The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike-22

Baada ya kukaa na kumfikiria sana Majeed, nikajilaza kitandani ambapo nikapitiwa na usingizi, nilipokuja kushtuka, tayari ilikuwa asubuhi. Nikatoka kitandani na kwenda kuoga bafuni, nilikaa katika sinki kubwa huku nikijimwagia maji taratibu, huku nikiwa huko, nikaanza kusikia simu ya mezani ikiita, harakaharaka nikaenda kuipokea, nilipoipokea, nikamsikia dada akiniuliza maswali, sikumuelewa alichoniambia ila hapohapo akalitaja jina la Majeed. Nikashtuka.

SONGA NAYO

Jina lake halikuwa la Kingereza hivyo kuelewa isingekuwa tatizo lolote lile, nilijua kwamba atakuwa akizungumziwa yeye ila kilichonifanya kushtuka, kama alikuwa akizungumziwa yeye, ilikuwaje awe hotelini hapo?

Nilimwambia wazi kwamba nilikuwa nakuja hapo Florida lakini sikumwambia kuhusu hoteli niliyokuwa nikifikia, sasa iweje awe hapo? Nilijiuliza lakini sikupata jibu lolote lile. Wakati nikiwa nimeduwaa, yule dada wa mapokezi akampa Majeed mkonga wa simu.

“Zakia! Upo?” aliniuliza mara baada ya kuchukua simu.

“Ndiyo! Majeed hapo?”

“Ndiyo mpenzi!”

“Mmh!”

“Mbona unaguna?” aliniuliza, bila shaka uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana.

“Umejuaje kama nipo katika hoteli hii?”

“Uliniambia.”
“Nilikwambia? Wakati gani?”

“Tulipokuwa tunaagana, yaani umesahau mpenzi?”

“Mmh!”

“Naomba nije nikusalimie,” aliniambia.

“Sawa. Karibu.”

Nilikuwa na hofu kubwa, sikukumbuka kabisa kama niliwahi kumwambia Majeed juu ya hoteli niliyokuwa nimefikia bali nilichokikumbuka ni kwamba nilimwambia kuwa nakuja Florida kwa sababu kulikuwa na kitu cha kufanya.

Wakati nikiwa kwenye mawazo hayo, hata kabla sijatoka katika eneo la kimeza kilichokuwa na simu, nikasikia mlango ukigongwa, kwanza nilishtuka lakini hofu hiyo ikanipotea baada ya kuhisi kwamba inawezekana akawa mhudumu.

Nilipokwenda kufungua mlango, macho yangu yakagongana na macho ya Majeed. Alikuwa akiniangalia kwa makini na alionekana kuwa na furaha mno ila kwangu nilikuwa na maswali sana kwamba inakuwaje Majeed awe amefika katika korido hiyo kwa haraka namna hiyo? Hata kama angetumia lifti asingeweza kufika kwa haraka namna hiyo mpaka kwenye korido ya kumi na mbili.

“Eeh!” nilijikuta nikihamaki.

“Nini tena?” aliuniuliza huku akiingia.

“Imekuwaje?”
“Kuwaje vipi?”
“Umefika kwa haraka sana katika ghorofa hii,” nilimwambia.

“Nimefika kwa haraka? Kivipi tena jamani? Mbona sikuelewi!” aliniambia huku akiniangalia, wakati huo alikuwa akijiweka kitandani.

Kiukweli nilikuwa na mawazo mengi, wakati mwingine nikahisi kwamba inawezekana Majeed alikuwa jini kwani vitu vilivyokuwa vikitokea vilinipa maswali mengi mno.

Wakati najiuliza hivyo, nikahisi kabisa moyo wangu ukianza kubadilika, kila nilipomwangalia, niliachia tabasamu pana, alinipagawisha sana na wakati mwingine nilibaki nikijiuliza sababu ya kuwa na hofu juu ya mwanaume mzuri kama Majeed, sikutakiwa kuwa na hofu hata mara moja.

“Naomba nikuulize swali kwanza,” aliniambia baada ya mazungumzo ya dakika chache.

“Uliza tu.”
“Umekuja huku kufanya nini?’ aliniuliza.

“Kutembea tu.”
“Hapana! Si kweli na sidhani kama unaniambia ukweli mpenzi,” aliniambia katika hali ambayo nilihisi kwamba alikuwa akifahamu kila kitu.

“Ndiyo hivyo, nimekuja kutembea kwani nimechoka kukaa Tanzania muda wote,” nilimwambia huku nikimsogelea kitandani.

Baada ya kumjibu hivyo, hakuniuliza swali lolote lile zaidi ya kuniangalia na kunitolea tabasamu pana. Nilikuwa na uhakika kwamba alikuwa akifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea, kuna kipindi nilitaka kumuuliza kama alifahamu chochote kile lakini niliogopa.

Alichoniambia ni kwamba alikuja kunichukua na kutaka tuende sehemu fulani kutembea. Kidogo nilimshangaa, kumbuka tulikuwa chumbani, tulikuwa wawili tu ambapo kwa watu wengi wangetamani kufanya mapenzi lakini kwa Majeed, wala hakuwa na mawazo hayo kabisa.

Nikamwambia basi anisubiri niende kuoga, akasubiri hapohapo kitandani. Kiukweli nilijitahidi sana kumuonyeshea kila dalili za kutaka kufanya naye mapenzi lakini alionekana kama kutokunielewa, nilivaa khanga yangu, tena nikiwa nimeishusha, cheni yangu ilionekana vizuri na kwa nyuma kidogo nilijazia lakini wala hakuelewa, hakutaka kabisa kunitazama mara nyingi.

“Twende tukaoge,” nilimwambia kwa sauti nyororo.

“Usijali, nenda kaoge mpenzi,” aliniambia, tabasamu lake halikuisha, bado lilionekana usoni mwake.

Nilipofika bafuni nikaanza kujiuliza kama kweli Majeed alikuwa mwanaume rijali au la, isingekuwa rahisi hata kidogo kwa mwanaume aliyekamilika kuniacha namna ile pasipo kunionyeshea hali yoyote ile ya matamanio, sikutaka kujali sana, nilichukua dakika kumi kuoga, nilipomaliza, nikatoka nje, kitu cha ajabu sasa, eti Majeed hakuwepo pale nilipomuacha, na nilipoangalia mlango, haukuwa umefunguliwa kabisa, sasa kama hakuwepo, alikuwa wapi na alipitia wapi? Mwili wangu ukaanza kuweweseka.

 

Je nini kiliendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

Comments are closed.