The House of Favourite Newspapers

Nilichogundua kwa waendesha bodaboda

0

bodaBodaWakati watu walipokuwa wakiendelea kudanga-nyana kimapenzi kwa kisingizio cha Valentain, mimi nilikuwa nafanya utafiti kuhusu ishu moja veri siriaz. Utafiti huu ambao ni wazi utakaa kwenye kumbukumbu za Kitaifa na Kimataifa milele, unahusu hawa ndugu zetu waendesha bodaboda.

Lengo lilikuwa kujua kwa nini waendesha bodaboda hawaogopi kufa wala kuumia. Baada ya utafiti uliochukua siku kadhaa, sasa kwa mara ya kwanza naweza kuweka matokeo haya ya kisayansi hadharani.

Katika utafiti nilioshirikiana na profesa mwenzangu kutoa Uchina tuligundua kuwa kimsingi waendesha bodaboda huzaliwa kama binadamu wengine na hukua katika mazingira ya kawaida kabisa, hivyo ubongo wao na wetu sisi raia wengine hauna tofauti kabisa.

Najua wengi mtabisha hili lakini hayo ndio matokeo ya utafiti wetu. Baada ya mchanganuo wa mambo kadhaa tumegundua kuwa huwa kunatokea mabadiliko makubwa katika mfumo wa ubongo wa mwendesha bodaboda mara tu makalio yake yanapogusa kiti cha pikipiki yake.

Kitendo cha makalio kugusa kiti cha bodaboda kusababisha neva za makalio zipeleke taarifa kwenda sehemu ya ubongo inayoitwa Medula Oblongata na hapa hutokea mchakato wa taarifa za kineva ambazo hupeleka taarifa katika ubongo wa kushoto ambazo huzima sehemu ya ubongo inayohusika na ustaarabu na woga, sehemu hii kitaalam nimeiita Bongoliasis.

Kuzimwa kwa Bongoloiasis husababisha mwendesha bodaboda kuamini kuwa pikipiki ina miguu minneĀ  na ni nyembamba kama nyoka na ina mabawa, hivyo basi haianguki na inaweza kupenya popote bila tatizo, pia inaweza kupaa. Na pia huamini kuwa pikipiki ikianguka hakuna kuumia, ukiumia hapaumi wala hapatoki damu, pakitoka damu ni kidogo tu. Athari hizi huacha mara akiondoka kwenye kiti cha bodaboda.

Utafiti umegundua kuwa pasenja wa bodaboda hupatwa na athari kama hizo mara wakaliapo kiti cha bodaboda, hivyo huwa wanaona yote anayofanya dereva wao ni sawa tu na kamwe hawalalamiki hata pale inapoonekana na ulimwengu wote kuwa wanachezea kifo.

Utafiti unaendelea kuona ni dawa gani itumike kuzuia madhara haya, kumekuwa na mawazo kuwa igunduliwe dawa ya kupaka aidha kwenye kiti chenyewe au kwenye makalio ya hawa jamaa kila asubuhi ili kuzuia athari zilizotajwa hapo juu. Na pia serikali iteuwe ni taasisi ipi ipewe jukumu la kuwapaka hawa jamaa dawa hiyo kila asubuhi kabla hawajapanda bodaboda. UTAFITI BADO UNAENDELEA…

Leave A Reply