The House of Favourite Newspapers

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-2

0

Ilipoishia wiki iliyopita

“Nikaachana na kile kibanda kule Mburahati, nikafungua duka moja kubwa sana maeneo ya Tabata Bima, nikawa nauza vyakula na vitu vingine vingi vya nyumbani. Nikawa napata heshima mtaani, nikifika walipokaa watu, nilipishwa kiti, nilipata faraja na kuanza kuota ndoto za utajiri.”
Sasa endelea..

Kwa kweli maisha yalienda kwa kasi ambayo sikuitegemea kabisa, baada ya kuliimarisha sana lile duka langu la pale Tabata Bima, nikaweza kupata fremu zingine maeneo ya Buguruni ambako niliwaleta ndugu zangu kutoka Tabora wakawa wananisaidia kuuza, maana lilikuwa ni kubwa kidogo lililouza vifaa vya ujenzi kama simenti, mbao, misumari na mabomba ya maji.

Sasa lengo langu lilikuwa ni moja tu, kupata fremu katika eneo la Kariakoo, kwa sababu baadhi ya wajasiriamali wenzangu waliniambia kuwa endapo nitafanikiwa kupata hapo, basi nijihesabu tajiri ndani ya muda mfupi kwa sababu hakuna biashara ambayo inakataa katika eneo hilo.

Mke wangu alikuwa ndiye msimamizi mkubwa wa shughuli zangu na mimi kazi yangu ikawa ni kuzunguka kila sehemu kutafuta fursa zaidi ili tuendelee kuwekeza, niliamini kama tutaendelea na kasi yetu, basi mafanikio yalikuwa karibu. Ila baadhi ya rafiki zangu waliniambia ni tatizo kumuamini mwanamke katika utafutaji.

Walisema kuwa mara nyingi wanawake wakiona shughuli zinaenda sawa, wanaanza kuleta maneno kuonesha kuwa wao ndiyo sababu ya mafanikio na hutaka vilevile kuwa juu ya waume zao, kitu ambacho kwangu sikutaka kitokee, kwani pamoja na kumheshimu sana mke wangu, lakini suala la yeye kuwa juu ya shughuli zetu sikulipenda.

Hata hivyo, sikutaka kuhukumu, nilihitaji nione kama kweli akianza tabia hiyo, basi nijue namna ya kumdhibiti bado na mapema, maana nilijua maisha hayawezi kwenda sawa kama yeye atataka kuwa juu yangu, hasa kwa kuwa licha ya kunisaidia sana, lakini mimi ndiye hasa chanzo cha kila kitu.

Siku moja nilikuwa na rafiki zangu tumekaa sehemu moja mitaa ya Kinondoni, tukiwa tunabadilishana mawazo namna ya kukabiliana na maisha, mara mmoja wetu akatueleza kuhusu habari za machimbo, kwamba vijana wengi wanatoka kimaisha baada ya muda mfupi tu. Simulizi zilikuwa nyingi, lakini kwa kweli zilinivutia kiasi cha kushangaza sana.

Niliporudi nyumbani jioni ile, nikamwelezea mke wangu kuhusu mazungumzo yale na juu ya kiu yangu ya kutaka kwenda huko machimboni ili kujaribu bahati yangu. Ingawa mke wangu naye alikubaliana nami juu ya watu wengi kubadili maisha yao haraka wakitokea machimbo, lakini hakupendezwa na wazo langu la kwenda huko.

Tukajadili sana suala hilo, hatimaye tukakubaliana, kwamba mimi niende nikatazame nione kitu gani nitaweza kufanya nikiwa huko. Nikaanza taratibu za kwenda katika machimbo ambayo huyo rafiki yangu aliyasifia, alinielekeza huko Songea sehemu moja iliitwa Kitai, eneo la Masuguru.

Baada ya kumuachia maelekezo yote muhimu juu ya namna ya kuendesha biashara kipindi nikiwa sipo, nikapanda basi kuelekea Songea, alfajiri ya siku hiyo, miaka mingi iliyopita.

Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli katika toleo lijalo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

Leave A Reply