The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike – 8

maiti-cover

ILIPOISHIA SEHEMU YA SABA

Wakati nikijiuliza hayo yote, mwanaume huyo, hata kabla ya kuzungumza nami, akatoa tabasamu pana usoni mwake, tabasamu lililoonyesha matumaini makubwa kwamba nisiwe na wasiwasi kwani tayari nilipata nilichokitaka.

“Naitwa bwana Hassani Mudi…” alijitambulisha huku akiniangalia kwa uso wenye tabasamu hilo pana.

“Naitwa Zakia…” nilimwambia, na mimi nikatoa tabasamu pana vilevile.

MWAGIKA NAYO HAPA…

Dickson akaanza kuniambia kwamba huyo ndiye alikuwa mtu aliyeniambia kwamba ningepata utajiri kupitia yeye, nilipomwangalia, bado nilikuwa na maswali mengi ambayo yote hayo hayakuwa na majibu yoyote yale.

Huyo mzee akaniambia niende naye pembeni kwani suala ambalo nililitaka halikuwa la kulizungumzia juujuu, ilitakiwa tutulie sehemu na aniambie kila kitu, nikakubaliana naye hivyo Dickson kutulia pembeni akitusubiri.

“Kweli unataka kuwa tajiri?” lilikuwa swali lake la kwanza kuniuliza.

“Ndiyo!” nilimjibu huku nikionekana kumaanisha nilichomwambia.

“Kweli?” aliniuliza.

“Ndiyo!”
“Sidhani kama unataka utajiri…” aliniambia.

“Kweli tena, nataka kuwa tajiri…” nilimwambia kwa sauti yenye msisitizo kabisa.

“Zakia, huna moyo, huna moyo, unaonekana tu…”

“Moyo ninao, nipo tayari kwa lolote lile.”

Niliposema hivyo, yule mzee akaanza kucheka sana, sikujua alikuwa akicheka nini, sijui kama alifurahishwa na jibu langu au la. Nilibaki nikimwangalia kwa mshangao, yeye mwenye aligundua kwamba nilikuwa nikijiuliza mengi kuhusu kicheko kile.

“Eti una moyo! Moyo gani na wakati unaogopa hata mende?” aliniuliza.

“Siogopi mende…nimetoka Morogoro mpaka hapa kwa ajili ya kutafuta utajiri tu, jua kwamba nina kiu ya kuwa tajiri, nipo tayari kufanya lolote ili nipate huo utajiri,” nilimwambia.

“Hata kuua?” aliniuliza.

“Sidhani, ila nikiambiwa kwamba nikimuua huyu napata utajiri, nitaua tu, sitokuwa na budi,” nilimwambia.

Nilichokuwa nikikiongea, nilimaanisha kutoka moyoni mwangu, kwa wakati huo nilikuwa tayari kwa lolote lile, kiu kubwa ya kuwa tajiri ilikuwa imenikamata. Mzee Hassani akaniambia kwamba jioni ya siku hiyo angenifuata hivyo nijiandae kwani kuna sehemu nilitakiwa kwenda naye, hilo halikuwa tatizo, nikakubaliana naye, akazungumza kidogo na Dickson kisha kuondoka, ndiyo kwanza muda huo ilikuwa saa saba mchana.

Aliniacha na mawazo tele, kichwa changu kilivurugika kabisa, wakati mwingine nilikuwa namuamini huyo mzee kwamba angenifanya kuwa tajiri mkubwa lakini wakati mwingine nilikuwa na wasiwasi kwamba asingeweza kufanya hivyo.

Kama kweli yeye alikuwa akitoa utajiri, kwa nini yeye mwenyewe hakuwa tajiri? Kama alikuwa akitoa utajiri, kwa nini Dickson hakuwa tajiri na wakati alikuwa rafiki wake wa karibu? Kila nilichojiuliza, nikawa na uhakika kwamba inawezekana mzee huyo alikuwa muongo.

“Dickson…unamuamini kweli huyu mzee?” nilimuuliza Dickson.

“Ndiyo!”

“Kweli atanisaidia?”

“Sana tu…kuna marafiki zangu kama watano, kawasaidia na sasa hivi ni matajiri wakubwa hapa mjini,” aliniambia.

“Sasa kama yeye anatoa utajiri, kwa nini na wewe asikupe? Au hutaji kuwa tajiri?” nilimtupia swali.

“Nataka!”

“Sasa kwa nini hujamwambia akupe?”

“Basi tu, nataka utajiri ule wa kuutafuta kwa nguvu zangu ili baadaye niwe na ushuhuda jinsi nilivyosota,” aliniambia huku macho yake yakionekana kuwa na jambo lililojificha.

Sikutaka kujali sana, nilichokuwa nikikiangalia ni maisha yangu tu kwani kwenye ridhiki za kuwa na maisha mazuri, Mungu aliwapa wale waliokuwa na kiu kubwa kama niliyokuwa nayo kipindi hicho.

Basi baada ya saa kadhaa, mzee Hassani akarudi mahali hapo na kukutana naye. Akanichukua na kuanza kuondoka naye mahali hapo. Kumbuka kwamba kwa kipindi chote tangu nifike Dar es Salaam sikuwa nimetoka ndani ya kituo kile, hivyo kutoka humo ndipo nikaanza kuona mazingira halisi ya jiji hilo.

Lilikuwa zuri, lililopendeza machoni mwangu.

Mzee Hassani alifika na gari lake na kulipaki nje. Tulipotoka, tukapanda na kisha kuondoka, tulipoelekea kwa kipindi hicho sikuwa nikipafahamu ila kwa sasa, ninapajua mno, palikuwa ni Bunju.

Njiani tulikuwa tukizungumza mambo mengi, katika kila sentensi aliyoongea ilionyesha alikuwa miongoni mwa watu waliojiamini kwa kila walichokuwa wakikifanya. Sikutakiwa kuwa na hofu hata kidogo.

Tulikwenda mpaka tulipofika sehemu iliyokuwa imeunganishwa na barabara moja ya vumbi, tukaingia nayo, tulikwenda zaidi mpaka tukaanza kuingia sehemu iliyokuwa na miti mingi.

Sikuwa na uhakika kama huko kulikuwa na watu walikuwa wakiishi, kulikuwa kimya sana, hatukusimama, tuliendelea kuifuata barabara hiyo ya vumbi mpaka kufika sehemu ambayo barabara ilifika mwisho, sasa tukaanza kuelekea katika njia ambayo hakukuwa na njia rasmi, nikaanza kushikwa na hofu, nikahisi kuna hatari mbele yangu! Mzee Hassani hakutaka kuzungumza tena, naye alikuwa kimya, macho yake yalikuwa mbele, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, ila kwangu, nilitamani nirudi. Eti huko ndipo kulipokuwa na utajiri! Nikasubiri nione nini kingetokea.

****

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kesho hapa kujua kitakachoendelea katika sehemu ya TISA.

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

halotel-strip-1

Comments are closed.