The House of Favourite Newspapers

Nilivyoivunja Ndoa Yangu na Shetani – 10

0

ILIPOISHIA:

 

 Siku hiyo sikulala mawazo yote yalikuwa juu ya tukio lililonitokea lilikuwa tukio la pili. La kwanza nilipata kipigo na mpenzi wangu ambaye alivunjwa mbavu na kuwapoteza watu muhimu kwangu, Bantu na Abdul. Lakini la siku ile lilikuwa kubwa. Nilikuwa napoteza maisha ya bwana wangu ambaye najua familia yake ingeathirika kwa namna moja au nyingine pamoja na mimi mwenyewe.

 

SASA ENDELEA…

 

 Nilijua  kama nitaendelea na mwendo ule lazima mwanajeshi ataendelea kunitafuta na akinikamata lazima animwage ubongo. Ilibidi nibadili tabia yangu ambayo mwenendo wake unatishia maisha yangu. Lakini sikutaka kuachana na waume za watu kwa kujua wengi niliokuwa nao ni wastaarabu.

Niliamua kubadili mtindo wa kukutana nao nyumbani kwangu kwa kujua nitakuwa nimejiepusha na yule mwanajeshi ambaye dhamira yake ilikuwa mbaya kumkataa ilikuwa nongwa kama angekuwa mstaarabu kama wenzake nisingekuwa na haja ya kumkataa. Eti nimesababisha  maisha yake yayumbe.

Kama siyo alipima injini ya pikipiki kwenye samitela kama siyo kuipasua injini ni nini. Mwanaume aliyetaka kula raha na mimi alitakiwa asiwe na fedha za mawazo za mkopo au kusubiri mwisho wa mwezi lazima utachemsha na kuniona mwanga wako kama mwanajeshi.

Mpango wangu wa kukutana na mabuzi yangu kwangu ulikwenda vizuri kwa kila mmoja kuja kwa wakati wake na siku ambayo atapangiwa. Kwa kweli nilijikuta kumbe mpango ule ningeutumia mapema mbona masaibu ya kutokea kwenye tundu la sindano yasingenikuta.

Mambo yaliniendea vizuri, sikuwa na presha tena pesa ziliingia kama maji kwa vile kila mwanaume aliyekuja kwangu alichanganyikiwa kunikuta mtoto wa kike nipo sawa hata fedha waliotaka kuniachia waliiacha kulingana na hadhi yangu pia hata penzi alilopata lilikuwa geni machoni mwake.

Niliamini mwanajeshi kila kukicha alizunguka kwenye mabaa na hoteli kunisaka ili animwage ubongo. Kwa mtaji ule nilijua  angeng’aa macho mpaka yaote kengeza kwa kunitafuta. Nilishukuru wakati wa penzi letu sikuwahi kumuonesha  kwangu, mbona ningekoma!

****

Nakumbuka siku moja nikiwa natoka kufanya shoping, super market nilivamiwa na watu ambao waliniteka na kuniingiza kwenye gari na kuondoka na mimi. Mmh! Moyoni nilijua lazima watakuwa wametumwa na mwanajeshi kama itakuwa yeye nilijua nimekwisha, niliamini kabisa ningerudi jina.

Nilifungwa kitambaa usoni na kushindwa kuelewa napelekwa wapi na kwa nini wameniteka. Kila nikiwauliza kosa langu nini niliambiwa:

“Acha kelele, utalijua muda si mrefu.”

Sikuwa na la kuongeza zaidi ya kutulia kusubiri kujua kilichofanya wanitendee kitendo cha kigaidi. Baada ya mwendo mfupi gari lilisimama na kuamriwa kuteremka. Baada ya kuteremka nilishikwa mkono na kupelekwa ndani ya nyumba.

Nilipofikishwa ndani nilifunguliwa kitambaa usoni na kuona nilipopelekwa. Mbele yangu kulikuwa na akina mama zaidi ya watano waliokuwa wageni machoni mwangu. Nilikalishwa chini kwenye zuria.

Baada ya kimya kifupi mmoja wa wale akina mama alisema:

“Vijana mmefanya kazi nzuri, leo ndiyo siku huyu kibaka wa waume za watu atajua kuwa mume wa mtu ni sumu.”

Kauli ile ilinishtua na kujua nimekwisha mtoto wa kike, baada ya kuongea vile hapo ndipo nilipopata wazo huenda hawa ni wake wa wale wanaume ninaowachuna.

“Konso,” alinigeukia na kulitaja jina langu.

“Abee,” niliitika kwa unyenyekevu.

“Unatujua sisi?”

“Hapana.”

“Basi sisi ni wake wenzio ambao tunashea bwana mmoja, ila wewe umezidi kwa kutuchanganya kwa mabwana wengi.”

Sikujibu kitu, kusikia vile moyo ulinipasuka na kujua ipo kazi.

“Sasa leo najua itakuwa mwanzo na mwisho wa kuchukua waume zetu na kujua maana halisi ya cha mtu hakifai,” alisema mwanamke mmoja aliyekuwa amejaza juu chini kama kapigwa pasi, moyoni nilijisifia na kuona bwana yake alikuwa na haki ya kuchanganyikiwa na mimi.

“Jamani sikujua kama waume zenu naomba mnisamehe,” nilijitetea.

“Hivi Konso umri wa waume zetu  unaona bado vijana, usituone hivi tumekutafuta kwa muda mrefu mpaka kukutia mkononi. Pamoja na kutuchukulia waume zetu umekuwa ukitukashifu kuwa hatujui mapenzi. Hivi wewe ingekuwa unajua mapenzi ungekuwa kishata mtaa kuchukuwa waume zetu si ungeolewa  na kuwekwa ndani?

“Wewe ni mwanamke gani kama msala wa kituo cha basi kila abiria anajisaidia halafu unajiita mzuri tena unayajua mapenzi. Kwa uzuri kweli mzuri hakuna kati yetu anayekufikia pia tuna imani mapenzi unayajua lakini ulitakiwa kumfanyia mume wako si mume wetu. Hivi tukiachika na uzee huu twende wapi, unajua ndoa zetu zimedumu miaka mingapi halafu wewe utuharibie?” alihoji mama aliyejifunga mtandio kiunoni.

Je, kilifuatia nini? Usikose wiki ijayo kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply