The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo – 42

0

ILIPIUSHIA:
“Hongera, mi mbona nilijua kila kitu mapema sema wasiwasi wako tu.”
“Dah! Sasa itakuwaje?” ilibidi nimuulize kabla hatujafika kwa wakeze.
“Kuhusu nini?”

“Safari ya mjini maana nina muda wa siku mbili tu kabla ya kuondoka.”
“Wewe tu.”
“Kwa hiyo babu tunaondoka?”
“Kila nilichokuahidi ndivyo kitakavyokuwa.”
“Waooo.”
SASA ENDELEA…

“Si tunaondoka jioni ya leo?”
“Ndiyo babu.”
Tulirudi hadi nyumbani nikiwa nimebeba kikapu cha dawa na kumfanya Rose atanie:
“Umependeza sana kama mke na mume, babu mjukuu anafaa kuwa mke wa tano.”
“Ati eeh,” Babu aliitikia kwa utani.

“Sasa, yaani kwa jinsi alivyo akija hapa wewe ndiye utakuwa mke mkubwa.”
“Rose, wake wanne wanamtosha babu,” nilisema huku nikimuacha akipokewa na watoto wake.

Kwa vile nilikuwa mwenyeji nilikipeleka kikapu cha dawa sehemu anayoweka dawa. Baada ya kuweka dawa sehemu yake nilikwenda kwenye gari kushusha mizigo. Kwa vile nilijua hatutaonana kwa muda mrefu nilikuwa nimewanunulia vitu vingi.

Baada ya zoezi lile nilipata muda wa kuzungumza na babu kwa kituo kumpa taarifa ya kufanikiwa mpango alioutengeneza ambao kila hatua uliyabadili maisha yangu. Kabla ya mazungumzo nilimpatia bahasha iliyokuwa na kiasi cha pesa shilingi milioni moja.
“Babu zawadi yako.”

“Nini tena mjukuu? Leo naona mzigo kwenye bahasha.”
“Pesa babu.”
“Kiasi gani?”
“Milioni moja.”

“Acha utani?” Babu hakuamini.
“Kazi uliyofanya ni kubwa sana hata hicho kiasi kwangu nakiona kidogo niombee kwa Mungu niende salama nirudi salama ili ule matunda ya kazi yako.”
“Usiwe na wasi kila kitu naamini kitakwenda kama kilivyopangwa, acha cheo utakachokipata, nakuhakikishia hata ukiutaka ukurugenzi utaupata.”

“Usiniambie?” nilishtuka kusikia maneno yale japokuwa hayakuwa mageni mdomoni mwa babu, lakini muujiza alionifanyia kubadili matokeo nilimuamini kwa asilimia mia moja.

Jamani tamaa mbaya nilijikuta nikiutamani na ukurugenzi, lakini niliamini ule haukuwa muda muafaka. Kwa vile nilikuwa nakwenda kusoma na kuongeza elimu na cheo sikuona sababu ya kuutaka ukurugenzi kwa muda ule.
“Mjukuu kila kitu kwangu kinawezekana.”
‘Basi babu nikirudi tu tunaanza zoezi hilo.”

“Wewe tu mjukuu wangu, nyota yako inang’aa hainisumbui kukutengenezea mambo yako.”
“Sawa, babu basi jiandae tuondoke zetu.”

“Mjukuu kuna dawa nitakutengenezea pia kuna kihirizi cha kukuongezea mvuto na bahati pia nitakupa dawa ya kuoga na kujifukiza.”

“Ha! Babu nitawezaje kujifukiza wakati huko hakuna moto wa mkaa?”
“Chumba utakachokuwamo nitaipaka dawa ambayo itachanganywa na mafuta mazito kwenye mshumaa na kuuwasha usiuzime mpaka uishe.”
“Hapo sawa.”

“Basi ngoja nikuandalie sawa, nataka ukirudi usichukue hata miezi sita uwe mkurugenzi.”
“Babuu, sijui nitakupa zawadi gani?”
“Labda unizalie mtoto.”

“Babu watoto unao wengi.”
“Mbona ninao wachache baba yangu alikuwa na watoto ishirini na tano nataka mmoja toka kwako.”

“Basi yote hayo tutapanga nikirudi.”
“Hakuna tatizo mjukuu.”
Babu alinyanyuka na kuelekea kuandaa dawa zangu, nilibakia nikimtazama bila kummaliza kwani kwa umri wake hakutakiwa kuongeza watoto. Nilijua nikirudi hatakumbuka suala la kuzaa na mimi tena japo raha zake sikutaka kuzipa kisogo.

Nilijumuika na wakeze kwa mazungumzo huku nikiwaaga safari yangu ya kwenda nje ya nchi kimasomo. Kila mmoja aliniombea kwa Mungu niende salama na nirudi salama. Niliwashukuru kwa dua zao na kuwaahidi kuwafanyia mambo mazuri pindi nikirudi.

Pia nilitumia muda ule kuzungumza mengi na shoga yangu Rose huku nikimsihi asibebe mimba ovyo kwa vile maisha ya kule kijijini si mazuri. Aliniahidi kuwa makini kuhakikisha kuchukua muda mrefu kupata mtoto wa pili.

Kutokana na ukaribu wetu nilimpatia vitu vingi kwa ajili ya mtoto wake atakayezaliwa na baadhi ya pesa za matumizi yake binafsi. Shoga naye aliniombea kwa Mungu safari yangu iwe ya heri na baraka, tulizungumza mengi kwa muda ule nikimsubiri babu Sionjwi.

Tukiwa katikati ya mazungumzo babu aliwaita wake zake wote, nilibaki na watoto waliokuwa wakicheza. Baada ya muda walirudi, nilimdodosa shoga yangu Rose waliitiwa nini na babu!

“Vipi mbona mmeitwa wote?”
“Mmh! Tuliitwa kuagwa kuwa mnaondoka wote kwenda mjini kuna kazi anatakiwa kukufanyia siku mbili kabla ya wewe kuondoka.”
“Ni kweli, kwa vile kazi yangu ilikuwa ina vikwazo vingi ameona kabla ya kuondoka basi afanye mambo yake.”

“Hakuna tatizo, ungekuwa hujaniletea mambo yangu ningekuagiza kwa vile kila kitu umeniletea ukiondoka usafiri salama.”
“Asante shoga, nina imani kwa uwezo wa Mungu kila kitu kitakwenda alivyopanga niende salama nirudi salama ili tuonane.”
“Mjukuu nipo tayari,” ilikuwa kauli ya babu.

Nilipogeuka kumwangalia huku pua yangu ikilakiwa na manukato ya bei mbaya, sikuamini kumuona babu akiwa katika suti ya bei mbaya. Nilibakia mdomo wazi. Babu alikuwa amebadilika hakuwa yule mzee wa kijijini mwenye mavazi yasiyo na hadhi.
Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wake katika Gazeti la Risasi Jumatano.

Leave A Reply