ILIPOISHIA
Kesho asubuhi ilipofika, Dickson akaniaga, akaniambia kwamba siku hiyo asingefanya kazi yoyote ile bali anaondoka kwa ajili ya kwenda kumleta huyo mtu, hivyo nikabaki na presha kubwa.
SONGA NAYO…ILIPOISHIA
Kesho asubuhi ilipofika, Dickson akaniaga, akaniambia kwamba siku hiyo asingefanya kazi yoyote ile bali anaondoka kwa ajili ya kwenda kumleta huyo mtu, hivyo nikabaki na presha kubwa.
SONGA NAYO…
Nilikaa pale Ubungo na kuanza kumsubiria Dickson aliyeniambia asingechukua muda mrefu mpaka kurudi mahali hapo. Kama nilivyokwambia kwamba nilikuwa na presha kubwa, hakukuwa na kitu kingine nilichokifuata jijini Dar es Salaam zaidi ya utajiri tu, hivyo kuniambia kwamba angerudi akiwa na mtu ambaye angenifanya nitajirike, kwangu ilikuwa furaha tele.
Nilikuwa na presha kubwa, kila wakati nilikuwa nikiangalia saa yangu, hakukuwa na siku ambayo niliona mshale wa dakika ukienda taratibu kama siku hiyo, nilikuwa na presha kubwa na kitu nilichokitaka kwa wakati huo ni kuonana na huyo mtu na kumwambia kile nilichokitaka.
Baada ya kusubiri kwa saa tatu ndipo Dickson akarudi huku akiwa na huyo mtu. Alikuwa mwanaume mtu mzima, mwenye ndevu nyingi ambaye alionekana kuwa wa kawaida sana kiasi kwamba nikashangaa, iweje mtu huyo anipe mimi utajiri na wakati yeye mwenyewe alionekana kuwa mtu wa kawaida sana.
Wakati nikijiuliza hayo yote, mwanaume huyo, hata kabla ya kuzungumza nami, akatoa tabasamu pana usoni mwake, tabasamu lililoonesha matumaini makubwa kwamba nisiwe na wasiwasi kwani tayari nilipata nilichokitaka.
“Naitwa bwana Hassani Mudi…” alijitambulisha huku akiniangalia kwa uso wenye tabasamu hilo pana.
“Naitwa Zakia…” nilimwambia, na mimi nikatoa tabasamu pana vilevile.
Dickson akaanza kuniambia kwamba huyo ndiye alikuwa mtu aliyeniambia kwamba ningepata utajiri kupitia yeye, nilipomwangalia, bado nilikuwa na maswali mengi ambayo hayakuwa na majibu.
Huyo mzee akaniambia niende naye pembeni kwani suala ambalo nililitaka halikuwa la kulizungumzia juujuu, ilitakiwa tutulie sehemu na aniambie kila kitu, nikakubaliana naye hivyo Dickson kutulia pembeni akitusubiri.
“Kweli unataka kuwa tajiri?” lilikuwa swali lake la kwanza kuniuliza.
“Ndiyo!” nilimjibu huku nikionekana kumaanisha nilichomwambia.
“Kweli?” aliniuliza.
“Ndiyo!”
“Sidhani kama unataka utajiri…” aliniambia.
“Kweli tena, nataka kuwa tajiri…” nilimwambia kwa sauti yenye msisitizo kabisa.
“Zakia, huna moyo, huna moyo, unaonekana tu…”
“Moyo ninao, nipo tayari kwa lolote lile.”
Niliposema hivyo, yule mzee akaanza akacheka sana, sikujua alikuwa akicheka nini, sijui kama alifurahishwa na jibu langu au la. Nilibaki nikimwangalia kwa mshangao, yeye mwenye aligundua kwamba nilikuwa nikijiuliza mengi kuhusu kicheko chake.
“Eti una moyo! Moyo gani na wakati unaogopa hata mende?” aliniuliza.
“Siogopi mende…nimetoka Morogoro mpaka hapa kwa ajili ya kutafuta utajiri tu, jua kwamba nina kiu ya kuwa tajiri, nipo tayari kufanya lolote ili nipate huo utajiri,” nilimwambia.
“Hata kuua?” aliniuliza.
“Sidhani, ila nikiambiwa kwamba nikimuua huyu napata utajiri, nitaua tu, sitokuwa na budi,” nilimwambia.
Nilichokuwa nikikiongea, nilimaanisha kutoka moyoni mwangu, kwa wakati huo nilikuwa tayari kwa lolote lile, kiu kubwa ya kuwa tajiri ilikuwa imenikamata. Mzee Hassani akaniambia kwamba jioni ya siku hiyo angenifuata hivyo nijiandae kwani kuna sehemu nilitakiwa kwenda naye, hilo halikuwa tatizo, nikakubaliana naye, akazungumza kidogo na Dickson kisha kuondoka, ndiyo kwanza muda huo ilikuwa saa saba mchana.
Aliniacha na mawazo tele, kichwa changu kilivurugika kabisa, wakati mwingine nilikuwa namuamini huyo mzee kwamba angenifanya kuwa tajiri mkubwa lakini wakati mwingine nilikuwa na wasiwasi kwamba asingeweza kufanya hivyo.
Kama kweli yeye alikuwa akitoa utajiri, kwa nini yeye mwenyewe hakuwa tajiri? Kama alikuwa akitoa utajiri, kwa nini Dickson hakuwa tajiri na wakati alikuwa rafiki yake wa karibu? Kila nilichojiuliza, nikawa na uhakika kwamba inawezekana mzee huyo alikuwa muongo.
“Dickson…unamuamini kweli huyu mzee?” nilimuuliza Dickson.
“Ndiyo!”
“Kweli atanisaidia?”
“Sana tu…kuna marafiki zangu kama watano, kawasaidia na sasa hivi ni matajiri wakubwa hapa mjini,” aliniambia.
“Sasa kama yeye anatoa utajiri, kwa nini na wewe asikupe? Au hutaki kuwa tajiri?” nilimtupia swali.
“Nataka!”
“Sasa kwa nini hujamwambia akupe?”
“Basi tu, nataka utajiri ule wa kuutafuta kwa nguvu zangu ili baadaye niwe na ushuhuda jinsi nilivyosota,” aliniambia huku macho yake yakionekana kuwa na jambo lililojificha.
Sikutaka kujali sana, nilichokuwa nikikiangalia ni maisha yangu tu kwani kwenye riziki za kuwa na maisha mazuri, Mungu aliwapa wale waliokuwa na kiu kubwa kama niliyokuwa nayo kipindi hicho.
Basi baada ya saa kadhaa, mzee Hassani alirejea akanichukua na kuanza kuondoka naye. Kumbuka kwamba kwa kipindi chote tangu nifike Dar es Salaam sikuwa nimetoka ndani ya kituo kile, hivyo kutoka ndipo nikaanza kuona mazingira halisi ya jiji hilo.
Lilikuwa zuri, lililopendeza machoni mwangu.
Mzee Hassani alifika na gari lake na kuliegesha nje. Tulipotoka, tukapanda na kuondoka, tulipoelekea kwa kipindi hicho sikuwa nikipafahamu ila kwa sasa, ninapajua mno, palikuwa ni Bunju.
Njiani tulikuwa tukizungumza mambo mengi, katika kila sentensi aliyoongea ilionesha alikuwa miongoni mwa watu waliojiamini kwa kila walichokuwa wakikifanya. Sikutakiwa kuwa na hofu hata kidogo.
Tulikwenda mpaka tulipofika sehemu iliyokuwa imeunganishwa na barabara moja ya vumbi, tukaiacha barabara kuu na kuifuata hiyo, tulikwenda mpaka tukaanza kuingia sehemu iliyokuwa na miti mingi.
Sikuwa na uhakika kama huko kulikuwa na watu walikuwa wakiishi, kulikuwa kimya sana, hatukusimama, tuliendelea kuifuata barabara hiyo ya vumbi mpaka kufika sehemu ambayo barabara ilifika mwisho, sasa tukaanza kuelekea katika njia ambayo haikuwa rasmi, nikaanza kushikwa na hofu, nikahisi kuna hatari mbele yangu! Mzee Hassani hakutaka kuzungumza tena, naye alikuwa kimya, macho yake yalikuwa mbele, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, ila kwangu, nilitamani nirudi. Eti huko ndiko kulikuwa na utajiri! Nikasubiri nione nini kingetokea.
Je, kiliendelea nini? Usikose kufuatia Jumanne ijayo.