The House of Favourite Newspapers

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-6

0

Ilipoishia wiki iliyopita

“Ningekuambia, lakini huonekani kama unaweza kunielewa, ila kama nilivyokuambia, usiifanye biashara hii zaidi ya mwaka mmoja, utakachopata ndani yake hamishia kwenye shughuli nyingine, lakini ukiendelea nayo, kama hautapoteza hata ulichokipata, basi ni lazima ufanye kama nilivyofanya mimi,” aliniambia huyo jamaa.

Sasa endelea…

Sikumwelewa. Nilimuuliza alikuwa na maana gani, ndipo akaniambia wazi kuwa biashara ile imempatia mafanikio makubwa sana, lakini hata hivyo ni baada ya kuamua kujitoa kwani alilazimika kutoa kafara kwa waganga. Nikaogopa sana maneno yake, sikuwa nimewahi kufikiria katika maisha yangu kama nitalazimika kumtoa mtu kafara ili kupata mafanikio.

Lakini huyu jamaa alinihamasisha sana, hasa baada ya kuona maisha yake. Aliniambia alikuwa anamiliki vitu vingi alivyopata kutokana na madini na mapato yake kwa mwaka yalifikia hadi shilingi bilioni moja.

Baadaye nikamwambia kuwa nilikuwa tayari kutoa kafara na akaahidi kunipeleka kwa mganga mmoja aliyesema alikuwa anapatikana sehemu za Ngende. Alisema kitu au mtu nitakayetakiwa kumtoa atachaguliwa na mganga mwenyewe. Licha ya hofu niliyokuwa nayo juu ya nani nitamtoa, lakini tamaa ya utajiri ilinifanya nijione mwepesi.

Tulienda huko Ngende baada ya wiki tatu, nikakutana na mganga ambaye alikuwa mzee sana na aliponiona tu, akaniambia hongera kwa kuchagua utajiri, lakini pole kwa kumpoteza mtu unayempenda. Kwa kuwa nilikuwa nimeshajipanga hata sikujali. Usiku, aliniambia niingie katika chumba kimoja chenye giza akaniambia nikae baada ya dakika kumi nitoke nikazungumze naye nje ya kibanda chake.

Nikiwa sielewi chochote, mara ghafla mbele yangu nikamuona mtoto wangu amesimama akiwa amejifunga shuka jeupe, nilishtuka sana. Nilitaka kupiga kelele, lakini nilipokumbuka nipo kwa mganga, nikajua huyo ndiye nitatakiwa nimtoe kafara. Wakati nafikiria hivyo ghafla mwanangu akatoweka giza likarejea tena.

Nikajua hicho ndicho alichotaka nione, nikafungua mlango na kutoka nje, ambako aliniuliza kama nipo tayari kukitoa kafara nilichokiona chumbani, nikatingisha kichwa kumkubalia. Yule rafiki yangu yeye alishaondoka kuendelea na shughuli zake, aliniacha na kuniambia nikimaliza nitarejea mwenyewe.

Nilikaa pale kwa mganga kwa muda wa siku mbili, siku ya tatu nikaondoka kurudi Dar es Salaam nikiwa na dawa nilizopewa, ikiwemo ambayo niliambiwa lazima nihakikishe amekunywa. Aliniambia akinywa hiyo dawa, atatoweka pale nyumbani, nikiona zimepita siku tatu bila kuonekana, nirudi kwa mganga kwani dawa zitakuwa zimekubali.

Siku ileile nikahakikisha mwanangu amekunywa ile dawa bila mama yake kujua, kwani tangu awali nilijua nikimshirikisha tu mama yake, kila kitu kingeharibika. Baada ya kuhakikisha amekunywa, nikaondoka kuelekea bar ili kupunguza mawazo kidogo.

Nilirejea usiku sana na sikutaka kuuliza kama mtoto alikuwepo au la. Asubuhi pia nikaondoka mapema sana, nikaondoka zangu kuelekea kwenye shughuli zangu zingine kwenye maduka niliyokuwa nayo Buguruni na Kariakoo.

Siku tatu zilipita lakini kijana wangu aliendelea kuwepo. Nikajiuliza kama nilikuwa nimekosea masharti, lakini nikaona nilifanya kila kitu kwa ufasaha kama nilivyoelekezwa.

Nikamtazama kijana wangu hakuonesha kama alikuwa na tatizo lolote. Nikajikuta naanza kuogopa, nikajishauri kesho yake lazima niende tena Ngende ili nikazungumze na yule babu.

Niliondoka asubuhi na mapema na nikafika siku hiyo hiyo jioni. Nyumbani kwa mganga kulikuwa na watu wengi waliokuwa wamekuja na magari yao, walionekana ni wale wa aina yangu. Aliponiona, akaniita pembeni na kuniambia ametambua kilichonipeleka na kwa maana hiyo nisubiri awapunguze watu.

Hadi usiku ulipoingia watu walikuwa bado wakiingia na kutoka, zamu yangu ilipofika, nikaingia. Akaniuliza kwa nini kijana wangu hakupotea kama alivyosema?-

Je, alimwambia nini? Usikose kufuatilia mkasa huu katika toleo lijalo.

Leave A Reply