The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike – 9

maiti-cover

ILIPOISHIA SEHEMU YA NANE

Tulikwenda mpaka tulipofika sehemu iliyokuwa imeunganishwa na barabara moja ya vumbi, tukaingia nayo, tulikwenda zaidi mpaka tukaanza kuingia sehemu iliyokuwa na miti mingi.

Sikuwa na uhakika kama huko kulikuwa na watu walikuwa wakiishi, kulikuwa kimya sana, hatukusimama, tuliendelea kuifuata barabara hiyo ya vumbi mpaka kufika sehemu ambayo barabara ilifika mwisho, sasa tukaanza kuelekea katika njia ambayo hakukuwa na njia rasmi, nikaanza kushikwa na hofu, nikahisi kuna hatari mbele yangu! Mzee Hassani hakutaka kuzungumza tena, naye alikuwa kimya, macho yake yalikuwa mbele, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo, ila kwangu, nilitamani nirudi. Eti huko ndipo kulipokuwa na utajiri! Nikasubiri nione nini kingetokea.

MWAGIKA NAYO HAPA…

Tuliendelea na safari mpaka tulipofika sehemu fulani ambayo ilikuwa na miti mingi na kwa mbali kulikuwa na nyumba ndogo ya udongo. Nilibaki na mshangao, sikuamini sehemu kama hiyo kungekuwa na mtu anaishi, niliogopa, wakati mwingine nilihisi kama nilikuwa kwenye sehemu mbaya, yenye kutisha ambayo ingenifanya nitekwe na watu wenye roho mbaya.

“Ila si natafuta utajiri, haina jinsi..” nilijisemea.

Mzee Mudi akaniambia niteremke na tuanze kwenda kule kwenye kile kijumba, wakati natembea, mwili wangu ulikuwa unatetemeka mno na wakati mwingine nilihisi ningeweza hata kuanguka.

“Mbona unatetemeka?” aliniuliza.

“Hakuna kitu.”

“Kweli?”

“Ndiyo!”

Japokuwa nilimficha lakini nilikuwa na uhakika kwamba alinigundua. Tuliendelea kusogea mbele mpaka tulipokifikia kijumba kile ambapo akaniambia kwamba hatukutakiwa kuingia moja kwa moja bali tulitakiwa kusubiri nje, tukafanya hivyo.

Baada ya dakika kama mbili, tukasikia sauti ndani ikitukaribisha, tukasimama na kuanza kuingia ndani. Huko, tulimkuta mzee mmoja, kwa kumwangalia harakaharaka, alikuwa na miaka kama sabini ila alikuwa amechoka sana kimaisha.

Kichwa changu kikaanza kujiuliza, je, mzee yule angeweza kunifanya niwe tajiri kama nilivyotaka? Wakati najiuliza hayo, nikashangaa mzee yule akisimama na kunishika kichwa changu.

“Usijiulize swali hilo, nitakufanya kuwa tajiri mkubwa sana,” aliniambia huku akiwa amenikazia macho.

Kwanza nikashtuka, ilikuwaje ajue kile nilichokuwa nikijiuliza, mpaka hapo, nikajua kwamba huyo mzee alikuwa na nguvu za ziada. Nikatulia na kumwangalia usoni. Kwa jinsi chumba kile kilivyokuwa, kiliniogopesha mno, kulikuwa na tunguli kila kona, harufu mbaya ambayo ilinifanya kutamani kuziba pua zangu.

“Unataka kuwa tajiri?” aliniuliza mzee huyo.

“Ndiyo!”

“Una uhakika?” aliniuliza.

“Ndiyo mzee!”

“Utayaweza masharti?” aliniuliza.

“Nitayaweza tu..”

Mzee yule akasimama na kuanza kuimba nyimbo ambazo sikuwa nikizielewa kabisa. Hakuishia kuimba tu bali akaanza kucheza pia. Nilibaki nikimwangalia, sikutaka kuzungumza kitu chochote kile kwani hata nguvu ya kufanya hivyo sikuwa nayo.

Akanisogelea na kunipaka unga fulani machoni mwangu. Ulikuwa na rangi nyeusi, alipoyapaka macho yangu, nikaanza kuhisi hali ya tofauti moyoni mwangu, furaha kubwa ambayo sikuwahi kuipata maisha yangu yote.

“Unajisikiaje?” aliniuliza.

“Najisikia vizuri….”

“Unahitaji utajiri wa aina gani? Wa kuku na mahindi au wa milele?” aliniuliza swali ambalo sikuwa nikilijua kabisa.

“Sijajua upo vipi!”

Mzee Mudi ndiye akachukua nafasi hiyo na kuanza kuniambia tofauti ya utajiri hiyo aliyoniambia mzee huyo. Utajiri wa kuku ulikuwa ni kwamba kuku anatupiwa mahindi chini, anaanza kula, kama akila mahindi matano, basi utajiri wako utakuwa ni wa miaka mitano, kama akila mahindi ishirini, basi utajiri wako utakuwa wa miaka ishirini, baada ya hapo unafilisika na kufa.

“Hapana huo siupendi!” nilimwambia mzee Mudi.

“Kwa nini? Huo ndiyo mzuri!”

“Mimi nautaka huo mwingine.”

“Unaujua upo vipi?”

“Sijui, ila nautaka huohuo!” nilimwambia.

Utajiri niliosema kwamba niliutaka ulikuwa ni wa masharti makubwa. Niliambiwa hilo lakini nikasema kwamba nautaka huohuo na kama ni masharti nitayafanya yote lakini si kukubali ule wa mwanzo wa kuwa tajiri kwa kipindi fulani kisha kufa.

“Huu una masharti makubwa mawili,” aliniambia mganga.

“Yapi?”

“Moja, unatakiwa kuwaua wazazi wako wote wawili,” aliniambia huku akikishika kitunguli kidogo kilichokuwa pembeni yake.

“Kuwaua wazazi wangu?”

“Ndiyo!”

“Na sharti jingine?” niliuliza huku nikionekana kuchanganyikiwa.”

“Kufanya mapenzi na maiti ishirini..” aliniambia.

****

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kesho hapa kujua kitakachoendelea katika sehemu ya 10

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

halotel-strip-1

Comments are closed.