Niliolewa na mganga kwa tamaa ya cheo kazini-30
ILIPOISHIA:
“Sawa babu ila…” nilijikuta nikishindwa kumalizia sentensi, nilianza kulia kitu kilichomfanya mzee Sionjwi kunisogelea na kunishika begani, Mmh! Makubwa ngozi yake kavu ya mkono ilipogusana na ya kwangu nilihisi msisimko wa ajabu.
“Una nini mjukuu?” aliniuliza kwa sauti ya kubembeleza.
“Sina majina uliyonituma.”
“Ha! Mjukuu, kwa sababu gani umekosa majina?”
SASA ENDELEA…
Huku nikilia nilimweleza sababu ya kutopata majina, baada ya kunisikiliza alinibembeleza na kuniambia:
“Mjukuu hakijaharibika kitu kwa vile muda bado unaweza kuondoka usiku huu ili uwahi kupumzika, ili kesho uamkie kazini na kupata majina yote kisha njoo nayo ili usiku wa kesho tufanye kazi. Huko Ulaya amini umeshaenda unasubiri kuambiwa.”
“Asante sana babu.”
“Basi mjukuu wahi ila kesho ukija usisahau ugonjwa wangu,” babu alikuwa akipenda sigara Embasy.
“Nitakuletea wala usiwe na wasiwasi na kesho nitakuletea vitu vingi.”
“Ndiyo maana nakupenda, nami nitaendelea kukufanyia maajabu ambayo toka niujue uganga sijamfanyia mtu. Siku zote mtu akikupa moja nawe usiwe mchoyo mpe tano.”
“Basi naomba uniamshie shoga yangu nimuage.”
“Mwache alale kwa vile kesho utarudi mtaonana.”
“Namjua lazima atanilaumu, hasa mwanamke akiwa kwenye hali ile hukasirika bila sababu ya msingi.”
“Basi twende ukamuage ndani maana yupo hoi.”
Niliongozana na mzee Sionjwi hadi chumbani alipokuwa amelala Rose, alimuamsha na kumfanya alalame.
“We mwanaume mbona huna huruma, mzigo wote huu ulionitwisha hunipi nafasi ya kupumzika.”
“Siyo hivyo bibie.”
“Siyo hivyo nini wakati mapenzi umegeuza chakula.”
“Bibie utanilaumu bure, siyo miye ni shogayo anataka kukuaga.”
“Mwambie aende.”
“Rose…Rose unasema hivyo wakati wewe ndiye ulisema nisiondoke bila kukuaga.”
“Ha! Kumbe shoga upo? Nilijua hiki kibabu kinanitania.”
“Ningekuwa kibabu ningekulaza kitandani?” mzee Sionjwi alijibu.
“We unatutafutia mada kesi, siku moja ufie kwenye kifua cha mtu,” Rose alijibu huku akikaa kitako kufikicha macho na kupiga miayo.
“Mmh! Ninyi waarabu wa Pemba siwawezi, sasa shoga nakuage Mungu akijalia tutaonana kesho jioni.”
“Nashukuru shoga, basi ukija usisahau nilivyokuagiza.”
“Ooh! Mwambie aende, haya ungemkumbusha saa ngapi?” mzee Sionjwi alimshushua Rose.
“Nawe unavishwa shanga unapenda mambo ya kike,” Rose alimjibu mzee Sionjwi.
Niliona malumbano ya waarabu wa Pemba yatanichelewesha , niliwaaga na kuwaacha wakirushiana vijembe. Kwa vile muda ulikuwa unaruhusu niliondoka mapema ili niwahi kupumzika ili kesho yake niwahi mjini.
Nilifika mjini majira ya saa saba kasoro usiku, kwa vile chakula cha usiku nilikula kijijini, nilipofika nilioga na kuiacha simu kwenye chaji kisha kupanda kitandani kuitafuta siku ya pili.
****
Siku ya pili niliamka kama kawaida na kwenda zangu ofisini nikiwa na kazi moja ya kuchukua majina ya watakaokaa kikao cha bodi pia jina la msichana atakayekwenda kusoma nje. Nilipofika ofisini nilikwenda ofisini kwangu huku nikijipanga kukabiliana na bosi wangu kwa kuondoka jana yake bila kuaga.
Kama kawaida nilitaka kumpigia simu Safia ili anipe ubuyu mpya japokuwa niliamini huenda ukazidi kuniumiza moyo. Kabla sijampigia, simu ya mezani iliita. Nilijiuliza nani anayeweza kunipigia simu asubuhiasubuhi, nilibeba mkonga na kuweka sambamba ya sikio na mdomo na kupokea.
“Haloo.”
“Haloo mhasibu,” ilikuwa sauti ya mkurugenzi.
“Abee bosi.”
“Vipi mama, mbona kimyaa?”
“Nilipatwa na dharura, shikamoo.”
“Marahaba, sasa mbona hukunijulisha?” aliniuliza kwa sauti ya upole.
“Kwa kweli nilichanganyikiwa, nilipigiwa simu na mlinzi wangu wa nyumbani kuwa kuna watu wamevunja nyumbani kwangu,” nilitengeneza uongo.
“Ooh! Pole sana basi ungetujulisha, nini kimeendelea?”
“Watu wale wamekamatwa namshukuru Mungu lakini hawakuchukua kitu.”
“Ooh! Afadhari, sasa ni hivi muone msaidizi wako kuna pesa unatakiwa kuidhinisha asubuhi hii kwa ajili ya kikao.”
“Sawa mkuu.”
Baada ya kukata simu, nilishusha pumzi ndefu baada ya uongo wangu kukubaliwa. Nilinyanyua simu na kumpigia msaidizi wangu ambaye alichelewa kidogo.
“Haloo Pili, njoo mara moja na maagizo uliyopewa jana.”
“Sawa dada Eflazia.”
Baada ya muda Pili aliingia na karatasi na kuniweka juu ya meza kisha alitoka. Nilizipitia haraka na kunionesha kunatakiwa pesa za kikao cha bodi, nilijiuliza kikao kile cha nini na mbona sikukijua mapema. Sikutaka kukihoji sana kwa vile kilikuwa hakinihusu.
Baada ya kuishinisha pesa nilimpa msaidizi wangu apeleke kwa mtoa pesa, nilipigia simu mkurugenzi amtume mtu akachukue pesa za kikao. Alimtuma Safia aje achukue, baada ya muda alifika kuchukua pesa za matumizi ya kikao. Alipoingia ofisini kwangu nilimuona mtu mwenye jicho la kutaka kusema kitu.
Je, anataka kusema nini? Usikose kufuatilia hadithi hii ya kusisimua katika Risasi Jumamosi siku ya Jumamosi.
Itaendelea Risasi Jumamosi.