Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike-21
ILIPOISHIA
Hakukuwa na mtu aliyejibu swali lake, kila mmoja akabaki kimya. Nilibaki nikijiuliza juu ya ya mahali pale kutetemeka. Wakati sijapata jibu, nikaisikia sauti ile ikiniambia tena:
“Jina langu ni kuu, jina langu lina utukufu. Kuna kipindi kitafika, nitakutoa katika shimo ulilokuwemo, wewe si mtu wa kuishi humo,” nilisikia sauti hiyo ikiniambia, ghafla nikasikia upepo mkali, hakukuwa na mtu mwingine aliyeusikia zaidi yangu, nikasikia ikiniambia maneno ya mwisho yasemayo:
“Nitakurudia tena muda na wakati kama huu.”
Ukimya ukatawala.
ENDELEA NAYO
Mara baada ya tukio hilo kutokea, hapo ndipo nilipoamini kwamba Mungu alikuwa na nguvu kubwa, kitendo cha mahali pale kutetemeka mara baada ya kulitaja jina lake, nikaona kabisa kule nilipokuwa hakukuwa sahihi hata kidogo, nilitakiwa kuondoka haraka iwezekanavyo.
Ila wakati nayafikiria hayo bado nilikumbuka kwamba nilikuwa na utajiri wa kishetani, sikutakiwa kuuacha kwa sababu bila kuwa tajiri kama nilivyokuwa maisha yangekuwa ya shida mno, moyo wangu ukagawanyika, upande mmoja ukatamani kumrudia Mungu lakini upande mwingine ukatamani sana kuendelea kuishi maisha niliyokuwa nikiishi kwani kupitia fedha, nilianza kuheshimika sana.
Siku hiyo ikapita na kurudi nyumbani, nilikuwa na mawazo tele na muda mwingi nilikuwa namfikiria yule mtoto, moyo uliniuma sana lakini sikuwa na la kufanya, kuna wakati mwingine nilipokuwa nikikaa, taswira ya mtoto yule ilinijia kichwani, alikuwa akinililia sana kiasi kwamba nikabaki nikiogopa.
“Kisa fedha umeniua…” niliiona taswira ya mtoto yule kichwani mwangu, ilisimama mbele yangu, alikuwa akilia mno.
Nilibaki kimya, moyo wangu ulikuwa kwenye maumivu makali, hakika alistahili kuishi, hakutakiwa kuuawa kinyama kama nilivyokuwa nimemfanyia, nilipoiangalia mikono yangu, kitu cha ajabu ilionekana kujaa damu za yule mtoto.
Siku ziliendelea kukatika huku nikiishi katika maisha ya hofu mno, nilikuwa tajiri lakini sikuwa na amani na muda mwingi nilionekana kuwa na mawazo tele.
Baada ya kuendelea kuishi katika maisha hayo, siku kadhaa mbele tukaambiwa kwamba kulikuwa na mkutano mkubwa ambao ulitakiwa kufanyika nchini Marekani.
Mkutano huo ulituhusu sisi watu tuliokuwa katika dini ya Illumiterant ambayo kazi yetu kubwa ilikuwa ni kumwabudu shetani. Sikuwahi kufika nchini Marekani, japokuwa nilikuwa na fedha nyingi lakini bado nilikuwa na imani kwamba mtu yeyote ambaye alikuwa na uwezo wa kufika katika nchi hiyo ilikuwa ni lazima uwe msomi.
Sikuwa nimesoma, sikuwahi kupelekwa darasani kwa kuwa baba yangu hakuamini katika elimu, nilibaki nikijiuliza ingekuwaje katika siku yangu ya kwanza kufika nchini humo? Hakika niliona kama ndoto ambayo kipindi hicho ilitakiwa itimie.
Hatukuhangaikia viza. Ngoja nikwambie kitu kimoja. Unapokuwa katika dini hii, kila kitu wanashughulikia wao, kuhusu viza, pasipoti na vitu vingine wao ndiyo wanafuatilia, tena si kwa kwenda ofisini huko bali wanaletewa mpaka hapo kanisani.
Kumbuka hiyo ilikuwa dini kubwa, yenye watu wengi duniani, tena wale watu maarufu na hata viongozi mbalimbali wa nchi nyingi hapa duniani. Kuhusu mambo madogo kama ya hati za kusafiria pamoja na vibali vingine vyote vilikuwa chini yao.
Baada ya siku kadhaa, nikapewa taarifa kwamba kila kitu kilikuwa tayari na kilichokuwa kikisubiriwa ni safari ya kwenda huko Marekani. Nilijiandaa vilivyo, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kutoka nje ya Tanzania, kuna kipindi nilihisi kwamba nilikuwa kwenye ndoto ambapo baada ya muda mfupi ningeamka na kujikuta nikiwa kitandani kijijini lakini ukweli ni kwamba kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kiliendelea katika maisha halisi.
Siku ambayo ndiyo tulitakiwa kufanya safari, nikaelekea mpaka uwanja wa ndege ambapo nilichukua ndege ya Shirika la Ndege la KLM na kuanza safari ya kwenda nchini Marekani.
Katika hili naomba nizungumze kitu kimoja. Huwa kwenye dini ile kuna aina mbili ya vikao, kuna kikao kinachoitwa Community, hicho ni kikao kinachowakutanisha wanachama wengi wa kanisa hili kwa watu wa Afrika, yaani kuna kipindi sisi tunaoishi Afrika tunakutana na kupanga mambo yetu, huko tutapanga ni jinsi gani ya kuendelea kuiteka dunia kutokana na mambo yetu mengi, mipango ambayo inapangwa kabla ya kukutana.
Ukiachana na Community, kuna kikao kikachoitwa Together, hiki ni kikao ambacho kinawakutanisha wanachama wote duniani. Wote tuliokuwa katika nchi mbalimbali tunatakiwa kufika sehemu husika ambapo mara nyingi tunafanyia nchini Marekani na kikao hiki hutokea mara mbili kwa mwaka.
Huwa kunakuwa na sadaka ya kafara na kila kipindi huwa na bara moja linalotoa kafara. Katika kipindi hiki tulichokwenda, Bara la Australia ndilo lililokuwa likihusika katika kuleta kafara, ilikuwa ni lazima wakusanye watu sita, kutokana na mgawanyiko wa mwaka na kisha kuwapeleka katika mkutano huo ambapo watatolewa kafara.
Siku iliyofuata nikapanda ndege na kuanza safari ya kuelekea nchini Marekani, pale nilipokaa, nilikuwa peke yangu, hakukuwa na mtu mwingine kwani ndege haikuwa na abiria wengi.
Ndege ilikata mawingu angani na baada ya saa kadhaa, tukafika katika Jiji la Nairobi nchini Kenya ambapo baadhi ya abiria wakaingia ndani ya ndege tayari kuelekea nchini Marekani pamoja nao.
“Habari yako!” nilimsikia mwanaume akinisalimia. Nikageuka kumwangalia.
Macho yangu yakakutana na sura ya mwanaume mzuri sana, alikuwa ana asili ya kiarabu, alikuwa akiniangalia huku akitabasamu, uzuri wake naweza kusema kwamba sikuwahi kuuona sehemu yoyote ile katika dunia hii, nilimwangalia kwa umakini hata kujibu salamu yake nikashindwa.
Ndiyo kwanza tulikuwa Nairobi nchini Kenya na yeye alikuwa amepanda ndege mahali hapo. Nilikuwa kama mtu aliyekuwa na kigugumizi, kila nilipotaka kuitikia salamu yake, nilishindwa kwani uzuri wake wa sura ulinipagawisha mno.
“Nimekusalimia, habari yako dada,” alinisalimia tena, tabasamu lake likaongezeka usoni mwake.
“Salama tu, karibu,” niliitikia na kumkaribisha tena, macho yetu yalipogongana kwa mara ya pili, mapigo ya moyo yakazidi kuongezeka, kwa kifupi ni kwamba nilianza kumpenda na kumuhitaji maishani mwangu. Swali likawa, je alikuwa ameoa au alikuwa na mchumba? Na yeye alikuwa safarini, je kule nilipokuwa naelekea au la! Kila nilichojiuliza, nikakosa majibu.
****
Kiukweli nilikuwa sijiwezi moyoni mwangu, nilimwangalia mwanaume yule mara mbilimbili na kujiuliza kama kweli alikuwa binadamu au jini. Mapigo yangu ya moyo yaliendelea kudunda kwa nguvu mpaka kuna wakati nilihisi kama yangeweza kuchomoka.
Kama ni nyota, basi nyota yake ilikuwa kali mno na iliikimbiza nyota yangu kwa kiasi kikubwa sana. Nilimwangalia kwa umakini lakini yeye wala hakuwa na habari, aliendelea kufanya mambo yake, kiukweli nilitamani kumwambia tuzungumze kwani mwenzake kipindi hicho nilikuwa hoi.
“Unaelekea wapi?’ aliniuliza mwanaume huyo, Kiswahili chake kilikuwa kizuri na sidhani kama kweli alikuwa Mkenya.
“Naelekea Marekani, wewe?” alinijibu na kuniuliza.
“Hukohuko! Nakwenda New York kisha nitaruka Texas,” alinijibu, muda wote alikuwa akitoa tabasamu lililonifanya niwe hoi.
“Ooh! Oke!’
“Na wewe?”
“Nakwenda Florida,” nilimjibu.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mazoea yetu, tulikuwa tukizungumza sana kana kwamba tulikwishawahi kuonana miaka kumi iliyopita, hakuna aliyetaka kuonekana mnyonge katika mazungumzo, tulizungumza mpaka watu wengine wakaonekana kutushangaa.
Moyoni mwangu niliridhika kabisa, kuna wakati nilijiona kuwa mtu mwenye bahati kuliko hata yule aliyeshinda mamilioni ya shilingi kutokana na jinsi nilivyokuwa nikizungumza pamoja na mwanaume huyu aliyejitambulisha kwa jina la Majeed.
“Ninapenda kukupa kampani hata tukiwa huko Marekani, hivi itawezekana kweli?’ aliniuliza.
“Hahah! Kwa nini isiwezekane!”
“Mmh! Isije ikawa mke wa mtu halafu sumu yote nikawekewa mimi,” aliniambia.
“Hakuna bwana! Sijaolewa wala nini, nipo singo,” nilimwambia.
“Kwa maana hiyo hata mpenzi huna?”
“Sina kabisaaaa…”
“Acha uongo, inakuwaje uwe singo na wakati u mzuri namna hiyo?” aliniuliza huku akiniangalia kwa macho ya kunichunguza.
“Ni maamuzi tu.”
“Mh! Aya bwana!”
Safari ilikuwa ikiendelea mpaka tulipofika nchini Uholanzi ambapo hapo tulitakiwa kubadilisha ndege, yaani kwa wenye lugha yao husema kupata connection nyingine ya ndege na kuendelea na safari.
Mahali ambapo tulikaa, tuliagiza chakula na kuletewa, tulikula na kunywa kwa furaha, tulionekana kama mume na mtu na wakati ndiyo kwanza hiyo ilikuwa mara yetu ya kwanza kuonana.
Nakumbuka tulikaa Uholanzi kwa saa mbili ndipo tukaitwa katika ndege nyingine ya Shirika la KLM na safari kuendelea kama kawaida, hapo tukaanza kuitafuta Hearthrow, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Uingereza uliokuwa katika Jiji la London.
Kutoka hapo Uholanzi mpaka Uingereza tulichukua saa mbili, tukafika na hivyo kuunganisha na ndege kuelekea nchini Marekani kwa kuivuka Bahari ya Atlantiki. Mpaka tunaanza kuitafuta Marekani tayari tulitumia saa ishirini na tatu lakini kitu cha ajabu sikuwa nimelala kabisa, muda wote tulikuwa tukizungumza pamoja na hakukuwa hata na mtu mmoja aliyejisikia kuchoka.
Safari iliendelea mpaka tunaingia nchini Marekani, tayari tulitumia saa nyingine tano, tulipofika tu katika Uwanja wa Ndege wa JFK, sikutakiwa kubaki mahali hapo, nilitakiwa kupanda ndege nyingine na kuelekea Florida ambapo ndipo kulikuwa na kikao chetu.
“Kwa hiyo mpenzi?” nilimuuliza mara baada ya kuteremka, hata hilo jina la ‘mpenzi’ lilinitoka tu mdomoni.
“Basi sawa, naomba tuachane hapa, ila kesho, nitakuja kukuona,” aliniambia.
“Hakuna tatizo.”
Tukaagana kwa mabusu kemkem kisha kupanda ndege na kuelekea Florida. Njiani nilikuwa na mawazo tele, Majeed alinipagawisha sana, aliiteka akili yangu mpaka kuona sili silali kwa ajili yake.
Kipindi hicho cha kwenda Florida nilijiona mpweke sana, sikuwa kama kipindi cha nyuma, hata kama ungeniangalia ungegundua kwamba sikuwa na furaha kabisa, nilikuwa mnyonge kupita kiasi.
Tulitumia saa mbili mpaka kufika, harakaharaka nikateremka kutoka ndani ya ndege na kwenda nje ambapo huko nikamkuta mtu akinisubiri huku akiwa na bango lililoandikwa jina langu.
“Are you Zakia?” (wewe ni Zakia?) aliniuliza, nikamjibu kwa kutingisha kichwa mimi ndiye.
Tukaingia ndani ya gari na kuanza kuelekea hotelini. Njiani nilikuwa kimya, macho yangu yalikuwa yakiangalia huku na kule, nilishangazwa na jinsi jiji hilo lilivyokuwa.
Nilihisi kama nilikuwa peponi na ilikuwa ngumu kuamini kama pale nilipokuwa ilikuwa duniani, kila kitu nilichokuwa nikikiangalia, kilionekana kuwa kigeni machoni mwangu, nilibaki na mshangao mkubwa mno na wakati mwingine nikaanza kumkufuru mpaka Mungu.
Tulipofika hotelini, nikateremka na kisha kuanza kuingia ndani huku nikitangulizana na yule mwanaume aliyekuja kunipokea. Yeye ndiye alikuwa mkalimani wangu ambaye alinisaidia kuuliza na hata kujibu maswali niliyokuwa nikiulizwa, baada ya hapo, nikaingia hotelini.
Chumba kilikuwa kizuri mno, kilinishangaza na namna kilivyokuwa, nadiriki kusema kwamba tangu nizaliwe sikuwahi kuingia katika chumba kilichokuwa na uzuri kama hicho, nilifurahi sana lakini niliona kama kutokukamilika kwani kama ningekuwa na Majeed chumbani hapo basi ingekuwa furaha sana kwa usiku huo.
Baada ya kukaa na kumfikiria sana Majeed, nikajilaza kitandani ambapo nikapitiwa na usingizi, nilipokuja kushtuka, tayari ilikuwa asubuhi. Nikatoka kitandani na kwenda kuoga bafuni, nilikaa katika sinki kubwa huku nikijimwagia maji taratibu, huku nikiwa huko, nikaanza kusikia simu ya mezani ikiita, harakaharaka nikaenda kuipokea, nilipoipokea, nikamsikia dada akiniuliza maswali, sikumuelewa alichoniambia ila hapohapo akalitaja jina la Majeed. Nikashtuka.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi hapahapa.
Comments are closed.