The House of Favourite Newspapers

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-5

0

Ilipoishia wiki iliyopita

Tukachukua chupa zetu na kuhamia sehemu mbali kidogo na watu, tukaanza kuzungumza yetu. Sasa endelea

Huyu jamaa kwa kumtazama, alionekana kuwa na maisha mazuri kunizidi, kwa sababu kila alipokuwa akija kununua madini, wengi walionekana kumheshimu, ikanipa ishara kuwa alikuwa mfanyabiashara mkubwa, mwenye mafanikio ya kutosha, hivyo nikawa makini kumsikiliza.

“Unaweza kunishangaa labda kwa nini nimekuita kando, nataka kabla sijakuambia lolote, nikuulize nini hasa malengo ya biashara unayoifanya, kwa sababu kwa muda mchache nimekuona kama mtu unayejituma sana kazini,” alianza kuniuliza huyo jamaa aliyejitambulisha kwangu kama Jerry White.

“Malengo yangu ni kuwa kama wewe kaka, maana unaonekana uko vizuri, mimi hii biashara siijui vizuri, ningependa sana siku moja na mimi nikawa nakuja kununua na kwenda kuuza huko Arusha na hata nje ikibidi,” nilimwambia huku nikinywa kinywaji changu taratibu.

“Watu wengi wanatamani kuwa zaidi yangu, lakini haya maisha yana siri kubwa sana, nimefurahi kuona jinsi unavyojituma, kama ungeweza twende wote Arusha ukaone wengine wanavyofanya hii biashara, au unasemaje?” Jerry White aliniuliza.

Nikakubali kwenda, lakini siyo safari hii, bali watakapokuja tena, kwani nitakuwa nimekusanya mzigo wa kutosha kwa ajili ya kuwauzia wao na mimi mwenyewe na kwenda nao. Tukakubaliana hivyo, tukarejea pale tulipowaacha wenzetu tukaendelea na unywaji hadi siku ilipomalizika.

Wiki mbili baadaye, Jerry White alikuja tena machimbo. Hata hivyo, siku zote nilikuwa nawasiliana naye, aliukuta mzigo wake na tukaondoka wote. Songea mjini nilihifadhi fedha zangu benki, nikabakia na kiasi kidogo, tukapanda ndege hadi Arusha. Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kupanda ndege, sikuwa na amani hadi tulipotua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kia.

Arusha mjini, tulifikia hoteli moja kubwa katikati ya mji na kwa kweli, kwangu ilikuwa ni mara ya kwanza kukaa katika eneo zuri kama hilo. Nadhani maisha haya ndiyo yalikuwa yanaanza, kwani malipo ya chumba licha ya kuwa makubwa, lakini nilikuwa naweza kumudu kukaa hata mwezi mzima bila matatizo.

Jerry White alikuwa mtu maarufu sana pale Arusha, kwani kila baada ya muda mfupi, wageni Wazungu kwa waswahili walikuja kumuulizia na kuzungumza nao. Alinisaidia na mimi kuuza madini yangu kwa bei nzuri sana, sikuwahi kufanya biashara yenye faida kubwa kama hiyo tangu nilipoanza kuuza madini.

Baada ya siku mbili, alinichukua na kunipeleka nyumbani kwake, sehemu ambayo aliniambia inaitwa Njiro pale Arusha. Sikuweza kuamini kama pale ni nyumbani kwa mswahili, ilikuwa nyumba nzuri, kubwa ikiwa imezungushiwa ukuta. Ndani kulikuwa na bustani, bwawa la kuogelea, sehemu ya kuchezea mpira wa meza, pool, vinywaji na vitu vingi ambavyo nilizoea kuviona kwenye nyumba za Wazungu.

Maisha yake yalikuwa ya juu sana, mkewe na watoto wake wawili kwa kuwatazama tu, walionekana wenye maisha mazuri mno. Alinitambulisha kwao, wakafurahi sana, hasa alipowaambia kuwa mimi ndiye hukusanya madini na kuwauzia kwa kule Songea. Nilichogundua ni kuwa Jerry White alikuwa akinunua madini pia Mererani, Mwanza, Dodoma na Morogoro.

Tukiwa kwenye bustani yake, tukinywa juisi, nilimuuliza mbinu hasa alizozifanya hadi kupata mafanikio aliyokuwanayo.

“Biashara ya madini ukitaka kufanikiwa usiizoee, kwa sababu inaambatana na mashetani, lakini ukijitoa, hakuna sehemu yenye hela ya uhakika kama madini,” aliniambia Jerry White, kauli iliyonishtua kidogo.

“Kivipi,” nilimwuliza.

“Ningekuambia, lakini huonekani kama unaweza kunielewa, ila kama nilivyokuambia, usiifanye biashara hii zaidi ya mwaka mmoja, utakachopata ndani yake hamishia kwenye shughuli nyingine, lakini ukiendelea nayo, kama hautapoteza hata ulichokipata, basi ni lazima ufanye kama nilivyofanya mimi,” aliniambia huyo jamaa.

Je, ni kitu gani? Jamaa atakubali atakachoambiwa? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli katika toleo lijalo.

Leave A Reply