Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-21

ILIPOISHIA:

Lakini nilipiga moyo konde na kuendelea na kazi kama kawaida, usiku nilijikuta nina hamu ya kuota ndoto za kufanya mapenzi na mzee Sionjwi lakini wapi mpaka kunakucha sikumuota mzee Sionjwi wala kivuli chake.

Kitu kingine kilichonishtua ni kupotea kwa Rose ambaye walisema aliaga anakwenda kwa rafiki yake lakini hakurudi, wapo waliosema Rose mtu mzima hawezi kupotea huenda amekwenda kwa mwanaume.

SASA ENDELEA…

Kwa upande wangu nilimlaumu Rose kuacha kazi kwa ajili ya mwanaume kibaya hata kwao hakufahamika. Niliona heri bwana aliyemuoa kuliko kujikurupukia leo na kesho anakuacha njia panda unakosa pa kushika.

****

Ilikuwa wiki mwezi Rose haonekani kwa kweli niliingiwa ukiwa kutoweka kwa shoga yangu Rose ambaye ndiye aliyekuwa mtu wangu wa karibu kuliko wote pale kazini. Kwa ukaribu wangu nilimgeuza kama ndugu yangu wa damu, kwa kweli nilipooza sana pale kazini kwani sikuwa na mtu wa kumpa siri zangu.

Kila kitu kina mwisho hata maumivu yana mwisho huwezi kuteseka milele, nilijikuta hali ya upweke naizoea hata kufikia hatua ya kumsahau shoga yangu Rose.

Siku zilikatika huku kazi nayo ikienda vizuri mshahara nao uliongezeka na marupurupu juu, baada ya miezi sita tangu Rose apotee nilipata tetesi kuwa kuna nafasi ya kwenda kusoma nje na ukirudi unakuwa mhasibu mkuu wa kampuni kwa kanda zote mahesabu yote yanapitia kwangu.

Nafasi ile ilitolewa baada ya aliyekuwa mhasibu mkuu wa kanda kukaribia kustaafu. Japo ilionekana kama mimi nina nafasi kubwa ya kwenda lakini kulikuwa na kaka mmoja aliyetoka chuoni ambaye ilionesha wazi huenda angeichukua nafasi ile.

Wazo la haraka lilikuwa kukimbilia kwa mzee Sionjwi sikuogopa kuniingilia kimwili kwangu hakikuwa kitu cha kunitisha sana. Cha muhimu kilikuwa kuipata nafasi ile kwa gharama yeyote.

Siku ya Alhamisi niliaga kazini kuwa Ijumaa nitakuwa na udhuru, nilikubaliwa kwa vile nafasi ile nilimuachia yule kaka ambaye alikuwa ndo ameanza kazi, mambo mengi nilimsaidia alionekana ni mstaarabu tena mwenye heshima kitu kilichonifanya nimpende.

Siku ya Ijumaa asubuhi nilifunga safari mpaka kijijini kwa mzee Sionjwi, nilifika mapema sana, mpaka saa mbili na nusu nilikuwa nimesimamisha gari mbele ya nyumba ya mzee Sionjwi. Kama ilivyo kawaida yangu niliwanunulia mahitaji muhimu kwa maeneo yale. Sukari, chumvi, mchele sabuni na mafuta.

Nilipokelewa kama Malkia kila mtu alinifurahia mimi, nilipokuwa nateremka kwenye gari macho yangu yaliona kitu ambacho kwa kweli kilinishitua sana. Sikuamini macho yangu mara moja kuwa ninachokiona ndicho chenyewe. Sikuamini niliacha gari bila kufunga na kusogea karibu ili nipate uhakika ni kweli au naota au nafananisha.

“Efrazia unashangaa nini, karibu shoga.”

“Mmm! Siamini ni wewe Rose?”

“Ndiyo mimi shoga nimejaa tele kama pishi la mchele.”

Mmh, ukishangaa ya Musa utayaona ya Firauni, Rose alikuwa amejifunga shuka nyeupe iliyoishia juu ya matiti mgongo ulikuwa nje, chini alikuwa amevaa ndala za matairi mkono wa kushoto alikuwa amejifunga hirizi ndogo nyeusi. Yote tisa kumi alikuwa na ujauzito mkubwa tumbo lilimwelemea, nilibakia mdomo wazi.

“Efrazia, unashangaa nini mpenzi?” aliniuliza akiwa anatafuna embe bichi.

“Rose lini tena huku?”

“Tangu nilipopotea kazini,” alinijibu bila wasiwasi.

“Na ujauzito huu wa nani?”

“Ukiona ujauzito ujue una baba yake, mbona maswali kama umesikia nimepewa na bwana wako?”

“Rose siamini”

“Usiamini nini au ulisikia mimi mgumba?”

“Siyo hivyo kukukuta huku.”

“Rose, usitake kuyajua ya watu, fuata yaliyokuleta ya kwako si uliitoa tuache tuzae.”

“Unataka kuniambia ujauzito huu ni wa mzee Sionjwi?”

“Kwani mwanamke yule?”

“Sina maana hiyo najua ni mwanaume tena shababi lakini bado hujaniweka wazi ujauzito huu ni wake?”

“Eeh.”

“Mmh.”

“Unaguna nini?”

“Aah, basi.”

“Basi karibu mi ndo mwenyeji wako.”

Nilipewa mkeka wakati huo chai na viazi ilikuwa tayari na imetengwa kwenye mkeka wake wote wanne wa mzee Sionjwi walijumuika akiwemo shoga yangu kipenzi Rose. Sikutaka kukataa chai ile tulijumuika wote na kuinywa chai ile.

Baada ya chai nilikaa chini ya mti wakati huo mzee Sionjwi hakuwepo alikuwa amedamka alfajiri kwenda kuchimba dawa, nilikaa na Rose hata kumuuliza maswali niliogopa kutokana na majibu yake. Nilitulia kwenye mkeka nikiwa na mawazo mengi kichwani nikijiuliza nini kilichomfanya Rose kuacha kazi na kuja kwa mzee Sionjwi na kuolewa na kuwa mke wa nne.

Kwa kweli jibu lilikuwa gumu kupatikana na kuuliza niliogopa kuudhiana na shoga yangu, niliamua kukaa kimya mpaka nitakapoondoka na hata mjini sitamwambia mtu niliyoyaona kwa mzee Sionjwi hata wazazi na ndugu wa Rose niliapa sitawaambia kitu chochote kuhusiana na Rose niliogopa kumuudhi mzee Sionjwi na kukosa tiba ya matatizo yangu.

Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma kwenye toleo lijalo.     


Loading...

Toa comment