Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-29
ILIPOISHIA:
“Vipi mama, mbona kimyaa?”
“Nilipatwa na dharura, shikamoo.”
“Marahaba, sasa mbona hukunijulisha?” aliniuliza kwa sauti ya upole.
“Kwa kweli nilichanganyikiwa nilipigiwa simu na mlinzi wangu wa nyumbani kuwa kuna watu wamevunja nyumbani kwangu,” nilitengeneza uongo.
“Ooh! Pole sana basi ungetujulisha, nini kimeendelea?”
“Watu wale wamekamatwa namshukuru Mungu lakini hawakuchukua kitu.”
SASA ENDELEA…
“Ooh! Afadhali, sasa ni hivi muone msaidizi wako kuna pesa unatakiwa kuidhinisha asubuhi hii kwa ajili ya kikao.”
“Sawa mkuu.”
Baada ya kukata simu, nilishusha pumzi ndefu baada ya uongo wangu kukubaliwa. Nilinyanyua simu na kumpigia msaidizi wangu ambaye alichelewa kidogo.
“Haloo Pili, njoo mara moja na maagizo uliyopewa jana na mkurugenzi.”
“Sawa dada Eflazia nakuja.”
Baada ya muda Pili aliingia na karatasi na kuniwekea juu ya meza kisha alitoka. Nilizipitia haraka na kunionesha kunatakiwa pesa za kikao cha bodi, nilijiuliza kikao kile cha nini na mbona sikukijua mapema. Sikutaka kukihoji sana kwa vile ilikuwa hainihusu.
Baada ya kuidhinisha pesa nilimpa msaidizi wangu apeleke kwa mtoa pesa, nilimpigia simu mkurugenzi amtume mtu akachukue pesa za kikao. Alimtuma Safia aje achukue, lakini kabla hajakwenda kuchukua pesa za matumizi ya kikao alikuja ofisini kwangu. Alipoingia ofisini nilimuona mtu mwenye jicho la kutaka kusema kitu:
“Karibu shoga.”
“Asante, naona jana umeondoka na kutuzimia simu.”
“We acha tu nilichanganyikiwa sana.”
“Sasa ndiyo ukazima simu?”
“Niliona usumbufu hasa baada ya kuona simu ya bosi.”
“Ndiyo maana alinieleza nikutafute, nimepiga simu mpaka nimekoma kumbe umezima.”
“Shoga kikao cha ghafla kinahusu nini?”
“Si kile cha kuteua jina.”
“Jina! La nini?”
“Kweli Eflazia umevurugwa, si la kwenda kusoma nje.”
“Kikao si wiki ijayo?”
“Ni kweli kilitakiwa kiwe wiki ijayo, taarifa zilizofika jana zimesema masomo yataanza mapema hivyo mtu anayetakiwa kwenda aondoke Jumatano ya wiki ijayo.”
“He! Makubwa, unamaanisha bado siku nne tu?”
“Siyo nne, kikao hiki si kilitakiwa kukaliwa Ijumaa ya wiki kesho?”
“Ndiyo.”
“Basi baada ya kikao hiki jina litatoka baada ya kikao kwenye ubao wa matangazo japokuwa kila kitu kama nilivyokueleza. Baada ya hapo msafiri atatumia wiki kesho kujiandaa na Jumapili au Jumatatu saa saba usiku anaondoka.”
“Mmh! Sawa,” nilijibu kwa unyonge.
“Sasa shoga kuna vitu vinatakiwa kikao kinaanza saa mbili na nusu asubuhi hii.”
“Sawa basi.”
“Kuna mengi tutazungumza baadaye.”
Niliagana na Safia na kubakia ofisini nikiwa nimechanganyikiwa na kuona kama nataka kufanya mchezo kwa kupeleka majina ya watu watakaokuwepo kwenye kikao kwa vile isingesaidia kitu kwa vile kikao kitakuwa kimeisha na jina litakuwa limebandikwa na mwisho wa wiki itakayofuata mtu anaondoka.
Lakini bado sikutakiwa kuhukumu kwa kukata tamaa kurudia kosa la awali la kufanya tofauti na nilivyoagizwa na mzee Sionjwi na matokeo yake kwenda kinyume na mganga. Japo niliamini ilikuwa kazi ngumu ya kubadili matokeo lakini sikutakiwa kwenda kinyume zaidi ya kumpelekea majina anayoyataka nione uongo wake.
Japokuwa sikuwa na hamu ya kazi, nilijilazimisha kufanya kazi ili niimalize siku ile ambayo kwangu ilikuwa sawa na mwaka mzima. Nikiwa naendelea na kazi Safia alikuja na karatasi iliyokuwa na majina ya watu wa kikao cha bodi ambao walitakiwa kupewa posho baada ya kikao.
Kwangu ilikuwa kama bahati ya mtende kupata majina niliyokuwa nikiyatafuta bila Safia kujua kitu. Nilipiga foto kopi na kubaki na majina yale kisha niliandaa pesa za posho za kikao.
Baada ya kupiga mahesabu ya pesa wanayotakiwa kulipwa kwa ujumla nilimpigia mtunza fedha aliyekuja kuchukua karatasi ya malipo ili awalipe watakapomaliza kikao chao.
Baada ya kupata majina ya watu waliokuwa kwenye kikao cha bodi nililipitia karatasi lingine lililokuwa nyuma ambako pia ilikuwa mshangao baada ya kukuta kuna majina yetu watu watano tulioingia katika kinyang’anyiro cha mwisho.
Katika majina yale kulikuwa na wanaume watatu na wanawake wawili mmoja nikiwa mimi. Mwanamke aliyebaki niliamini ndiye aliyeteuliwa kwa upendeleo na mkurugenzi na rafiki yake. Nilichukua jina lake alikuwa akiitwa Happy Kinono, sikuwa na haja ya kuliandika pembeni kwa vile karatasi zile zilikuwa jibu la maswali yangu.
Niliamini chochote kinachotokea hakuna mtu atakayenishuku hata Safia asingejua kitu, ila niliamini kama ningemuulizia majina ya wajumbe na la msichana aliyeteuliwa na kikatokea kitu basi angeweza kujua mimi ndiye niliyefanya.
Nilijikuta nikipata furaha ya ajabu baada ya kupata kitu nilichokitafuta kwa muda mrefu na kukipata bila kumshirikisha mtu. Japokuwa kazi ya kubadili matokeo niliiona ngumu lakini kidogo moyo ulitulia na kufanya kazi yangu kwa utulivu.
Itaendelea wiki ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.