The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na mganga kwa tamaa ya cheo kazini-39

0

ILIPOISHIA:

Nilikata simu ili niendelee na kazi lakini hamu yote ilikatika hasa nilipokumbuka kauli ya Safia kuwa hata nikikosa sitapungukiwa na kitu bila kujua jinsi gani nilivyoitafuta nafasi hiyo kwa udi na uvumba kufikia hatua ya kujidhalilisha kwa kiasi kikubwa. Kwa kauli ile ilionesha wazi hakuna safari.

SASA ENDELEA…

Nilijiuliza ile taarifa ya kushtua niliyoambiwa  nitaisikia jana yake ambayo niliamini ilikuwa ni ile ya mchumba wa meneja kugoma kusafiri lakini imekwenda kinyume. Matumaini yalikatika ghafla ya kujiona kama nimetwanga maji kwenye kinu na kupewa matumaini yasiyo na ukweli.

Niliwasha kompyuta ili nianze kazi, lakini moyo ulitumbukia nyongo, niliangalia kioo cha kompyuta lakini hamu sikuwa nayo kabisa, wazo lilikuwa niombe ruhusa kuwa naumwa ili nirudi kwa babu kumuuliza. Sikutaka kufanya kitu, niliamua kuizima kabisa.

Nilipitia mkoba wangu ili niende kuomba ruhusa niondoke zangu kwani mambo yalikwenda ndivyo sivyo. Nilipofika mlangoni simu ya mezani iliita, nilijiuliza niipokee au niachane nayo. Lakini niliona si busara kuiacha simu iite huenda ni mkurugenzi.

Nilirudi kwenye meza na kuchukua mkonga wa simu na kupokea.”

“Haloo.”

“Ooh! Eflazia upo?”

“Ni…ni…nipo bosi,” ilikuwa sauti ya mkurugenzi iliyonifanya nipate kigagaziko cha ghafla.

“Njoo mara moja ofisini.”

“Sawa nakuja.”

Kwa vile ndiyo nilikuwa nataka kutoka niliweka mkoba juu ya meza na kwenda kumsikiliza bosi. Nilipofika kwa katibu wake muhtasi, ambaye alikuwa shoga yangu Safia aliponiona alishtuka.

“Vipi shoga kwetu asubuhi asubuhi?”

“Mkuu kaniita.”

“Pita hakuna mtu.”

Niligonga mlango na kulakiwa na sauti nzito ya bosi.

“Pita ndani.”

Nilifungua mlango na kuingia, bila kukaa niliitikia na kusimama kusubiri kuelezwa nilichoitiwa.

“Eflazia kaa kwenye kiti.”

Nilifanya nilivyoelekezwa na kusubiri maelekezo, bosi alionekana yupo bize na kusoma moja za karatasi zilizokuwa mbele yake.  Nilikaa dakika kumi bila kuelezwa kitu chochote, baada ya kumaliza kusoma aliniita jina langu:

“Eflazia.”

“Naam bosi.”

“Kweli riziki ya mtu huwezi kuizuia bali utaichelewesha.”

“Ni kweli, unamaanisha nini?”

“Unajua nafasi ya wewe kwenda kusoma nje nilipendekeza mimi, lakini kikao cha bodi kilinishinda kwa hoja.”

“Sasa tatizo nini?”

“ Ndiyo maana nikasema riziki haizuiliki bali huchelewa.”

“Bado sijakuelewa.”

“Nafasi uliyoitaka umeipata.”

  “Nafasi ipi?”

“Ya kwenda kusoma nje.”

“Na aliyechaguliwa?”

“Anawaza mapenzi zaidi kuliko kazi.”

“Una maanisha?”

“Namaanisha kuwa yule msichana tuliyemchagua amegoma kwenda kusoma,  baada ya taarifa ile niliweza kuwasiliana na wenzangu tukutane leo ili tuteue mtu mwingine. Mmoja alitoa wazo tukuchague wewe nami niliunga mkono basi umepita hivyo mama jiandae na safari.”

“Etii?” nilimsikia lakini sikumwelewa nilikuwa kama nipo ndotoni.

“Umechaguliwa.”

“Ooh! Asante Mungu.”

Nilipiga magoti kumshukuru Mungu huku nafsi ikinisuta nikiamini haikuwa amri ya Mungu bali  kazi ya mzee Sionjwi ndiyo iliyobadili matokeo yale. Nilijua kabisa haikuwa hiyari yake Happy kuikataa safari adhimu kama ile bali kugeuzwa  mawazo na nguvu za kiza.

Nilikubaliana na mzee Sionjwi kuwa hashindwi na kitu kilicho nje ya kudra za Mungu. Nilishika mikono kifuani huku machozi yakinitoka kwa furaha, mkurugenzi alizunguka meza yake na kuja kuninyanyua na kunipigapiga mgongoni kunipongeza.

“Hongera kwa kuipata nafasi adhimu kama hii, nakuamini katika kazi yako na nidhamu yako nina imani utafanikiwa na Mungu akutangulie kwa kila jambo.”

“Amen, asante bosi.”

“Basi nikuache ukaendelee na kazi, kesho utamkabidhi msaidizi wako aendelee na kazi zako zote, ili kuanzia kesho kutwa uwe na mapumziko na kujiandaa na safari.”

“Asante sana bosi,” nilijibu huku nikifuta machozi ya furaha.

“Basi kamalizie kazi.”

“Sawa bosi,” nilitoka ofisini kwa bosi nikiwa nimechangangikiwa kwa furaha.

Nilijikuta nikimpita Safia bila kujua mpaka aliponishtua.

“He! Shoga kulikoni kunipita kama gogo kuna nini tena?”

Niligeuka kumtazama Safia aliyekutana na machozi kitu kilichozidi kumshtua na kutoka kwenye kiti chake na kuja haraka kunikumbatia akiamini nina matatizo.

“Jamani shoga yangu kuna nini tena?” Safia aliniuliza kwa sauti ya huruma.

“Hamna kitu.”

“Hapana niambie mpenzi.”

“Kweli, haya ni machozi ya furaha.”

“He! Furaha ya nini mpenzi?” aliniuliza huku akinishika mabegani na kunitazama usoni. Nilikutana na michirizi ya machozi  mashavuni kwake kuonesha jinsi gani matatizo yangu yanavyo ugusa moyo wake.

“Ile nafasi nimeipata.”

“Nafasi! Nafasi ipi?”

“Na kwenda kusoma.”

“Wewee! Kweli?”

“Kweli kabisa, nashukuru shoga Mungu amesikia maombi yetu.”

Tukijikuta tukikumbatiana tena kwa furaha, Safia  aliacha ofisi yake na kunisindikiza mpaka ofisini kwangu. Niliamini naye alikuwa na furaha kama yangu, nilimuomba akaendelee na kazi ili jioni tupate muda wa kuzungumza kwa kirefu.

Je nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika gazeti la Risasi Jumamosi siku ya Jumamosi.

Leave A Reply