela akaegesha gari nje, akaniita

na kunipa bahasha yenye hela hizo, niliogopa sana maana zilikuwa ni hela nyingi, halafu napewa barabarani, kwa kweli nilitishika sana.

“Kitu kingine kilichonisikitisha, sikupewa ushirikiano wakati najiandaa kwenye mashindano ya dunia ambayo yalifanyika Misri mwaka ule. Hata siku naondoka, sikusindikizwa na yeyote, nililetewa bendera ya taifa uwanja wa ndege, lakini nashukuru, nilipofika Misri wale waandaaji waliponiona tu, wakasema nina nafasi nzuri maana niko vizuri.

“Kule nilipata msaada mkubwa kutoka kwa mtu mmoja anaitwa Gedion Shayo, ndiye alikuwa akinipa moyo na kunipa mbinu. Kule kulikuwa na washiriki kutoka mataifa 42 duniani, nashukuru pia nikaingia Top 15, halikuwa jambo dogo, lakini nilifurahi zaidi baada ya kushinda kipengele cha Miss Photogenic World na nikaingia Top 5.

“Kwa kuwa ilikuwa ni mara yangu ya kwanza na nilifanya vizuri, nikapata connections nyingi kutoka Italia, India, America, Canada na Denmark. Ushindi ulinipa mzuka kiasi kwamba sikutaka kuendelea na masomo ya digrii, nikajikita zaidi kwenye uanamitindo.

“Septemba 2014 nikaenda zangu Afrika Kusini kuangalia namna naweza kufanya kazi huko, kulikuwa na mamodo wa Kitanzania kule nawajua Daxx Cruz na Lotta Mollel ambao wote wako na Ice Models ya Johannesburg, nilipoenda kwenye kampuni yao hiyo, wakasema mimi ni mfupi.

“Nikapelekwa Boss Models, wakanikubali na baada ya msoto sana wakanipa mkataba wa miaka mitano. Nimeshafanya kazi nyingi sana na sasa nipo likizo lakini naangalia namna ya kuingia Marekani na Ulaya, connections zipo nyingi, lakini wale jamaa zangu wa Boss ndiyo watakaonipeleka nafikiri ni Italia, Marekani au Uingereza.

“Kuna wakati nilipata sana msoto kwa sababu sikuweza kupata kazi na kazi za mitaani siyo rahisi kwa sababu elimu ya Tanzania haiwezi kukupatia ajira Afrika Kusini. Nikalazimika kufanya kazi katika klabu za

usiku za kuwakaribisha wageni, kidogo maisha yakawa yanakwenda.

“Kazi kubwa kabisa ambayo nimewahi kufanya na kulipwa fedha nyingi ni tangazo ambalo tulifanya na Kampuni ya Simu ya Cell C, ni kampuni kubwa kule, nililipwa kiasi cha Rand 37,000. Baada ya kukaa sana Johannesburg, niliazimwa kwa muda kwa jamaa wa Full Circle Models ya Cape Town, ambako nilifanya kazi nyingi kwa miezi tisa na kule nilikutana na wanamitindo wa kimataifa kutoka mataifa mbalimbali ambako nilipata uzoefu zaidi.

“Kitu kimoja ambacho nimejifunza ni kuwa Tanzania ni nchi yenye heshima kubwa sana nje, lakini wenyewe hatuoni. Ninapowaambia wanamitindo wenzangu kuwa natoka Bongo, wanashangaa sana na wanasema nchi yetu ni nzuri. Baadhi ya marafiki zangu nilipowaambia nimerudi nyumbani, wanataka kuja ili waende kwenye vivutio vya kitalii.

“Nimewahi kukutana na Millen, ilikuwa kwenye hafla ya BET 2015, lakini zaidi ya kusalimiana hakuna kingine tuliongea, ila Flaviana Matata nimewahi kuwasiliana naye na ananisaidia maswali machache ninayomuuliza.

“Zamani nilikuwa nikisikia wanamitindo wakubwa kama Naomi Campbell nilikuwa siwazi kama naweza hata kukaribia walipo, lakini nilipo sasa siko mbali nao, ni suala la muda tu, lakini nina imani nitakutana na kufanya kazi na mastaa wakubwa tu duniani.

“Wito wangu kwa wasichana wenzangu, kuna ajira kubwa sana kwenye urembo na uanamitindo na hii ni kazi kama kazi zingine, inalipa. Wazazi wawaruhusu watoto wao wakionyesha kuipenda sanaa hii, siyo umalaya.

Leave A Reply