The House of Favourite Newspapers

NILICHOKIONA NYUMBANI KWA HAYATI NYERERE

 JUZI Jumapili, Oktoba 14, imetimia miaka 19 tangu kufariki dunia kwa muasisi wa taifa hili na rais wake wa kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.  

Mwalimu Nyerere alifariki katika Hospitali ya St. Thomas jijini London, Uingereza na kunifanya nijiulize kwamba, kwa nini Mungu anawachukua mapema watu wazuri wenye busara na uadilifu mkubwa na kutuachia majambazi ambao kazi yao kuu baada ya kuingia madarakani ni kujilimbikizia mali; wao, familia zao na marafiki zao?

 

Pamoja na upungufu wake wowote aliokuwa nao, mengine yakitokana na udhaifu wa kibinadamu; Kitu kimoja kikubwa ambacho Mwalimu Nyerere aliwapatia Watanzania, ukiacha ukombozi wao kutoka kwa makucha ya ukoloni, ni heshima ya nchi yao mbele ya dunia kwani alikuwa anachukia udhalilishaji wa aina yoyote dhidi ya wananchi wake.

Si mara moja au mbili amewahi kuwatimua wageni waliokuja kufanya kazi hapa au kuwekeza, pale ilipobainika kwamba mgeni huyo alitukana au kuwanyanyasa wananchi wazalendo. Leo hii kitu kama hicho ni nadra sana, mgeni kunyanyasa wananchi mara chache hufanyiwa kitu chochote, wale wanaomtuhumu ndiyo huandamwa na pengine kufukuzwa kazi, iwapo ni wafanyakazi wa umma.

 

Mwalimu aliweza kulinda heshima ya mwananchi. Kwa kiasi kikubwa aliweza kufanya hivyo kwa sababu yeye mwenyewe aliwaongoza wananchi wake kwa uadilifu mkubwa, hakutaka makuu, hasa katika kujilimbikizia mali. Alifanya hivyo ili kutoa mfano kwa viongozi wenzake na hata kusisitiza kwa kuwawekea miiko mikali ya uongozi chini ya Azimio la Arusha.

 

Watanzania wengi wenye umri mkubwa au wanajishughulisha na historia au kwa kusoma vitabu, bado wanayafahamu yote hayo. Kwa wanaomkumbuka, hakuna anayeweza sasa hivi kusema bila kutafuna maneno kwamba katika utawala wake Mwalimu alijilimbikizia mali. Hakuna.

 

Kama wapo, ni waongo wakubwa, wanafiki waliokubuhu, wenye ajenda zao za siri. Mwalimu Nyerere na familia yake waliishi maisha ya kawaida tu. Binafsi nakumbuka kwa mara ya kwanza nilifika nyumbani kwa Mwalimu Nyerere Msasani mwaka 1996 nikiwa na mjukuu wake Jacton Manyerere, mwandishi wa habari mwenzangu wakati akiwa anaishi na rais mstaafu.

Siku hiyo pia nilikuwa mmoja katika kundi la waandishi wa habari aliowaita kuzungumzia suala la hoja ya kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika ilioanzishwa na kikundi cha Wabunge kilichoitwa G55. Niliingia katika nyumba ya Mwalimu Nyerere; ilikuwa nyumba ya kawaida tu, kama zile za maeneo ya Ilala au Mwananyamala ambapo mpita njia hana sababu ya kulitupia macho mara mbili.

 

Niliona kwa macho yangu baadhi ya vioo vya madirisha ya luvas (louvre) vimevunjika, nyavu zake za kuzuia m’bu zimechanika, huku rangi ya kuta imepauka. Binafsi nikafikiri labda jengo hili ni la walinzi na wafanyakazi wa Mwalimu na kudhani kuwa makazi yake halisi yalikuwa nyuma ya jengo hilo. Fikra hizi zilifutika muda mfupi baada ya kukaribishwa kwenye varanda iliyotazamana na Bahari ya Hindi kwa mbali, hapo ndipo ilikuwa sehemu alipokuwa akikutana na kuongea na viongozi mashuhuri duniani wakati wa uongozi wake.

Baada ya muda tukatangaziwa ujio wa Mwalimu. Punde tukamuona anateremka ngazi kutoka ghorofa ya juu akifuatana na katibu muhtasi wake wa miaka mingi; Mwingereza, Joan Wickens na msaidizi wake mwingine wa kiume. Akatusalimia kwa kutushika mikono wote, nami ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kupeana naye mkono na akatuashiria kuketi. Wengine waliketi, wengine walisimama kwa kuwa viti havikutosha.

 

Aliketi katika kiti chake cha kubembea (rocking chair) akiipa mgongo Bahari ya Hindi. Kuna baadhi yetu walipata bahati ya kukaa katika viti vya sofa kama vitatu hivi… viti ambavyo, pamoja na kile kiti chake cha kubembea, vilikuwa vimechoka, na hali iliyoo-nyesha kulipaswa kuwepo kwa samani mpya. Baada ya kuketi, mkutano ukaanza lakini mawazo yangu yalikuwa kwingine kabisa; nikijaribu kuyatuliza akilini yale niliyoyaona.

Ilikuwaje mtu huyu maarufu, shujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika na ambaye hata baada ya kustaafu uongozi, tena kwa hiari yake mwenyewe aliendelea na umaarufu wake kwa kushikilia msimamo wake wa uongozi wa kimaadili na visheni yake ya ujamaa, kuridhika kuishi katika mazingira duni kama yale?

 

Na bila shaka mazingira kama haya ndiyo alikuwa akiishi hata wakati akiwa rais, tabia inayoeleza jinsi Mwalimu alivyowapiku viongozi wengi sana duniani katika uadilifu na kujinyima. Kwa vipi alikataa maisha ya anasa?

Wakati nikimsikiliza Mwalimu akitoa mashambulizi yake dhidi ya kikundi cha G55 ambao alisema walikuwa wanadhamiria kuuvunja Muungano, alisema labda hiyo itokee juu ya kaburi lake. Wakati anahutubia, kuna wakati nilijisahau na kukasirika moyoni na kujiuliza kwa nini viongozi aliowakabidhi madaraka waliamua kuyatelekeza makazi ya Mwalimu katika hali hii?

Itaendelea wiki ijayo.

MAKALA: Elvan Stambuli

Comments are closed.