Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-24

ILIPOISHIA:

Niliagana nikiwa na furaha ya ajabu, kutokana na furaha niliyokuwa nayo nilimpa babu Sionjwi laki tatu. Nilimuaga Rose ambaye aliniuliza narudi lini, nilimjulisha alinituma baadhi ya vitu alivyokuwa akivitaka. Muda ulikuwa umekwenda ilikuwa inakaribia saa mbili usiku niliingia kwenye gari langu na kurudi mjini nikiwa na furaha ya ajabu kama nafasi tayari nimeipata.

SASA ENDELEA…

 Njiani nilikuwa nikiwaza mengi bila kupata jibu la Rose kwenda kijijini kwa mzee Sionjwi na kuacha kazi, sikuona cha maana alichokifuata kule zaidi ya tabu ya maisha kuzaa watoto wasio na malezi bora bila kuwa na uhakika wa maisha ya mbeleni.

Kila nilipoangalia maisha ya mzee Sionjwi na wakeze ya kubahatisha na shoga yangu Rose naye kwenda kulekule. Sikuamini kabisa kama kwenda kwa mzee Sionjwi haikuwa akili yake bali ya kiganga.

Nilivyojiangalia mimi na Rose nilikuwa namzidi kwa kiasi kikubwa kwa uzuri, nilijikuta nikiwa na wasiwasi kama ameweza kumshika akili shoga yangu niliamini kwa tamaa yake angeweza kunishika akili na mimi na kuingia kijijini na kuongeza idadi ya wanawake zake.

Lakini niliyapuuza na kuamini huenda ni tamaa ya Rose kwani nilishuhudia vitendo vya ngono muda mwingi. Nilikumbuka siku ya kwanza niliwafuma wakifanya mapenzi kwenye majani, kwa hilo liliniondoa hofu kwa kuamini huenda walikubaliana wenyewe.

Hilo lilinifanya niondoe hofu moyoni mwangu, kwa kuamini mzee Sionjwi na Rose walikuwa wakijuana huenda penzi tamu la mzee Sionjwi ndilo lililomchanganya akili na kulifuata porini.

Nilifika Dar majira ya saa saba usiku, ajabu nilikuwa mtu mwenye furaha kutokana na kuhakikishiwa kuipata nafasi ile. Sikuwa na wasiwasi nilijua majina ya bodi ya kuchagua mtu atakayetakiwa kusafiri kwenda kusoma nje nitayapata kupitia shoga yangu Safia katibu muhtasi wa mkurugenzi ambaye alikuwa akinieleza kila  kilichokuwa kikiendelea kuhusu mchakato ule.

Nilipofika nyumbani nilijilaza ili kuisubiri siku ya pili kwa hamu kubwa, asubuhi ilipofika nilijiandaa kama kawaida na kuelekea ofisini. Nilifika ofisini kwa kuwahi kidogo na kuingia ofisini kwangu. Japo niliwahi ofisini lakini akili yangu ilikuwa katika kuyajua majina ya bodi ya uteuzi wa jina la mtu atakayekwenda nje kusoma.

Katika majina yote yaliyopendekezwa mimi nilikuwa nina sifa zote lakini kutokana na tabia za ndugunaizesheni niliingiwa wasiwasi wa mkuu mmoja kumteua ndugu yake. Kutokana na kuifahamu vizuri kazi ya mzee Sionjwi niliamini kabisa kazi ile haikuwa ngumu kwake hasa baada ya kumuondoa kigogo wa uchawi Mbwana.

Nilijikuta nikipingana na wazo la kumpigia simu shoga yangu Safia katibu muhtasi wa mkurugenzi ili aniambie kina nani wapo kwenye bodi ile japokuwa kulikuwa na watu niliwajua lakini ilikuwa lazima wajumbe wachache watoke kwenye matawi yetu hasa baada ya malalamiko kuonesha makao makuu hujiamulia wenyewe na viongozi wa matawi kukosa fursa ya wao nao kumpendekeza wanayemuona anafaa kwenda.

Pamoja na upinzani wa kijana aliyeonekana anatishia kazi yangu kutokana na kuwa na kivuli cha mkubwa bado niliamini uwezo wa mzee Sionjwi ulikuwa mkubwa sana mimi kuipata nafasi ile. Wakati nikiamini mbaya wangu ni yule kijana lakini nilipata taarifa nyingine kuwa kuna msichana mmoja anatoka katika moja ya tawi letu ana elimu kama yangu japokuwa mimi nilimzidi kidogo lakini alikuwa mpenzi wa meneja wa matawi ambaye ni swahiba wa mkurugenzi hivyo ushawishi wake kwenye bodi ulikuwa mkubwa ili mtu wake apite.

Wazo la kumpigia simu Safia niliona kama ni kuvujisha kile ninachokihitaji, niliamini kumuona uso kwa macho kuna nafasi kubwa ya kumshawishi mtu kwa vile uso umeumbwa na aibu.  Nilinyanyua simu kumpigia Safia kumjulia hali pia kujua ratiba zake.

Baada ya simu kuita ilipokelewa upande wa pili:

“Halo Efrazia niambie shoga, leo umeniota nini?”

“Kwa nini?”

“Naona asubuhiasubuhi.”

“Walaa, nilitaka kukujulia hali tu shoga yangu.”

“Asante sijambo sijui wewe?”

“Mi sijambo, kazi zinasemaje?”

“Ziko poa.”

“Eti kikao cha kupitisha majina kitakuwa lini?”

“Ijumaa, tena kuna ubuyu (umbea) nataka kukuambia.”

“Ubuyu! Unahusu nini?”

“Tukutane lunch nikumwagie ubuyu.”

“Poa.”

Nilijikuta nikiwa na shauku ya kujua shoga yangu Safia ana ubuyu gani ambao ameupata toka bodi ya uteuzi wa jina la mtu atakayekwenda kusoma nje ili aje ashike madaraka makubwa baada ya aliyekuwa akishika wadhifa huo kuwa katika hatua za mwisho za kustaafu.

Ilionesha kuna mizengwe mikubwa katika uteuzi tofauti na siku za nyuma.

Hata hamu ya kazi  iliniisha zaidi ya kutaka kuumung’unya niijue ladha yake kama ni chungu au tamu lakini kwa kauli ya Safia ilionesha kuna kitu hivyo ubuyu niliuona si mzuri kabisa.

Lakini kwa upande mwingine haukunitia shaka sana kwa vile niliishajua kuna ushindani na ndiyo sababu iliyonifanya niende kwa mzee Sionjwi. Pia ile ilikuwa nafasi yangu nzuri ya kujua watu watakaokuwepo kwenye bodi ya uteuzi, hivyo ilikuwa rahisi kuyajua majina ya watu hao ili niwahi kuyapeleka kwa mhusika. Baada ya kuwaza yale nilijikuta nikipata nguvu za kufanya kazi. Muda wa chakula cha mchana ulipofika   niliongozana na Safia kwa kutumia gari langu hadi kwenye hoteli iliyokuwa pembezoni kidogo na mji palipokuwa patulivu ili shoga animwagie ubuyu kwa uhuru mkubwa.

Baada ya kufika kwenye hoteli iliyokuwa na hadhi ya nyota tatu tulitafuta meza ya pembezoni na kukaa kisha tuliagiza chakula. Baada ya chakula kuletwa tulianza kula huku nikiwa na shauku ya kuujua huo ubuyu. Lakini Safia alinieleza nipunguze pupa tule kwanza baada ya chakula tulikuwa na muda wa kutosha wa mazungumzo.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia  wiki  ijayo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment