The House of Favourite Newspapers

Nilitaka Kumuua Mwanangu Mara 3, Leo Ananisaidia!-8

0

Ilipoishia wiki iliyopita:
Kama niliyezinduka, nikajikaza na kujifanya kukasirika, nikamuuliza alikuwa na ujasiri gani kuniambia mambo ya ajabu kama yale mbele ya shemeji yangu, lakini tofauti na nilivyotegemea, wote wawili waliangua kicheko cha nguvu ambacho kilikuwa ni kama wananikebehi!
Sasa endelea…

Mke wangu na dada yake wakaacha kucheka, halafu mama watoto wangu akasema kuwa ninafahamu ninachotaka kufanya, kwa hiyo ni juu yangu kuamua, kwa sababu yeye hatakubali kuona mtoto wake akiondoka kirahisi namna ile na kwamba endapo nitamuua, basi nielewe nami uhai wangu hauko mbali.
Ukweli nilikuwa naujua, lakini nilishindwa kukubali moja kwa moja. Ili kupoteza lengo, nikajifanya kupandwa na jazba na kuuliza ni wapi alipo mwanangu, lakini wao waliendelea kuwa wapole na kuniambia kuwa mtoto alikuwa anapata matibabu na sitaweza kumuona hadi baada ya siku mbili, kwani mganga aliagiza hivyo.
Nikaondoka kwa hasira hadi nyumbani, aibu ikiwa imenijaa, sikuelewa mke wangu aliwezaje kufahamu juu ya harakati zangu, lakini nikajikaza kisabuni ili sakata hilo liishe. Akili hata hivyo haikukaa sawa, ina maana kukubali kushindwa ni kukubali maisha yaendelee kuwa magumu na kutimiza lengo ni kukaribisha utajiri.
Nikiwa nimejipumzisha kitandani chumbani, saa tisa hivi mke wangu alirejea akiwa amepandwa na jazba sana, akaanza kunifokea mara tu baada ya kuingia ndani. Alinishambulia kwa maneno akiniambia nimekosa shukurani kwa Mwenyezi Mungu, kwani hadi hapo nilipofika ni kwa juhudi zake, leo ninapata tamaa ambayo itaniangamiza.
Alisema siku zote mtu anayeshiriki ushirikina mwisho wake huwa mbaya na kwa sababu hiyo hataki tena kuendelea kuishi na mimi kwa vile nimeonesha dhamira mbaya, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuweza kumuua hata yeye.
Maneno yake sikuyategemea, lakini ndivyo ilivyokuwa. Nilijaribu sana kujitetea, lakini mke wangu hakuelewa lolote, vikao vya ndugu wa karibu vikakaa na yeye akadai talaka yake. Kitu ninachoshukuru ni kwamba wakati wa kudai talaka hakusema sababu halisi, bali aliwaambia ndugu zake kuwa amechoshwa na vitendo vyangu ambavyo hakuvitaja.
Baada ya mvutano wa karibu wiki mbili, hatimaye nikalazimika kutoa talaka na hivyo kugawana mali tulizochuma pamoja. Wakati wa mgawanyo wa mali nilitaka nipewe mtoto, lakini mke wangu alisema kitu hicho hakitatokea kabisa katika maisha yake, akisema nitakaa na mtoto huyo akishakuwa mkubwa na anayejitambua!
Kwenye mgawanyo, nilibaki na nyumba moja tu, kwani yeye licha ya kupata nyumba, alilazimika kuchukua pia na maduka mawili makubwa kwa kile wanafamilia walichosema ni kwa ajili ya kumhudumia mtoto katika maisha yake ya shule. Nikakubali, kwani nilijua ninao uwezo mkubwa wa kujinasua kimaisha.
Nilipomaliza suala la mgawanyo wa mali, niliondoka kwenda kwa yule mganga wangu wa Ngende, ambako nilipofika nilimweleza kilichotokea naye akaniambia kuwa katika ufanyaji wake wa kazi, hakuwahi kukutana na ugumu kama ule aliopata kwa mwanangu. Akanishangaza aliponiambia kuwa inavyoonekana, kuna jambo kubwa linaweza kutokea kama nitaendelea kumhitaji kijana wangu, akanishauri niachane naye.
Badala yake akasema anaweza kuniangalizia mtu anayeweza kuchukua nafasi ya mtoto wangu, nikakubali. Basi baada ya kuangaliaangalia kwenye vitu vyake, akajikuta akicheka aliponiambia, ni bora tu nifanye kazi kwa bidii bila kuhitaji nguvu za ziada, maana baada ya kuangalia, amegundua mtu mwingine anayenifaa ili nitajirike ni mke wangu, ambaye alisema anaonekana ana uwezo usio wa kawaida.
Kijasho kikanitoka. Nikafikiria jinsi gani ninaweza kufanya, nikaona hapa njia rahisi ni kurudi tena kwa rafiki yangu aliyenishauri kuhusu suala hili. Nikatoka kwa mganga na moja kwa moja nikaelekea Masuguru, ambako nilitaka nikapate ushauri mpya, kwa sababu bado nilihitaji utajiri!

Je, nini kitatokea? Usikose kufuatilia mkasa huu wa kweli katika toleo lijalo.

Leave A Reply