The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike-23

Nilipofika bafuni nikaanza kujiuliza kama kweli Majeed alikuwa mwanaume rijali au la, isingekuwa rahisi hata kidogo kwa mwanaume aliyekamilika kuniacha namna ile pasipo kunionyeshea hali yoyote ile ya matamanio, sikutaka kujali sana, nilichukua dakika kumi kuoga, nilipomaliza, nikatoka nje, kitu cha ajabu sasa, eti Majeed hakuwepo pale nilipomuacha, na nilipoangalia mlango, haukuwa umefunguliwa kabisa, sasa kama hakuwepo, alikuwa wapi na alipitia wapi? Mwili wangu ukaanza kuweweseka.

ENDELEA NAYO

Si mimi tu, hata ungekuwa wewe hakika ungesisimka, nilishikwa na butwaa sana, kitendo cha kutokumuona Majeed ndani ya chumba kile kilinishtua sana, wakati nimekaa huku nikijiuliza, nikauona mlango ukifunguliwa na Majeed kuingia ndani.

Nilishtuka, yeye mwenyewe akaligundua hilo, akanisogelea na kuniuliza tatizo lilikuwa nini, sikumjibu kitu chochote kile zaidi ya kumwambia kwamba nilimmisi tu hivyo nilitamani kuona akirudi haraka.

Mkononi mwake alikuwa na mfuko, akaufungua na kutoa choklate, kulikuwa na choklate mbili, moja ilikuwa ile yenye rangi ya kawaida, kahawia ila nyingine ilikuwa na rangi nyekundu, ilifanana kabisa na damu, nikashtuka.

“Mh! Chokleti nyekundu!” nilijikuta nikimuuliza.

“Hujawahi kuona?” aliniuliza.

“Hapana!”
“Basi karibu Marekani! Utakutana na vitu vingi vya kushangaza,” aliniambia kwa sauti ndogo huku lilelile tabasamu lake likiendelea kuwepo usoni mwake.

Kiukweli nilishangaa sana, niliwahi kuona chokoleti na hata kuzila lakini katika maisha yangu sikuwahi kuona chokoleti iliyokuwa na rangi nyekundu, tena wekundu wenyewe ulikuwa kama damu kabisa.

“Naomba nikulishe mpenzi,” nilimwambia huku nikiichukua chokleti yangu na kutaka kumlisha, kitu cha ajabu, akakataa.

“Hupendi?” nilimuuliza.

“Napenda….” alijibu.

“Tatizo nini sasa?” nilimuuliza.

“Hakuna tatizo.”
Nadhani kati ya watu waliokuwa wakiongoza kwa kutabasamu basi Majeed alikuwa namba moja, muda wote aliachia tabasamu pana usoni mwake. Alinidatisha sana kwani uzuri wake ulikuwa wa ajabu kabisa na ninakiri kwamba sikuwahi kumuona mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa yeye.

Tulikula chokleti mpaka tulipomaliza ambapo tukatoka na kuelekea kutembea tu. Njiani, tulikuwa tukiongea mambo mengi mno, aliniambia kwamba yeye alikuwa mfanyabiashara ambaye mara nyingi alikuwa akisafirisafiri, alikuwa Mtanzania ila hata pale Nairobi alipokuwa amepanda ndege alitoka kukutana na wafanyabiashara wenzake na kupanga mambo yao ya kibiashara.

Nilifurahi sana kwani niliona kwamba hatimaye nilimpata mfanyabiashara mwenzangu, tena wa kimataifa ambaye angenifundisha mambo mengi na hatimaye na mimi kuwa kama yeye.

Siku hiyo ya Alhamisi tulitembea na kurudi hotelini ambapo nilijilaza kitandani na kukaa mapozi ya kumuita kitandani hapo lakini hakutaka kabisa kuja, akaniaga tayari kwa kuondoka.

“Unataka kuondoka?” nilimuuliza kwa sauti ndogo.

“Ndiyo! Natakiwa niwahi, kesho nitapanda ndege kuelekea Dubai,” aliniambia.

“Jamani! Naomba ulale nami mpenzi,” nilimwambia kwa sauti ya kumtaka alale nami kwani nilikuwa tayari kwa kila kitu kipindi hicho.

“Usijali mpenzi, mimi ni wako, hivyo kuna siku tutalala mpaka utachoka,” aliniambia huku akiachia tabasamu, kilichofuata ni kuondoka chumbani hapo.

Kwa kweli nilimshangaa sana, sikuamini kile kilichokuwa kimetokea, hapo ndipo nilipopata mawazo kwamba inawezekana huyu Majeed hakuwa mwanaume kamili kwani kwa jinsi ninavyojua, kama angekuwa mwanaume kamili, asingetaka kuchelewa, palepale kitandani angenirukia na kuanza kuchezacheza kitoto.

Moyo wangu uliumia sana, penzi lake liliniteka sana. Nilibaki katika hali hilo ya mawazo kama dakika arobaini na tano hivi na ndipo usingizi mzito ukanijia na kulala fofofo.

Nakumbuka vizuri sana usiku wa siku hiyo niliota ndoto iliyonisisimuua sana, nilijiona nikiwa kitandani nimekaa, mara ghafla nikamuona mwanaume akiwa amesimama mlangoni, alikuwa mtupu kabisa, japokuwa sikujua alikuwa nani lakini moyo wangu haukuwa na hofu kabisa.

Mwanaume yule akaanza kusogea kule nilipokuwa, alipokuja karibu yangu, kumbe alikuwa Majeed. Moyo wangu ukafarijika, sikuamini kumuona chumbani hapo muda kama huo.

Aliponisogelea pale kitandani, akanishika na kisha kuanza kufanya kile nilichotamani sana kufanya pamoja naye. Kiukweli nilifurahi sana, kitendo kile kilichukua kama dakika arobaini, alipomaliza, akaondoka na mimi kushtuka kutoka usingizini.

“Kumbe nilikuwa naota!” nilijisemea.

Kuna kitu cha ajabu kilichokuwa kimetokea, ile ilikuwa ndoto lakinii sasa nilishangaa kuona kitanda kikiwa shaghalabaghala, nilishindwa kuamini kwani kama kile kitu kilitokea ndotoni, iweje kitanda kiwe vile.

“Mmh! Hivi ilikuwa ndoto au?’ nilijiuliza pasipo kupata jibu lolote lile.

Nikaamka na kwenda bafuni kujimwagia kwani mwili wangu ulikuwa umechoka mno, nilipofika huko, nikajimwagia maji, nilipotoka na kwenda chumbani, nikaanza kusikia manukato mazuri, niliyafahamu kabisa, yalikuwa yaleyale ambayo alikuwa akitumia Majeed, yalinukia vizuri sana.

Nikabaki nikijiuliza, je, Majeed alikuwa ameingia chumbani humo? Kama hakuwepo, ilikuwaje harufu ya manukato yake isikike chumbani mule? Kila nilichojiuliza, nilikosa jibu.

****

Hakukuwa na siku ambayo nilichanganyikiwa kama siku hiyo. Kwa kweli nilibaki nikijiuliza kuhusu manukato hayo sikupata jibu kabisa. Moyo wangu uligawanyika sehemu mbili, upande mmoja uliniambia kwamba Majeed alikuwa jini lakini upande mwingine ulikataa suala hilo kwa nguvu zote.

Sikujua ni upande upi nilitakiwa kuuamini, nilibaki kitandani huku nikiwa na mawazo mengi, nikimfikiria sana Majeed, sijui kama alikuwa akijua hilo au vipi, mara nikasikia simu ikianza kuita, kwa uchovu mkubwa nikaanza kuifuata, nilipoifikia, nikachukua na kuipeleka sikioni.

“Halo! Zakia, upo chumbani? Nakuja, nina habari njema,” nilisikia sauti, hata kabla sijajibu kama nilikuwa chumbani wala kuuliza juu ya habari njema hiyo, hapohapo simu ikakatwa.

Sauti ilikuwa ni ya Majeed, niliizoea sauti yake kwa kipindi kifupi na hata kama angepiga kwa simu nyingine bado ningegundua kwamba ni yeye, nikabaki na maswali mengi juu ya hiyo habari njema aliyotaka kuniambia, ilikuwa habari gani na iliwezekanaje kunihusu mimi na wakati hatukuwahi hata kuambiana mambo mengi ya sirini.

Wakati nimetulia, ghafla nikasikia mlango ukigongwa, nikasimama na kuufuata kisha kuufungua. Macho yangu yakagongana na macho ya Majeed, alikuwa vilevile, kama alivyokuwa jana yake ndivyo alivyokuwa siku hiyo. Tabasamu pana lilikuwa usoni mwake, tabasamu hilo tu likaniondolea hofu moyoni mwangu, nikajikuta na mimi nikianza kutabasamu.

“Huwezi kuamini Zakia,” aliniambia huku akiniangalia machoni.

“Kuamini nini?”
“Niliwaambia wazazi wwangu kuhusu wewe, nikuoe,” alisema.

“Wamesemaje?”
“Wamekubali! Siamini kama wangekubali kirahisi namna ile mimi kuwa na binadamu,” aliniambia, kidogo nikashtuka. Akaugundua mshtuko wangu, hapohapo akaongezea.

“Wewe ni binadamu, na sidhani kama wamekubali mimi niwe na binadamu, si unajua kuna binadamu na watu?” aliniuliza.

“Ndiyo!”

“Yeah! Wazazi wangu ni watu, nasema hivyo sitaki wajue, ila wana roho mbaya kwani nilijaribu kuwapeleka wanawake wawili, wakakataa, sasa wewe umekuwa binadamu, una roho nzuri, mkarimu, mcheshi tofauti na wao, sikuamini kama wangemkubali binadamu, nilidhani wangekataa kwa kuwa nao wana roho mbaya sana,” alisema Majeed, maneno mengi sana kiasi kwamba akanichanganya na kunitoa katika kile nilichokuwa nikikielewa.

Hii nadhani inajulikana kwamba watu wametofautiana, wale wasiokuwa na utu tunawaita watu wa kawaida lakini mtu anapokuwa na huruma, utu na tabia njema tunamuita binadamu na ndiyo maana wanasema ubanidamu kazi, basi ndivyo alivyomaanisha.

“Kwa hiyo mimi ni binadamu?” nilimuuliza huku nikitabasamu kama yeye.

“Ndiyo! Siamini kama una ubinadamu namna hiyo mpenzi,” aliniambia na kisha kunikumbatia.

Siku hiyo kama ilivyo jana yake tulikwenda kutembea kama kawaida yetu, huko, tulishikana kimahaba huku kila mmoja akionekana kufurahia maisha. Kumbuka kwamba siku hiyo ilikuwa ni Ijumaa ambapo usiku wa siku hiyo nilikuwa nikihitajika katika nyumba ya ibada kwa ajili ya kumuabudu shetani katika mkusanyiko wa waumini wengi wa dini yetu.

Tukiwa katika matembezi yetu kulikuwa na kitu kilichokuwa kikinishangaza sana, huyu Majeed hakuwa mtu wa kula chakula chochote kile wala kunywa kinywaji chochote, nilishangaa sana, halikuwa jambo la kawaida kwa binadamu kutokunywa au kula chakula chochote kile.

Hakulalamika njaa wala kiu, mimi mwenyewe nilishindwa hivyo kuna kipindi nilimwambia kwamba nina njaa, alinipeleka kwenye mgahawa na kula, ila yeye, alikataa kula kwa sababu alisema ameshiba.

“Umekula nini?” nilimuuliza.

“Chakula…”
“Kipi tena mpenzi, tangu asubuhi ile mpaka sasa hivi saa kumi na moja, sijakuona ukila, sasa umeshiba kwani umekula nini na chakula gani kinaweza kukaa muda mrefu namna hiyo?’ nilimuuliza huku nikionekana kujawa na mshangao mkubwa.

“Nilikula sana asubuhi…”
“Mmh!”

“Ndiyo baby, naogopa nikila sana, nitavimbiwa,” aliniambia.

Kiukweli ilibidi tu nikubaliane naye kwanii sikuona kama kuna kitu kingine ningeweza kufanya tofauti na hicho. Tulipomaliza matembezi yetu, tukarudi mpaka hotelini ambapo hakukaa sana, akaondoka zake.

Nilikuwa na mawazo juu yake na hata yale mambo yaliyokuwa yametokea kwa kweli yalinipa wakati mgumu sana. Zile pande mbili za moyo wangu ziliendelea kunitesa, ziliendelea kumzungumzia Majeed lakini sikuwa katika upande wowote ule zaidi ya kuchanganyikiwa na kutokujua nini cha kufanya.

“Mmh! Sasa Majeed ni jini au mtu wa kawaida?” nilijiuliza swali hilo, huku nikiwa nafikiria ni jibu gani nililotakiwa kuwa nalo, ghafla nikaanza kuhisi mwili wangu ukianza kutetemeka sana, kama mtu aliyekuwa akihisi baridi kali mno kiasi kwamba mpaka meno yangu yakaanza kugonganagongana.

Hali ile ilinishangaza sana kwani ilikuwa ghafla mno, niliendelea kutetemeka na sikujua ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea mwilini mwangu. Nilichokifanya ni kwenda kuzima kiyoyozi kwani nilihisi kwamba hicho ndicho kilichosababisha hali hiyo.

Sikutaka kubaki hivyohivyo bali nilichokifanya ni kulala kitandani na kujifunika na blanketi kwani baridi lile lilikuwa kali mno na mwili wangu uliendelea kutetemeka kama kawaida.

Kitandani hapo nikapitiwa na usingizi. Nilikuja kushtuliwa na simu ya mezani iliyokuwa ikiita kwa fujo sana, mlio wake ulikuwa tofauti na siku nyingine, ulisikika kitofauti sana kiasi kwamba nikaanza kujiuliza maswali juu ya kile kilichosababisha simu hiyo kulia hivyo.

Nikatoka kitandani, sasa kitu cha ajabu kilichotokea, mwili wangu haukuwa ukitetemeka kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma, nilikuwa mzima wa afya kabisa mpaka mimi mwenyewe nikabaki nikishangaa.

“Zakia, muda umefika,” nilisikia sauti upande wa pili.

Niliposikia maneno hayo tu, nikayapeleka macho yangu katika saa ya ukutani na kugundua kwamba ilikuwa ni saa sita kamili usiku. Nilishtuka, muda ulikwenda kasi sana na wakati nilijiona kulala kwa muda mchache kabisa.

Harakaharaka nikaanza kujiandaa, nilipomaliza, nikatoka chumbani na kuelekea nje ya hoteli hiyo kwa kushuka na lifti, nje nikakutana na gari maalumu ambalo lilifika hapo kwa ajili ya kunichukua.

“Karibu sana,” aliniambia mwanaume mmoja aliyenipokea, aliongea kwa lugha ya Kiingereza, lakini kitu cha ajabu kabisa niliweza kutambua alimaanisha nini.

Nikaingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea huko kanisani. Kiukweli mpaka leo hii ukiniuliza juu ya njia tulizopita mpaka kufika huko kanisani, kwa kweli sikumbuki kwani nina uhakika zile njia tulizopita hazikuwa za kawaida hata kidogo.

Baada ya dakika kadhaa tukafika katika jengo kubwa, ninaposema kubwa ninamaanisha kubwa, mbele kabisa kulikuwa na picha kubwa, hii picha ilimuonyesha mwanaume mmoja alikuwa amesimama, mwili wake ulikuwa mwekundu mno.

Kwa hapa kati alikuwa mwanaume kamili, yaani kifua kipana, lakini miguu yake huku chini ilikuwa tofauti, alifanana na simba na hata ukimwangalia juu kabisa, alikuwa na kichwa cha binadamu, sura ya simba na mapembe na mkononi mwake alishika chumba fulani kama reki ile ya kukusanyia majani baada ya kuyakata.

Moyo wangu haukutaka kujiuliza juu ya picha hiyo, alikuwa shetani ambaye kipindi hicho ndiyo tulikuwa tumekusanyika hapo kanisani kwa ajili ya kumuabudu yeye.

Kanisa hili lilikuwa tofauti na lile la Tanzania, hili lilikuwa na eneo kubwa mno na hapo nje kulikuwa na magari mengi mno. Tukaingia ndani ambapo kwenye floo ya kwanza kabisa tulipewa mavazi maalum ya kuingilia humo, hivyo tukayavaa.

Hayo ni mavazi ya ajabu kabisa, unapoyavaa unajisikia hali ya tofauti kabisa, tuliingia mpaka ndani ambapo wenzangu wakaenda katika kidirisha kimoja hivi, wakaingiza mikono ndani, walipoitoa, ilikuwa imepigwa chapa iliyosomeka 666.

“Hii ni namba ya nini?” nilijikuta nikimuuliza mwanaume mmoja kwa lugha ya Kiingereza, sikuijua lugha hiyo lakini ukiniuliza ni kwa jinsi gani niliizungumza, nitashindwa kukwambia.

“Hii ni tiketi…”

“Ya wapi?”
“Wewe jua ni tiketi! Wewe ni mgeni hapa?” aliniuliza.

“Ndiyo!”

“Ni mara ya kwanza?”
“Ndiyo!”

“Basi ingiza mkono na wewe upigwe chapa hii,” aliniambia mwanaume huyo.

Kiukweli sikuwahi kuwa mtu wa dini na sikujua maana ya alama ya 666, nikaingia mkono katika kitundu kile kwa lengo la kupigwa chata ile, kitu cha ajabu kabisa, sikuweza kupigwa chapa mpaka nautoa mkono wangu, alama ile ya zile namba hazikuonekana mkononi mwangu.

Nilibaki nikishangaa ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, sikuuliza kwa kuwa hata maana ya namba zile sikujua kabisa. Nikaondoka na kwenda ndani ya kanisa lile.

Shetani yupo ndugu zangu na siku hiyo ndiyo nililiamini hilo. Ndani ya kanisa hilo kulikuwa na watu zaidi ya elfu kumi au zaidi, wote walikuwa katika mavazi ya rangi moja, katika viti vyote vilivyokuwa humo, vilikuwa na chapa ya 666 ambazo zilipigwa katika kila sehemu.

Nikakifuata kiti kimoja na kutulia, tukaletewa vitabu vidogo kwa lengo la kuimba nyimbo za kumtukuza shetani, mbali na vitabu hivyo vidogo tukaletewa vitabu walivyoviita Biblia lakini kitu cha ajabu Biblia hizi zilikuwa tofauti kabisa.

Pale mbele kabisa yaani kwa juu ziliandikwa LUSIFA…tena kwa herufi kubwa. Nikashangaa!

 

Je, nini kitaendelea?

Tukutane Alhamisi hapahapa

Comments are closed.