The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike – 5

maiti-cover

 ILIPOISHIA SEHEMU YA NNE

“Kwa hiyo hauna ndugu?” aliniuliza.

“Ndiyo! Ila nakwenda kutafuta maisha…” nilimjibu.

Akanionea huruma, kiukweli macho yake yalionyesha jinsi gani hakutaka mimi niende huko lakini hayakunishawishi niendelee kubaki hapo Ifakara, iwe isiwe ilikuwa ni lazima niendelee na safari ya kuelekea Dar es Salaam, kama wazazi walishindwa kunizuia, basi niliamini hata huyo Mudi naye asingeweza.

“Una nauli sasa?” aliniuliza.

MWAGIKA NAYO HAPA….

“Hapana! Sina nauli…”

Akaingiza mkono mfukoni mwake na kutoa kiasi cha shilingi elfu hamsini na kunipa. Sikufichi, wakati akitoa fedha ile nilimuonea huruma mno, alikuwa katika maisha ya shida, yeye mwenyewe alihitaji fedha sasa ilikuwaje anipe kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo? Nilijisikia hukumu moyoni mwangu.

“Unanipa fedha zote hizi?” nilimuuliza kwa kushangaa.

“Usijali Zakia! Ninakupenda na ndiyo maana nimekupa kiasi hiki cha fedha, chukua tu, katafute maisha, naamini Mungu atakupigania. Ila kumbuka, kila hatua utakayopiga, kila pumzi utakayotoa, kila moyo wako utakapodunda, jua kuna mtu anaitwa Mudi, anaishi Ifakara na ananipenda sana na yupo tayari kwa lolote kwa ajili yangu,” aliniambia Mudi maneno ambayo yalinifanya nione ni jinsi gani alikuwa akinipenda.

Asubuhi ya siku hiyohiyo nikaondoka nyumbani kwake, akanisindikiza mpaka kituoni, hakutaka nilipe nauli, akamwambia utingo wa basi tulilokuwa tunataka kusafiri kwamba alikuwa mume wangu hivyo nisidaiwe nauli, hilo halikuwa tatizo kabisa.

Nikaingia na kutulia katika kiti cha dirishani, macho yangu bado yalikuwa yakimwangalia Mudi aliyekuwa nje. Kwa kumwangalia harakaharaka alionekana kuwa wa kawaida lakini ukweli ni kwamba alikuwa mtu mwenye majonzi sana, kila aliponitupia jicho dirishani, alitamani kuniambia nirudi niishi naye.

“Nitarudi na kukusaidia Mudi, hata iwe vipi, nitarudi kulipa fadhila,” nilijisemea huku basi likiwashwa na safari ya kuelekea Ruaha kisha Morogoro Mjini kuanza.

Siku hiyo nilikuwa na mawazo tele, nilikuwa njiani kuelekea Ruaha ambapo huko ningeteremka kisha kuchukua chumba na kesho yake kuendelea na safari ya kuitafuta Morogoro huku tukipita katika mbuga ya wanyama ya Mikumi.

Niliifikiria familia yetu, nilijua kwamba wazazi wangu walikuwa na mawazo tele, kitendo cha kutokuniona najua kiliibua maswali mengi juu ya mahali nilipokuwa lakini sikutaka kujali kwa kuamini kwamba wakati mwingine tunatakiwa kufanya maamuzi pasipo kuwasikiliza wazazi, kwani kama utawasikiliza, unaweza usifanikiwe hata kidogo.

Safari ya kutoka Ifakara kwenda Ruaha ilikuwa ndefu sana, njiani nililala na kulala, kila nilipoamka bado tulikuwa njiani. Nakumbuka siku hiyo tulitumia saa tano njiani, nilipofika Ruaha, sikutaka kuunganisha safari japokuwa kulikuwa na magari ya kwenda Morogoro, nikaenda kwenye nyumba ya wageni kupumzika.

Huko, hata usingizi haukunipata, nilikuwa na mwazo tele, wakati mwingine nilimfikiria Mudi, alionekana kuwa mwanaume mwenye mapenzi ya dhati ambaye hakutaka niondoke mikononi mwake lakini kutokana na kunikuta nikiwa safarini, hakuwa na budi kuniacha.

“Nikuletee nini dada?” aliniuliza dada wa mapokezi baada ya kumwambia kwamba nilihitaji chakula.

“Niletee chipsi kama zipo…” nilimwambia japokuwa sikuwa hata na hamu ya kula.

Nikaondoka na kuelekea chumbani, baada ya dakika kadhaa, dada yule akaja chumbani na kuniletea chakula hicho. Hata hamu ya kukila sikuwa nayo zaidi ya kukishikashika kisha kukiweka pembeni.

Maneno ya baba ya kunikataza kwenda Dar yakaanza kujirudia kichwani mwangu. Kwa kweli yalinigusa lakini sikuwa na jinsi, iwe isiwe ilikuwa ni lazima niondoke na kuelekea huko, na muda huo ndiyo nilikuwa njiani.

Usiku huo nikalala hapohapo na kesho asubuhi kuanza safari ya kuelekea Morogoro Mjini. Safari ilikuwa ndefu sana ila baada ya saa kadhaa tukafanikiwa kuingia Msamvu ambapo nikateremka, kabla ya kuondoka, kwanza nikaanza kuangalia kila kona.

Sikuwa nimewahi kufika mjini, kitendo cha kuona mazingira mazuri tofauti na kule kijijini nilipokulia, hakika ilinishangaza sana, nilipaona pale Morogoro Mjini kuwa sehemu nzuri sana, sikuwahi kuona maghorofa, kwa mara ya kwanza niliyaona, mambo mengi yaliyoonekana mbele yangu yalinishangaza mno.

“Dada unataka kwenda wapi?” aliniuliza mwanaume mmoja.

“Dar…” nilimjibu kwa kifupi.

“Mbona upo hapa sasa, twende, magari yale kule,” aliniambia mwanaume huyo.

“Kiasi gani?”

“Elfu kumi, unayo?”
“Ndiyo!”
“Basi twende…”
Mwanaume yule akachukua kibegi changu na kuanza kuelekea ndani ya basi moja, sikumbuki liliitwaje. Nikaingia ndani, akanipa mzigo wangu na kisha kutulia kitini. Sikuwa nikiamini kilichokuwa kikiendelea, eti Zakia mimi, leo hii nilikuwa njiani kuelekea Dar. Safari ikaanza.

Kumbuka kwamba sikuwa na ndugu yeyote ndani ya Jiji la Dar es Salaam, nilikuwa nikienda mimi kama mimi, sikujua ningefikia wapi lakini hamu yangu ilikuwa ni kufika ndani ya jiji hilo tu. Njiani, sikutaka kulala, nilikuwa macho japokuwa nilichoka sana, nilitaka kuona huko mwanzomwanzo wa jiji hilo kulionekanaje.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kesho hapa kujua kitakachoendelea katika sehemu ya SITA.

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

halotel-1

Comments are closed.