The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo

0

ILIPOISHIA:

“Kwani unaniona nafanya nini?” Rose alimjibu kwa mkato huku akimtengeneza mtoto aliyekuwa mgongoni.

SASA ENDELEA…

“Na…na…na huyu si…si…si shoga yako nani kweli?”

“Eflazia,” nilimjibu nikiwa nambembeleza mwanangu aliyekuwa anataka kulala.

“Jamani hii si kawaida kuna kitu, watoto wazuri kama ninyi kuja kwa kibabu hiki si bure lazima kuna kitu,” mama Sabuni alilalamika kwa sauti ya huzuni nilimsikia lakini sikumuelewa.

“Bibi eeh fuata kilichokuleta ya huku mengine  hayakuhusu,” Rose alikuwa mkali baada ya kuona kama tunaingiliwa maisha yetu.

Kwa vile mama Sabuni alimleta mtu, alionana na mzee Sionjwi kisha alirudi mjini akiwa na kitu moyoni mwake. Hakukubali kuliacha lipite, alikwenda hadi ofisini kuulizia tunapoishi. Kwanza walishangaa kusikia mimi nipo japo kuna watu waliamini nilikwenda kusoma lakini sikurudi kazini na Rose aliacha kazi kwa hiyari yake.

Alipoelekezwa alikwenda kwenye familia zetu na kuwaeleza habari zetu walizoziona mpya masikio mwao baada ya kutoweka kwetu ghafla. Baada ya kutoweka akili zao zilipumbazwa na dawa za babu hakuna hata mmoja aliyetukumbuka.

Baada ya sisi kutoweka wengi hawakutuwaza na kuona jambo la kawaida na kulipuuzia na kuendelea na mambo yao mengine. Baada ya kupewa taarifa mama Sabuni aliongozana na familia zetu pamoja na polisi mpaka kijijini ambako tulichukuliwa mpaka kituo cha polisi.

Ilikuwa kama wana kijiji kwa jinsi tulivyokuwa watoto wetu walikuwa jumla ishirini na tano, wake tuliowakuta wote walikuwa na watoto kumi na nne na mimi na Rose tulikuwa na watoto kumi na moja. Wote jumla tulikuwa thelathini pamoja na mume wetu.

Babu mzee Sionjwi ambaye alikuwa mume wetu wakati huo alikuwa amechoka kwa umri alifunguliwa mashtaka ya kututorosha. Lakini sisi wote wake zake watano tulipinga kuwa hatukutoroshwa bali tulikwenda kwa hiyari yetu kwa vile tulikuwa tumevuka umri wa miaka kumi na nane tulikuwa na maamuzi yetu.

Maelezo yetu yalifanya babu kuachiwa kwa vile hakukuwa na ushahidi wa kututorosha watu wazima kama sisi. Wakati huo ilikuwa imepita miaka tisa na nusu nikiwa na watoto sita ambapo uzao wa kwanza mapacha wawili, wa pili mtoto mmoja, wa tatu mapacha wawili wa nne mtoto ambaye alifariki akiwa na umri wa miezi minne na wa mwisho mtoto mmoja.

Mapacha wa kwanza muda huo walikuwa na umri wa miaka minane aliyewafuata  alikuwa na miaka sita, mapacha wengine walikuwa na miaka mitano na wa mwisho mwaka mmoja na nusu ambaye walinikutana nambebembeleza.

Familia zetu zilipotuchukua kwa nguvu lakini wote tulitoroka na kurudi kwa mume wetu. Ilibidi nao wahangaike kwa waganga baada ya kuonekana tulichezewa mchezo na babu wa kupumbazwa akili kutufanya tumuwaze yeye tu muda wote.

Kitendo cha babu kukamatwa na misukosuko ya polisi kisha kuswekwa ndani kwa siku mbili, kilifanya apate mshtuko hata alipoachiwa huru hali yake haikuwa nzuri kwa presha kuwa juu sana.

Kutokana na kupatwa shinikizo la damu ilibidi akimbizwe hospitali ambako alikaa siku mbili na kufariki dunia. Kifo cha babu kilituchanganya sana wake zake, tulichanganyikiwa tulijiuliza duniani bila babu tutaishije kwani tuliamini yeye ni kila kitu kwetu chini ya jua.

Lakini kila jambo lilikuwa na makusudio yake baada ya mazishi, familia zetu zilipata urahisi kutuchukua japokuwa wake wenzatu mwanzo hawakujulikana wanatoka wapi kwa vile kila mke wa babu hakuwahi kutembelewa na ndugu yake.

Baada ya kutolewa kijijini tulipelekwa kwa mtaalamu ambaye aliweza kutuzindua na kuzirejesha akili zetu za kawaida. Kila mmoja akukubaliana na hali aliyojikuta nayo. Tulikuwa watu tulioishi kama misukule tusiojielewa baada ya kutekwa akili na babu.

Sikuamini kujikuta nikiwa nimechoka huku nikiwa na watoto sita mwenye afya dhaifu na shoga yangu Rose akiwa na watoto watano kwa kuzaa mara tano. Kiafya nilionekana kama mwanamke wa miaka sitini wakati nilikuwa nina miaka 37 na Rose 39, hata wake wenzatu nao pia walikuwa wamechoka kwa maisha ya kijijini.

Baada ya kuzinduliwa na akili yangu ya kawaida kukaa sawa, kila mmoja alikumbuka alipotoka na kwa msaada wa polisi tulifikishwa makwetu. Niliporudisha kumbukumbu zangu nilikumbuka muda ule nilitakiwa niwe wapi na pale nipo wapi. Kwa kweli nililia sana badala ya kwenda kusoma Ulaya nilikwenda kuolewa na mganga wa jadi huku elimu yangu ikipotea bure kwa tamaa ya cheo.

Katika miaka tisa ambayo niliondoka nyumbani nilishukuru Mungu familia yangu niliikuta ipo katika hali nzuri japokuwa nilikuwa nimempoteza baba yangu kipenzi miaka mitatu iliyopita. Nyumba yangu aliyokuwa akiisimamia mama ilikuwa imeisha wakati huo ilikuwa  imepangishwa kwa kampuni moja ya nje.

Kwa kweli kila nilivyofikiria dhamira yangu na sehemu niliyoangukia nilikuwa nikilia huku nikiwaangalia watoto wangu wadogo wasio na baba tena wenye afya dhaifu.

Je, kiliendelea nini? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave A Reply