The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa Tamaa ya Cheo Kazini-30

0

ILIPOISHIA:

“Sasa ushindwe mwenyewe.”

“Sijawahi kushindwa na kitu cha kibinadamu, siwezi kudra ya Mungu lakini si ya mwanadamu wala majini sijawahi kushindwa.”

“Sasa babu leo ndiyo kikao kimekaa na jina tayari limepitishwa, unafikiri hapo kuna uwezekano?”

“Hii kazi ilikuwa iishe jana usiku lakini haikwenda tulivyotaka, japokuwa najua kazi iliyopo mbele yangu si ya kitoto sawa na kumrudisha duniani mtu aliyekufa kwa amri ya Mungu.”

SASA ENDELEA…

“Ni kweli babu ndiyo maana naona kuna ugumu .”

“Ugumu gani?”

“Kwa vile kikao tayari kimefanyika na jina limeshateuliwa, tutakuwa tumechelewa.”

“Mjukuu, hata kama angekuwa ameshafika chuoni hilo lisingenishinda, nilikuahidi utakwenda kusoma na cheo kitapanda, ahadi yangu ipo palepale.”

“Mmh,” kauli ya babu ilinifanya nigune.

“Mjukuu hii si kazi ngumu, zipo kazi nimeshaifanya ambapo niliyemfanyia haamini mpaka leo.”

“Kazi gani?”

“Ilikuwa kwenye uchaguzi mmoja, mteja wangu nilimfanyia dawa akashinda lakini aliwasahau wapiga kura wake, mwaka mwingine alipogombea alikuwa hakubaliki na mpinzani wake ndiye aliyekuwa akikubalika sana.”

“Ehe kitu gani kiliendelea?”

“Huwezi kuamini, hata mikutano yake ya kampeni alikuwa hapati watu, alipokuja alionesha kukata tamaa. Lakini nilimuahidi lazima atashinda na siku ya mwisho alishinda.”

“Mmh! Babu alishindaje?”

“Ni kweli mpinzani wake alishinda tena kwa kura nyingi, lakini siku ya mwisho nilibadili majina kwa njia nijuazo na msoma matokeo aliposoma alimsoma ameshinda.”

“Mmh! Hii kali, unataka kuniambia mpinzani wangu kama akifika chuoni nitawezaje kwenda kusoma au kuna nafasi nyingine itapatikana?”

“Walaaa, hiyohiyo tu.”

“Sasa nitaendaje?”

“Wewe unataka kwenda kusoma au kujua utakwendaje?” Swali la babu lilionesha kama kuchoshwa na mswali yangu ya kitoto.

“Hapana, nataka kwenda kusoma.”

“Basi kazi yote niachie mimi ili kesho ukitoka hapa ukajiandae kusafiri na safari hiyo utakwenda wewe siku ileile aliyotaka kusafiri huyo msichana.”

“Sawa babu,” nilikubali mdomoni lakini moyoni niliona kama haiwezekani, kama ingekuwa bado hakijafanyika kikao ningeona inawezekana. Lakini nilitakiwa kukaa kimya ili nije nione uongo wa mganga.

“Nina imani mambo yamekwenda vizuri!” babu aliniuliza.

“Ndiyo babu leo kila kitu kimekwenda vizuri.”

“Sasa yako umemaliza imebakia kwangu kukutengenezea maajabu ambayo hutokea ndotoni tu.”

Mzee Sionjwi alinyanyuka kwenda kilingeni kwake na kurudi na chungu nilichokuwa kimezungushwa sanda na shanga za rangi mbalimbali na kukiweka mbele yangu na kusema:

“Nipe kwanza majina ya viongozi waliokaa kikao.”

Nilinyofoa karatasi lililokuwa na majina ya viongozi wa bodi na kumpatia mzee Sionjwi ambaye alichukua karatasi na kuiweka kwenye chungu kilichokuwa na maji yaliyochanganywa na dawa. Baada ya muda alichukua kipande cha sanda alichokiweka kwenye maji yale kisha aliitoa karatasi ya majina na kulifunga kwenye sanda na kuiweka pembeni.

Aliniomba jina la yule msichana aliyechaguliwa kwenda kusoma, kwa vile karatasi ilikuwa na majina mengi, kila jina lilikuwa na picha mbele yake.

“Sasa babu karatasi hii ina majina na picha nyingi tutafanyaje?”

“Chana sehemu zenye majina mengine na kubakiza moja.”

“Sawa.”

Nilifanya vile kwa kuchana majina manne, kwa vile jina la mhusika lilikuwa la mwisho, niliyachana ya mwanzo na kuliacha jina moja linalotakiwa. Aliishika picha ya yule msichana na kuchukua kisu kisha aliipasua kichwani na kuweka dawa eneo la kichwa huku akisema maneno yake na kulitaja jina yule msichana.

 Baada ya kumaliza maneno yale alichukua kiberiti na kuichoma picha ile ambayo iliungua yote na kuchukua majivu yake kisha alitoa kitambaa cheusi na kuliweka jivu lile. Baada ya zoezi lile alibeba  vitambaa vyote viwili na kuniambia nimfuate.

Nilimfuata hadi nyuma ya nyumba kulikokuwa na mashimo madogo mawili.

Alichukua kitambaa kimoja chenye majina ya bodi ya uteuzi na kukiweka kwenye moja ya shomo na kumwagia dawa na kuyazika. Alichukua jina la msichana aliyeteuliwa alilokuwa amelifunga kwenye kitambaa cheusi nalo akalizika.

Baada ya zoezi lile alinieleza  nilifuate ndani ya kilinge, tuliingia ndani na kunieleza nikae chini na yeye alikaa kwenye kigoda mbele yangu na kuchukua karatasi nyeupe iliyokuwa na picha ya nyota na kalamu nyekundu na kunipa kisha aliniambia niandike jina langu  katikati ya picha ya nyota.

Nilifanya vile, wakati huo alikuwa ameisimamisha mishumaa minne mbele yangu na kuuwasha mmoja, ilipokolea moto alinieleza niichome ile karatasi kisha moto wake niiwashe mishumaa iliyobaki, nilifanya vile kwa kuiwasha yote na wakati huo karatasi yenye jina langu ilikuwa imewaka yote na kubakia jivu ambalo nilielezwa niliweke kwenye sahani.

Baada ya kumaliza zoezi lile alinieleza nikapumzike ili nijiandae na zoezi usiku kwa ajili ya kumalizia kazi iliyobaki na mimi kurudi mjini kujiandaa na safari ambayo kwangu bado niliona ni ndoto.

Itaendelea wiki ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply