The House of Favourite Newspapers

Niliolewa na Mganga kwa tamaa ya cheyo kazini-26

0

ILIPOISHIA:

Hata katika mazungumzo yetu hakugusia habari za mjini zaidi ya kusifia mapenzi anayopata toka kwa mzee Sionjwi, mtu aliyemuona ni kila kitu katika maisha yake. Pamoja na moyo wa mtu kupenda ni utashi wake, sikuamini kama mapenzi ya Rose kwa kizee kile yanatoka moyoni.
SASA ENDELEA…

Lakini wazo langu lilipingana kwa vile uhusiano wa Rose na mzee Sionjwi haukuwa wa ghafla bali ni watu walioanza muda mrefu toka wakati alipokuwa akinisindikiza. Siku zote nilibaki nikijiuliza maswali yasiyo na majibu kipi kimemvutia shoga yangu mpaka kukubali kuhama mjini na kuhamia shamba.

Ingekuwa mzee Sionjwi ni tajiri ningesema labda kafuata mali ya kizee kile ambacho kisingekaa muda mrefu kingejifia na yeye kupata sehemu ya mali ile. Lakini hakuwa na mali yoyote ya maana zaidi ya mashamba na vimifugo vichache, ningesema labda sura yake imemvutia lakini mzee alikuwa kituko, kama una moyo mwepesi ukikutana naye lazima avunjike mbavu sura yake kama ngedere.

Ila niliamini uwezo wa kimapenzi, mzee yule Mungu alimjalia kwa vile hata mimi nilionja ladha yake akimshika mwanamke lazima amuweke moyoni mwake. Lakini bado sikuona sababu ya kumtoa Rose mjini kwenye maisha mazuri kuhamia kijijini kwenye maisha kama yale.

Lakini bado niliyaheshimu maamuzi yake kwa vile kila mtu ana sababu ya kumpenda mtu, hata wanawake wazuri huwakimbia wanaume wenye pesa na kuwafuata wasio na kitu kutokana na kukidhiwa haja zao za mwili.

Mpaka kiza kinaimeza nuru ya mchana hakukuwa na dalili za kuonekana mzee Sionjwi, nilijua yaleyale ya kulala shamba. Sikuwa na matumaini ya kufanyiwa kazi yangu kwa vile ilikwenda tofauti na nilivyoagizwa zaidi ya kumueleza kilichotokea ili nijue atanisaidia vipi.

Pamoja na kumuamini katika kazi zake ya kutegua mabomu ya hatari kwa hatua iliyofikia ya yule msichana aliyechaguliwa kwa siri, hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kuelezwa nisubiri safari nyingine kitu ambacho sikutaka kukisikia kuwa nijiandae na safari.

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu, Rose aliniomba akajilaze ndani, alikuwa hajisikii vizuri.
“Shoga leo sijaamka vizuri na mzee mwenyewe alisema atarudi mapema mpaka sasa hivi sijamuona, naomba nikajipumzishe kidogo kitandani.”
“Hakuna tatizo.”

“Lakini usiondoke bila kuonana.”
“Lazima nitakuamsha.”
“Basi bakia na bibie akupe kampani.”
“Hakuna tabu.”

Nilibakia na mmoja wa mke wa mzee Sionjwi ambaye naye alikuwa mchangamfu kuliko wenzake. Pamoja na uchovu wa kutopumzika sikutaka kufumba jicho mpaka mzee Sionjwi atakaporudi ili nijue nitasuka au nitanyoa.
Mpaka saa tatu usiku alikuwa hajarudi.

Pamoja na kuzungumza na kucheka na mke wa mzee Sionjwi akili yangu ilikuwa mbali hasa baada ya usiku kuwa mkubwa na mwenyeji wangu haonekani. Nilijikuta nikiwaza jinsi mkurugenzi na meneja wa kanda kutuzunguka na kumpeleka mtu wanayemtaka.

Kiherehere chote kiliniisha mtoto wa kike na kuziona ndoto zangu za mchana kuwa mtu mkubwa katika kampuni yetu upande wa fedha zikiyeyuka. Kila nilipofika hapo moyo uliniuma na kutamani kulia kwa kupiga kelele lakini nilijikaza na kutulia.

Nilijiuliza nitakuwa nimekosea kitu gani kilichosababisha kuipoteza nafasi ile, niliamini kuna kitu nilikuwa nimekosea. Lakini nilikumbuka sikupewa sharti lolote zaidi ya kupeleka majina. Tukiwa katikati ya mazungumzo mzee Sionjwi aliingia. Alikuja moja kwa moja tulipokuwa tumekaa kwenye mkeka akiwa na kikapu na mfuko wa rambo.
“Jamani kumbe kuna mgeni?”
“Ndiyo babu, shikamoo.”

“Marahaba mjukuu, umefika zamani?”
“Toka saa kumi na moja.”
“Ooh! Kumbe muda, karibu sana.”
“Asante.”

Wakati huo mkewe alikuwa amempokea mizigo aliyokuwa nayo na kupeleka ndani na kutuacha wawili. Kabla ya kusema kitu alipaza sauti kutaka maziwa, mmoja wa wakeze alikuja na kibuyu cha maziwa. Ilionesha jinsi gani mzee yule alivyokuwa akiwanyanyasa wakeze, kama hayupo basi hakuna kulala mpaka arudi.
Itaendelea Risasi Jumamosi.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply