Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-24

ILIPOISHIA:

“Vipi mwenzangu kiuno kimepona au ndiyo kakizidisha?” Nilimuuliza baada ya kujifikiria kukaa huku ameuma meno.

“Dada kimepona.”

“Sasa mbona upo hivyo?”

“Dada weee kikongwe yule anapenda sifa hiyo dawa hajui kama nina tumbo hapa nipo hoi.”

“Mmmh, pole.”

“Dada usinipe pole, nipe hongera.”

SASA ENDELEA…

Hongera ya nini?”

“Tiba niliyopata si ya kitoto maumivu yote ya kiuno yamepotea.”

“Mmh, dawa yenyewe ilikuwa ya kuchua au kuchanja maana mmechukua muda mwingi?” Nilitia umbeya.

“Dada we mkubwa, ukiona ndevu ujue kuna mdomo.”

“Mmh, haya nimekuelewa.”

“Dada mzee yule kabarikiwa kanyimwa utajiri lakini nguvu za kumtoa pweza pangoni weee acha tu.”

Tukiwa katikati ya mazungumzo niliitwa kwenda kuonana na mzee Sionjwi aliyekuwa pembeni amekaa kwenye kigoda chake na pembeni kulikuwa na mkeka mdogo, muda nao ulikuwa umekwenda kiza kilianza kuingia, nilikwenda na kukaa pembeni ya mzee Sionjwi pamoja na sekeseke na Rose hakuonekana kutetereka pamoja na kudamka asubuhi na kushinda porini na kurudi muda umekwenda. Bado ameweza kugawa dozi ya kiuno kwa Rose huku akionekana bado imara kama chuma cha pua.

“Mmh, mjukuu karibu sana,” alisema kwa sauti ya chini.

“Asante babu, za siku?”

“Aah, Mungu analeta neema zake.”

“Hata mimi naona.”

Mzee Sionjwi hakusema kitu alitabasamu tu kisha alibadili mada kwani niliamini alikosa jibu hasa baada ya kumkuta shoga yangu kipenzi kwake tena kamjaza tumbo.

“Mm’hu, lete habari una jipya au ni yaleyale?”

“Kuna jipya babu.”

“Ehe, lete habari.”

Nilimweleza kisa na mkasa ulionifanya nifunge safari ya ghafla kwenda kumuona kule kijijini. Baada ya kunisikiliza alitulia kwa muda kama anasoma kitu kisha alisema kwa sauti ya chini.

“Kwa hiyo nafasi hiyo unaitaka?”

“Ndiyo maana yake babu?”

“Mbona nafasi umepata.”

“Kweli babu?”

Japo nilimwamini mzee Sionjwi niliona kama jambo lenyewe alichukulia kiwepesi sana tofauti na uzito uliokuwepo kwenye nafasi ile  baada ya mkubwa mmoja kumwandaa ndugu yake na kwa vile wao ndiyo wanaoteua mtu wa kwenda.

Pamoja na sifa zilizotajwa kuwa nazo, bado upendeleo ungechukua nafasi kubwa.

“Kwani wasiwasi wako nini?” Mzee Sionjwi aliniuliza.

“Mazingira yamejaa utata mtupu.”

“Ni wasiwasi wako tu, nafasi hiyo utaipata kinachotakiwa ni kunipa majina ya wote watakaokuwepo kwenye bodi ya uchaguzi niwakaange ili jina lako likae akilini mwao na ndilo litapita mbona kazi ya kitoto hiyo.”

“Babu unasema kweli?”

“Lipi nililokudanganya?”

“Hakuna babu.”

“Basi amini  nafasi hiyo utaipata.”

“Babu nikiipata kabla ya kuondoka nitakuletea zawadi kubwa ambayo hutaamini.”

“Kama zawadi ipo bora unipe kabisa Ulaya umekwenda mjukuu wangu.”

”Siamini,” nilijikuta nikikumbatiana na mzee Sionjwi kwa furaha.

Tulikumbatiana kwa muda huku nikihisi kitu fulani mapigo ya mzee Sionjwi yalikuwa juu kitu kilichonishtua. Baada ya kuachiana nilimsikia akihema kama mtu aliyeutua mzigo mzito.

“Vipi babu?” Nilimuuliza.

“Aah, kawaida nafasi umepata usihofu mjukuu wangu,” alisema kwa sauti ya chini.

“Kwa hiyo naweza kuondoka leo?”

“Ruksa ila hakikisha unawahi kuleta majina hayo.”

“Babu kesho jioni utaniona, nikitoka kazini breki ya kwanza hapa.”

“Basi nisikucheleweshe nikuache uwahi.”

Niliagana na babu nikiwa na furaha ya ajabu, kutokana na furaha niliyokuwa nayo nilimpa babu Sionjwi laki tatu. Nilimuaga Rose ambaye aliniuliza narudi lini, nilimjulisha alinituma baadhi ya vitu alivyokuwa akivitaka. Muda ulikuwa umekwenda ilikuwa inakaribia saa mbili usiku niliingia kwenye gari langu na kurudi mjini nikiwa na furaha ya ajabu kama nafasi tayari nimeipata.


Loading...

Toa comment