Nilimpa kilema mtoto wa tajiri!-2

Ilipoishia wiki iliyopita

“Baada ya kutua mizigo, moja kwa moja mama alianza kumsimulia baba juu ya yule mwanamke. Kama kuna siku niliwahi kuwa na furaha, basi ni siku hiyo nilipomsikia baba akikubali, lakini akitoa maelekezo kuwa ni lazima wapafahamu nyumbani kwa huyo mama ili wajue ni wapi mtoto wao alikuwa akikaa.”

Sasa endelea…

Binti huyo alidai kuwa kesho yake waliondoka tena na mama yake hadi sehemu ileile waliyokutana na yule mama na alikuja hapo majira ya mchana. Mama yake akamwelezea kuwa mumewe alikuwa amekubali aende akaishi na binti yao, lakini akamweleza kuwa ametoa sharti la wao kupafahamu anapoishi.

“Lile halikuwa tatizo kwa yule mama, kwani alituambia tupande kwenye gari lake, akaendesha kuelekea Kariakoo, tukapitia Ilala na kutokezea Magomeni. Hatimaye tukafika eneo alilotuambia linaitwa Sinza Madukani, kwenye nyumba moja iliyokuwa ndani ndani, tukaingia.

“Lazima nikiri kuwa kwangu, ilikuwa ndiyo nyumba nzuri zaidi niliyowahi kuingia kabla ya siku hiyo, kwani ilikuwa na sebule kubwa, yenye masofa ya bei mbaya na televisheni kubwa. Kulikuwa na zulia zuri ambalo lilinifanya nishindwe kujua kama pale sebuleni paliwekwa marumaru au simenti ya kawaida.

“Alitukaribisha vizuri, tukanunuliwa soda na mazungumzo yakaanza. Yule mama alimuomba mama asubiri hadi watoto wake watakapofika, maana mmoja alikuwa shuleni, na mwingine mdogo, alisema huwa anamuacha kwa mdogo wake anayeishi jirani na hapo. Akampigia simu na baada ya muda mchache, huyo mtoto akaletwa.

“Kalikuwa ni katoto kazuri kweli ka kike na saa saba na nusu, tukasikia mlio wa gari nje ya nyumba, akasema alikuwa ni kijana wake mkubwa ndiyo alikuwa anarejeshwa nyumbani. Akaingia kijana mmoja aliyekuwa na umri wa kama miaka minne na nusu au mitano, aliyedai alikuwa anasoma nasari.

“Akatutambulisha, akasema yule mkubwa anaitwa Toma na mdogo Enidi nao akawaambia kuwa mimi ni dada yao na mama aliwaambia ni mama yao mkubwa, yaani dada yake yeye. Basi tukakaa nao kwa furaha hadi raha. Saa kumi kumi hivi mama aliaga ili aanze kurudi, akapewa shilingi elfu arobaini ambazo aliambiwa ndiyo mshahara wangu.

“Mama alifurahi sana, akatoa elfu kumi na kunipa, lakini yule mama akakataa, akasema endapo nitakuwa na mahitaji yoyote ya fedha, atanihudumia kama mtoto wake, hivyo mama asijali. Akamshukuru na tukamsindikiza stendi ya daladala ambako alipanda basi na kuondoka zake.

“Nikarejea nyumbani na kuanza maisha mapya. Nilifurahi sana kwa kweli maisha ya pale, chakula kilikuwa kizuri, nyumba nzuri na kazi hazikuwa ngumu tofauti na nilivyotegemea. Maana nilikuwa tu nafua nguo za watoto, zake alizifua mwenyewe kila Jumapili alipokuwa hatoki nyumbani.

“Baadaye nikagundua kuwa yule mama hakuwa na mume, kwani watoto wake wawili kila mmoja alikuwa na baba yake na ilivyoonekana, ndiyo waliokuwa wakiwasomesha watoto wao, maana mara kwa mara niliona akizungumza nao kwa simu na kuwaambia mahitaji yao.

“Na kingine, ilionekana yule mama alikuwa anafanya kazi usiku, maana karibu kila siku kasoro Jumapili, alikuwa akitoka kuanzia saa mbili hivi na alirejea alfajiri. Hakuwa akitoka na gari wakati akienda kazini.

“Baada ya miezi mitatu ya kuishi naye vizuri, nikiwa sijarudi nyumbani Mbagala hata mara moja, nikaanza kuona mabadiliko ya tabia yake, kwani alianza kuwa ananifokea hata kwa kosa dogo, kitu kilichonishangaza sana. Siku za kwanza kufokewa, nakumbuka nilikuwa nalia sana.

“Baadaye licha ya kunifokea, akawa pia ananitukana na kunisimanga. Maneno hayo yalikuwa yananiuma sana, hasa kutokana na ukweli kwamba maisha ya nyumbani kwetu yalianza kupata uhai baada ya mimi kupata hiyo kazi, maana mama sasa alifungua biashara ya mama ntilie na baba naye akawa muuza genge.

“Walinihimiza sana kutofanya mchezo na kibarua changu, walinitaka kuwa mvumilivu na mwenye nidhamu. Kila nilipowaambia kuhusu manyanyaso yanayoanza, waliniambia ni mambo ya kawaida na yataisha, kwani kama yule mama angekuwa na tabia hiyo angeionyesha tokea mwanzoni.

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS UPATE HABARI KEMKEM ZA UCHAGUZI MKUU

globalbreakingnews.JPG
Toa comment